📌 *Asema Serikali itaendelea kuwawezesha wazawa kushiriki miradi ya nishati*
📌*Asema sekta ya nishati imepiga hatua kubwa*
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza waheshimiwa wabunge kwa kuihimiza Serikali kuendelea kuwezesha wazawa kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya sekta ya nishati.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Machi 24, 2025 wakati akijibu hoja za wabunge katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu randama ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/26 kilichofanyika bungeni Dodoma.
“ Nakubaliana na wabunge kuhusu kuangalia wazawa na kuwapa nguvu ili waweze kushiriki katika miradi ya nishati, tumekuwa tukifanya hivyo lakini tutaendelea kuangalia wazawa wenye uwezo ili tufanye nao kazi. Ninawashukuru sana waheshimiwa wabunge kwa kuwasemea Watanzania ili washiriki katika miradi,” amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa licha ya kuwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Serikali itaangalia zaidi namna ya kusaidia wazawa katika sekta ya nishati, huku akitolea mfano hatua iliyopigwa katika sekta hiyo.
Amesema kuwa kwa sasa Serikali imeliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwa na uwezo kuzalisha na kusambaza umeme nchini kwa kuimarisha mifumo na miundombinu mbalimbali.
“ Mwaka huu unaopita Watanzania 53,000 wamepata ajira katika sekta hii. Tumepokea pia maoni ya waheshimiwa wabunge kuhusu uwepo wa wazawa kwenye kila kampuni inayopewa kazi na kuangalia upya mfumo wa utoaji zabuni,” amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa mara baada ya kukamilisha mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere, Serikali inaanzisha miradi mipya ya kuzalisha umeme kwa kuwa mahitaji ya juu ya umeme yamekuwa yakiongezeka hadi kufikia megawati 253 mwaka 2025.
Aidha, kupitia kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Mathayo David kimejadili kuhusu randama ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/26.
EmoticonEmoticon