DKT.KAZUNGU AKAGUA MAENDELEO YA MRADI WA UMEME WA JNHPP

December 28, 2024


📌 *Asema ni chanzo kikubwa cha ukuaji wa uchumi nchini*


📌 *Apongeza kazi kubwa iliyofanyika katika mradi huo*


📌 *Mradi wafikia asilimia 99.5*


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu ametembelea mradi wa kufua Umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115kwa ajili ya kukagua hatua ya utekelezaji wa mradi.


 Akiwa katika eneo la mradi,  Rufiji mkoani Pwani, Dkt. Kazungu ametembelea maeneo yote ya mradi huo na kushuhudia kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).

Dkt. Kazungu amesema kuwa mradi huo ambao sasa unaingiza zaidi ya megawati 1000 kwenye gridi ya Taifa ni chachu kubwa katika kukuza uchumi wa nchi.


"Mradi huu ni kielelezo muhimu sana katika nchi yetu kwani  moja ya chachu kubwa za kukuza uchumi nchini ni matumizi ya umeme, kuna uhusiano mkubwa wa umeme na maendeleo ya kiuchumi na mifano halisi  tunaiona, nchi nyingi Duniani zenye matumizi makubwa ya umeme zimeendelea sana kiuchumi, hivyo Wizara ya Nishati tutaendelea kuongeza nguvu katika kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme. Amesema Kazungu.


Aidha, amemsisitiza Mkandarasi wa mradi kumaliza kazi kwa wakati na  kuwapongeza TANESCO kwa usimamizi wa mradi huo.



Vilevile ameitaka TANESCO kugeukia vyanzo vingine vya umeme kama Jotoardhi na Jua ili kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya ndani ya nchi na pia kuwezesha biashara ya umeme nje ya nchi.


Maendeleo ya jumla ya mradi wa JNHPP hadi kufikia tarehe 30 Novemba 2024 yamefikia asilimia 99.55 na kuingiza 1,175 MW katika gridi ya Taifa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »