MWENYEKITI WA CCM NA RAIS MSTAAFU DKT. KIKWETE AHITIMISHA KAMPENI ZA UCHAGUZI KATIKA MAJIMBO MATANO YA ZANZIBAR

October 23, 2025







Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo amehitimisha rasmi kampeni za uchaguzi kwa majimbo matano ya Zanzibar, akiwataka wananchi wa pande zote mbili za Muungano kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29 kupiga kura kwa amani, umoja na utulivu.

Dkt. Kikwete alihitimisha kampeni hizo katika mkutano mkubwa wa wa hadhara uliofanyikia katika uwanja wa Skuli ya Ghana jimbo la Uzini Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini na Shehia ya Kiboje, na kuhitimisha kampeni za majimbo ya Tunguu, Chwaka na Uzini katika Wilaya ya Kati, pamoja na majimbo ya Paje na Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja.



Akihutubia mkutano huo, Dkt Kikwete amesisitiza kuwa wananchi hawana sababu ya kuwa na wasiwasi, kwani Tanzania inasifika kwa utamaduni wa uchaguzi wa amani, uliosimama katika misingi ya demokrasia, uadilifu na umoja wa kitaifa.

Dkt. Kikwete amesema ana imani kubwa kuwa wagombea wa CCM wataibuka na ushindi kutokana na utekelezaji wa Ilani wa chama hicho kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 85.

“Asilimia 15 zilizosalia ni miradi ambayo utekelezaji wake unaendelea. Yaani kazi imeshaanza. Hii inathibitisha msemo wetu kwamba ‘CCM ikiahidi, inatekeleza,’” alisema kwa msisitizo, akipigiwa makofi na wananchi.



Amesema Ilani ya CCM imeendelea kudumisha misingi ya uhuru, umoja, amani na utulivu wa nchi, huku akiwataka wananchi kuendelea kuilinda amani hiyo ambayo ni tunu ya taifa.



“Tanzania ni nchi yenye utulivu na usalama. Wapo waliowahi kujaribu kuivuruga amani hiyo, lakini hawakufaulu, na hawatafaulu sasa. Rais na Amieri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan mwenyewe amewahakikishia Watanzania kuwa hakutakuwa na vurugu wala maandamano katika kipindi hiki cha uchaguzi,” aliongeza.



Dkt. Kikwete alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar, uchaguzi wa viongozi hufanyika kila baada ya miaka mitano, na mwaka huu, Oktoba 29, Watanzania watapiga kura kuchagua Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.



“CCM ina wagombea katika ngazi zote – kuanzia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa Zanzibar, pamoja na wagombea wote wa ubunge, uwakilishi na udiwani katika kila jimbo, kata na wadi. Hii ndiyo nguvu ya chama chetu,” alisema Kikwete.



Akiendelea kueleza falsafa ya chama hicho, alisema CCM imekuwa na utamaduni wa kutoa Ilani ya Uchaguzi kila baada ya miaka mitano, ikieleza ahadi na vipaumbele vya chama vitakavyotekelezwa na serikali zake endapo kitapewa ridhaa.



“Ilani ndiyo mkataba kati ya CCM na wananchi. Huo ndio mwongozo wa viongozi wetu wanapotekeleza majukumu yao. Hata hivyo, wagombea hawazuiliwi kuongeza mambo mapya kulingana na mahitaji ya wananchi,” alifafanua.



Akitolea mifano, Dkt. Kikwete alisema viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Hayati Rais Benjamin Mkapa, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, na hata yeye mwenyewe, waliwahi kutoa ahadi nje ya Ilani kutokana na maoni ya wananchi waliokutana nao wakati wa kampeni.

“Ahadi ni deni, na wananchi hawasahau. Ni kama msemo ule wa ‘mla kunde husahau, lakini mtupa maganda hasahau,’” alisema kwa tabasamu.



Dkt. Kikwete pia alitoa pongezi maalumu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendesha kampeni kwa uwazi, ukweli na ufasaha.



“Wananchi wanapenda kiongozi anayesema ukweli. Anayeonyesha mafanikio yaliyopatikana na kukiri changamoto zilizopo huku akieleza mipango ya kuzitatua. Huyo ndiye Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanamke jasiri, mkweli na mwenye dira ya maendeleo,” alisisisitiza





Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi chake cha uongozi, akisema kuwa ametekeleza miradi mingi mipya ambayo haikuwa hata kwenye Ilani ya CCM.



“Dkt. Mwinyi ameleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kiutawala Zanzibar. Hii ni ishara ya kiongozi mwenye maono na anayejali wananchi wake,” alisema.



Dkt. Kikwete alimaliza kwa kuwataka wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania Bara kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi, kupiga kura mapema, na kuhakikisha kuwa amani inatawala katika kila hatua ya zoezi hilo.



Tanzania ni yetu sote, na amani yake ni jukumu letu sote. Tuwaheshimu viongozi, tuwapigie kura kwa utulivu, na tushiriki katika kuimarisha demokrasia yetu,” alihitimisha huku akishangiliwa kwa vifijo na nderemo.



Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »