NMB YAGUSA MAISHA GEREZANI,SAAD MASAWILA NA TIMU YAkE WATOA MSAADA GEREZA LA SAME

October 11, 2025


Na Ashrack Miraji 


Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Meneja wa Benki ya NMB tawi la Wilaya ya Same, Saad Masawila, ameongoza timu ya wafanyakazi wa benki hiyo kutembelea Gereza la Wilaya ya Same, ambapo walitoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wafungwa na uongozi wa gereza hilo.


Ziara hiyo iliyofanyika mapema wiki hii ilikuwa ni sehemu ya juhudi za NMB kuonyesha mshikamano na kuunga mkono jamii, hasa makundi yenye uhitaji maalum. Mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na sabuni, dawa za meno, taulo, pamoja na vifaa vya usafi.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya makabidhiano, Masawila alisema kuwa benki ya NMB inatambua umuhimu wa huduma kwa jamii, siyo tu kwa wateja wao wa kila siku, bali pia kwa makundi yanayosahaulika kama wafungwa. Alisisitiza kuwa ni wajibu wa taasisi zote kuonyesha ubinadamu na kusaidia sehemu ambazo msaada unahitajika zaidi.


Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka duniani kote na taasisi mbalimbali, ikiwa ni nafasi ya makampuni kuthibitisha dhamira yao kwa wateja na jamii kwa ujumla. NMB ikiwa ni miongoni mwa benki kubwa nchini, imekuwa mstari wa mbele kushiriki kwa vitendo katika kuleta maendeleo ya kijamii.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »