WATENDAJI WA TUME YA MADINI WATEMBELEA MGODI WA GOD MWANGA

October 17, 2025



Makamishna wapongeza uwekezaji mkubwa wa mgodi


TANGA


Makamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi, wameongoza kikosi cha watendaji wa Tume ya Madini wakiwemo Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa katika ziara ya kutembelea Mgodi wa  Madini ya Kinywe (Graphite) wa God Mwanga uliopo wilayani Handeni, mkoani Tanga. 

Ziara hiyo, iliyofanyika Oktoba 17, 2025, imelenga kujionea shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini zinazofanywa na mgodi huo.


Ziara hiyo ni sehemu ya mikakati ya Tume ya Madini ya kufuatilia utekelezaji wa shughuli za madini nchini, kuhakikisha wachimbaji wanazingatia sheria, kanuni na taratibu, pamoja na kuhakikisha usalama wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji.


Makamishna wa Tume ya Madini wamesema wamefurahishwa na uwekezaji mkubwa wa kampuni hiyo na kuhimiza Tume ya Madini kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika madini ya kinywe (graphite), hasa ikizingatiwa kuwa mahitaji ya madini hayo duniani ni makubwa. Aidha, wamesisitiza umuhimu wa kuongeza viwanda vya uchenjuaji wa madini nchini.



Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa God Mwanga Gems Ltd, Godlisten Mwanga, amesema mgodi wake  umepiga hatua kubwa tangu kuanza shughuli za uchimbaji wa madini na kuomba Serikali kuendelea kutangaza madini ya kinywe yanayopatikana kwa wingi mkoani Tanga ili kusaidia kupanua masoko ya kimataifa.

“Mahitaji ya madini ya kinywe ni makubwa duniani. Tuna uwezo mkubwa wa kuzalisha madini yenye ubora wa hali ya juu. Tunaamini kuwa endapo Serikali itaendelea kuyatangaza, tutapanua masoko, kuongeza mchango kwenye mapato ya Serikali na kutoa ajira nyingi zaidi,” amesema Mwanga.

Meneja wa Mgodi wa God Mwanga, Henry Mbando, ameeleza kuwa kampuni ya God Mwanga  ilisajiliwa rasmi mwaka 2012 ambapo kwa mkoa wa Tanga, walianza rasmi shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya kinywe mwaka 2021.

Mbando amesema kuwa kwenye kiwanda cha kuchenjua madini ya kinywe, kina uwezo wa kuzalisha tani 700 za madini kwa siku, ingawa kwa sasa huzalisha tani 350 zenye ubora wa asilimia 97. 

Amesisitiza kuwa kampuni imejipanga kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 1,000 kwa siku na kuwa miongoni mwa wazalishaji watano wakubwa wa madini ya kinywe duniani.

Akizungumzia utunzaji wa mazingira, Mbando amesema: “ Mgodi  umekuwa mstari wa mbele kulinda mazingira kwa kupanda miti kwenye maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za uchimbaji, kutumia maji kidogo katika uzalishaji, kudhibiti kemikali kwa usalama, na kufuata mafunzo kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.”

Aidha, kampuni hiyo imechangia maendeleo ya jamii kwa kujenga Kituo cha Afya cha Kwa Msisi, madarasa 10 katika shule mbalimbali, kuboresha miundombinu ya barabara, na kutoa ajira 625 kwa Watanzania. Pia imekuwa ikishirikiana na wadau wakiwemo Tume ya Madini, Halmashauri na taasisi nyingine katika kuboresha huduma za kijamii.



God Mwanga Gems Ltd inatajwa kuwa kinara wa kimataifa katika uzalishaji na usafirishaji wa madini ya viwandani, huku ikitangaza Tanzania kwenye ramani ya dunia kupitia ubora na uadilifu. Dira yake ni kubadilisha sekta ya madini kuwa nguzo ya uwezeshaji na ustawi wa Taifa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na utaalam wa ndani.

Kupitia mbinu zake zinazolenga tija, kampuni hiyo huchimba kwa umakini, husafisha kwa umahiri, na huzalisha madini yenye ubora wa kimataifa, ikiwakilisha kituo cha kuaminika kwa mahitaji yote ya madini nchini.



Tume ya Madini inaendelea kufanya ziara katika migodi mbalimbali nchini ili kufuatilia maendeleo ya sekta, kuimarisha uwajibikaji na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji na jamii.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »