TCRA YAWAHIMIZA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIDIGITALI

October 12, 2024

 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewahimiza vijana nchini kuchangamkia fursa za kidijitali ikiwemo akili bandia (Artificial Intelligence), kwa kubuni mifumo itakayotatua changamoto za kijamii na hivyo kujipatia kipato.

Meneja TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali ametoa rai hiyo Ijumaa Oktoba 11, 2024 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana 2024 yanayofanyika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kuanzia Oktoba 08-14, 2024 yakiwa na kaulimbiu ya "vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa maendeleo endelevu".

Amesema mamlaka hiyo inawawezesha vijana kunufaika na matumizi ya kidijitali kwa kutoa rasilimali za mawasiliano ili kufanikisha mawazo yao ya kibunifu ikiwemo kupata masafa na namba za kuwafikia wateja bure.

"Vijana wenggi wamekuwa na kasumba ya kupuuzia fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotangazwa mpaka waone watu wengine wamefanikiwa, tunapaswa kuchangamkia soko la kidijiti ili kujikwamua kiuchumia" amesema John Waronga ambaye ni mmoja wa vijana waliotembelea banda la TCRA.

Maonesho ya wiki ya vijana yamefunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amewataka vijana kutumia mitandao kujiajiri na kukuza uchumi ili kuwa na taifa lenye uchumi imara huku akiwataka kutotumia maendeleo hayo ya kidijitali kwa matumizi mabaya ikiwemo kuchochea chuki, kueneza taarifa za uongo na picha ama video zisizo na maadili katika jamii.

Majaliwa amesema ili kufikia dira ya maendeleo ya taifa 2050, teknolojia ya kidijitali ina fursa muhimu na maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu kwa vijana kuwa chachu ya maendeleo na kwamba Serikali itaendelea kuwajengea vijana uwezo ili kufanikisha bunifu zao.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akitoa ufafanuzi wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete (kushoto) alipotembelea banda la TCRA.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete (kushoto) alipotembelea banda la TCRA.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea maonesho ya wiki ya vijana kuhusu kampeni ya 'Ni Rahisi Sana' inayoendeshwa na TCRA kwa lengo la kuhamasisha jamii kutambua fursa za kidijiti nk.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akioa elimu kwa mwananchi aliyeembelea banda la TCRA.
Tazama Video hapa chini

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »