SERIKALI KUJENGA MTANDAO MKUBWA WA MABOMBA YA GESI -DKT .BITEKO

March 06, 2025


📌 *Asema lengo ni kurahisisha huduma kwa wananchi*


📌 *Afanya mazungumzo na Kampuni ya Rashal Energies inayojenga Bomba la Gesi Kisemvule- Mbagala*


📌 *Aikaribisha Kampuni ya CNOOC ya China kushiriki Duru ya Tano Vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Rashal Energies, Farhiya Warsame ambayo inajenga Bomba la Gesi kutoka Kisemvule hadi Mbagala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya vituo vya  kujazia gesi kwenye magari (CNG) na viwanda.


Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe Machi 6, 2025 kando ya Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) linalofanyika kwa  siku tatu  jijini Dar es Salaam.


Dkt. Biteko amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwa na mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi  pamoja na vituo vya kujazia gesi kwenye magari ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.



Kutokana na hilo Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotaka kuwekeza kwenye kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Bi.Farhiya Warsame amemshukuru Dkt. Biteko kwa miongozo yake ambayo imepelekea kampuni hiyo kuanza kutekeleza mradi huo.

Ameeleza kuwa wananchi wameonesha mwamko mkubwa kwenye kuendesha vyombo vyao vya usafiri kwa kutumia gesi asilia badala ya mafuta kutokana na gesi asilia kuwa na gharama nafuu kuliko mafuta.


Vilevile, Dkt. Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Rock Mountain ya nchini Canada, Bw. Nick Lenstra ambayo imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya kuanza kazi za upembuzi yakinifu na kuzungumza na wadau wa ndani ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ili kutumia gesi asilia kutengeneza nishati kwa njia ya kimiminika ambayo inaweza kutumika kwenye ndege. 

Hali kadhalika, Dkt.Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa kampuni ya CNOOC kwa upande wa Uganda, Wang Juteng ambapo pamoja kuzungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini, ameikaribisha kushiriki Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia nchini.


MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »