HANDENI MJI YAELEMISHA UMUHIMU WA LISHE BORA KWA WAVIU

December 01, 2025

Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Esther Herman,akizungumza na wananchi leo Disemba Mosi,2025 katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika kata ya Msasa mjini Handeni.

Na Mwandishi Wetu, Handeni

Halmashauri ya Mji Handeni imehamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kama nguzo muhimu katika kudhibiti maambukizi na kuimarisha afya, hususan kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU).

Akizungumza na wananchi Desemba mosi, 2025, katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika kata ya Msasa mjini Handeni, Ofisa Lishe wa Halmashauri hiyo, Esther Herman, amesema lishe bora ina mchango mkubwa katika kuongeza uimara wa kinga ya mwili na kusaidia watumiaji wa dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (ARV) kustahimili matibabu kwa ufanisi zaidi.

“Lishe bora si suala la hiari, ni msingi wa afya kwa kila mtu, lakini kwa watu wanaoishi na VVU ina umuhimu wa pekee. Ulaji wa mlo kamili huongeza nguvu, hupunguza makali ya magonjwa nyemelezi na kuimarisha mwili kupambana na maambukizi,” amesema

Amesema Halmashauri imetoa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya vyakula vyenye virutubisho, mbinu za kuboresha afya ya mwili, pamoja na uelewa juu ya nafasi ya lishe katika kupunguza hatari za kudhoofika kwa kinga.

Katika maadhimisho hayo yenye Kauli mbiu: “ Imarisha Mwitikio, Tokomeza UKIMWI.” yameandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa afya, yakilenga kuongeza mwamko wa wananchi kujua hali zao, kuzingatia kinga, na kushiriki kikamilifu kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Wananchi wamepata huduma mbalimbali ikiwemo ushauri nasaha, vipimo vya hiari vya VVU, elimu ya afya ya uzazi, na uhamasishaji kwa vijana kuongeza ushiriki katika kampeni za kutokomeza UKIMWI nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »