Na Ashrack Miraji
ALIYEKUWA Diwani wa kata ya Bendera wilayani Same mkoani Kilimanjaro kupitia chama cha Chadema mwaka 2015-2020, Michael Mcharo (52), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kosa la mauaji ya Edson Shangari (59), mkulima kwa kumpiga risasi tatu mwilini mwake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa alisema kuwa, tukio hilo limetokea Disemba 26 mwaka huu majira ya saa tatu na nusu asubuhi huko kitongoji cha Kaloleni Kijiji cha Bendera kata ya Bendera.
Alisema kuwa, mtuhumiwa huyo alimpiga marehemu risasi tatu, moja mkono wa kushoto, kifuani kushoto na shavu la kushoto ambapo chanzo ni ugomvi baina yao uliotokana na mgogoro wa shamba tangu mwaka 2022.
Kamanda huyo alidai kuwa, mgogoro huo haukupatiwa ufumbuzi hadi tukio lilipotokea juzi.
Aliendelea kudai kuwa, marehemu alikuwa anaelekea shambani kwake na akiwa njiani hatua chache kabla ya kufika shambani alikutana na mtuhumiwa ambaye alimshambulia kwa kumpiga risasi tatu nakumsababishia kifo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya cha Ndungu kusubiria uchunguzi wa Daktari.
Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi ambao wa kata ya Bendera ambao hawakutaka majina yao kuandikwa walidai kuwa, Diwani huyo mstaafu mara kadhaa amekuwa akitumia nguvu kuchukua mali za watu hasa kipindi chake alipokuwa kiongozi huku mara kwa mara amekuwa akiwatishia wananchi.
“Huyo baba tunashukuru sana leo amekamatwa maana wananchi wote kwenye hii kata tulikuwa tunamuogopa sana na mara nyingi amekuwa akitisha wananchi na wakati mwingine anatumia nguvu kuzulumu wananchi mali hata hilo shamba ambalo alikuwa analigombea na marehemu sio lake sisi tunajua lakini sasa tulikuwa tunaogopa kueleza ukweli” alisema mmoja wa wananchi wa kata ya Bendera.
Aidha baadhi ya Madiwani ambao wamefanya nae kazi katika kipindi cha 2015/2020 katika halmashauri ya Same wamedai kuwa, mtuhumiwa huyo alikuwa akisimamishwa vikao mara kadhaa na wakati mwingine kufikishwa katika vikao vya maadili kutokana na tabia yake ya kutukana viongozi wa ngazi za juu za serikali.
“Mimi nimekuwa nae kwenye udiwani kwa kipindi cha miaka mitano lakini tukihesabu viako ambavyo alisimamishwa kutohudhuria ni vingi nah ii ni kutokana na utovu wa nidhamu kwa viongozi serikali na tulikuwa tukimuonya mara kwa mara kuacha lakini hakuwa tayari kutusikiliza alikuwa ni mtu mbabe sana” alisema Mmoja wa Diwani katika halmashauri ya Same.
EmoticonEmoticon