MKUU WA CHUO CHA IFM APONGEZWA KWA KUBUNI MIKAKATI MBALIMBALI

December 16, 2024

 Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Benk ambaye pia ni mwanajumuiya wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM) (Alumni) Abdulmajid Nsekela amempongeza Mkuu wa chuo hicho Profesa Josephat Lotto na timu yake kutokana na kubuni mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.


Nsekela ameyazungumza hayo wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya wanafunzi waliosoma zamani katika chuo hicho ,iliofanyika usiku wa kuamkia leo jijini Dodoma.

Nsekela amesema mkakati wa kushawishi wanafunzi wapende somo la hisabati lakini pia kukifahamu chuo hicho ni mzuri kutokana na kwamba utaongeza wigo wa wanafunzi kujiunga na chuoni hapo kusoma kozi mbalimbali zinazotolewa.

Aidha alisema wao kama Alumni watashirikiana pamoja na IFM ili kuhakikisha chuo hiko kinazidi kutanua wigo wa utoaji elimu ndani na nje ya nchi ili kuzalisha wataalamu wengi wa masuala ya fedha.

"Nampongeza mkuu wa chuo kutokana na kubuni mikakati mbalimbali ya kuboresha chuo hiko,"alisema Nsekela.

Kuhusu fedha milioni 52.8 zinazohitajika kwa ajili ya mkakati wa kupeleka conter book shuleni ili kushawishi wanafunzi kupenda kusoma hisabati na kuifahamu IFM,Nsekela aliendesha harambee kwa Alumni hao,ambapo ahadi zilipatikana shilingi milioni 36,huku fedha tasilimu zilipatikana shilingi milioni nane.

Kwa upande wa Mkuu wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),Profesa Josephat Lotto amewaomba Alumni waliosoma katika chuo hiko,ambao wapo katika ofisi mbalimbali,kuhakikisha wanawasimamia wanafunzi wanaoenda kufanya mafunzo kwa vitendo ili kupata uzoefu,badala ya kuwatuma kukoroga chai na kubeba mafaili.

Profesa Lotto amesema wanafunzi hao wanapoenda katika ofisi mbalimbali kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo ya fani walizosomea wengi wanaishia kutumwa mafaili na kukoroga chai jambo linalopelekea kushindwa kupata kile alichokusudia na kurudi chuoni akiwa hana kitu.

"Hili suala linasikitisha sana kwa sababu wanafunzi wanarudi chuoni wakiwa hawajapata kitu,naomba nyie kama alumni mliopo katika ofisi mbalimbali kuwasaidia wanafunzi hao ili wakihitimu waweze kuajirika au kujiajiri wao wenyewe,"alisema Profesa Lotto.

Alisema wao kama wadau,wakiamua kuwasimamia wanafunzi hao,basi itachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi hao,kupata uzoefu wa kutosha na kufanya vizuri hapo baadae katika sehemu ya vitendo watakapoajiriwa au kujiajiri wao wenyewe.

Kutokana na hilo,ametoa rai kwa alumni wa IFM kuwa sehemu ya mkakati wa chuo hiko wa kuanzisha platform ambayo itahusisha waajiliwa waliomaliza IFM kutoka taasisi tofauti,pamoja na wanafunzi ili kuwasaidia kufanya majaribio kupitia platform na kupata kile walichokusudia.

"Wanafunzi waliofikia muda wakwenda kufanya mafunzo kwa vitendo,wataingia kwenye platform hiyo pamoja na waajiri,hii itakuwa imesaidia kufanya majaribio kwa vitendo kupitia platform,"alisema Profesa Lotto.

Mbali na hilo alisema katika kuisapoti serikali kuzidi kuinua kiwango cha elimu hapa nchini,Chuo cha IFM kimebuni mkakati wa kupeleka madaftari yaliyo na nembo ya chuo hiko,katika shule mbalimbali hapa nchini,ili wanapohitimu wajue kuna chuo hiko.

Profesa Lotto alisema lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kuwashawishi wanafunzi kupenda somo la hisabati ambalo katika kozi nyingi zinazotolewa hapo ni lazima somo hilo lisomwe.

Alisema kwa kuanzia wameanza na shule 184 kutoka wilaya 40 za mikoa sita,ambapo alisema wanahitaji sh milion 52.8 ili kufanikisha mkakati huo wa kushawishi wanafunzi wapende somo la hisabati

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »