HAKIKISHENI MWANACHAMA WA PSSSF ASIONDOKE OFISINI KWETU HAJARIDHIKA: CPA. KASHIMBA

October 06, 2023

NA K-VIS BLOG, DAR ES SALAA.

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba, amewataka watumishi wa Mfuko huo kuhakikisha kwamba mwanachama anapofika ofisini kuhudumiwa asiondoke hajaridhika.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, Oktoba 6, 2023 kwenye kilele cha maadhimisho wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, alipokuwa akizungumza na watumishi wa PSSSF ofisi ya Kanda ya Kinondoni.

“Ombi langu kwenu, ule utaratibu mwanachama akiwa na tatizo anaambiwa andika barua, hatuuhitaji hapa, hizo ni taratibu za kizamani, tutatue matatizo ya wanachama wetu haraka.” Alisema.

Alisema ukigundua kuna tatizo, litatue, ukimwambia mwanachama aandike barua unamshawishi alalamike, tuhakikishe tatizo lisiwe upande wetu, huo ndio mtizamo wetu na hata kama litakuwa upande wa pili tujitahidi kulifuatilia sisi wenyewe na kulitatua, alisisitiza CPA. Kashimba.

Alisema watumishi wa PSSSF, popote walipo nchini, wahakikishe hakuna tatizo la mwanachama linalala halijatatuliwa.

Kuhusu uboreshaji wa utoaji huduma, CPA. Kashimba amewahakikishia wanachama azma ya Mfuko ni kuhakikisha wanatumia mifumo ya TEHAMA kupunguza kuonana na wanachama.

"Niwaambie wateja wetu kuanzia Juni mwakani, tumedhamiria kupunguza kuonana na wanachama, tunataka uwasilishaji madai unafanyika online, kuyachakata online, mwanachama akutane na fedha yake benki na hilo tayari tumelianza," alisema na kuongeza...nia hapa ni kumuondolea mwanachama gharama za kufuata huduma kwenye ofisiz etu, kuokoa muda, lakini pia kupunguza matumizi ya karatasi, na kwa vile karatasi ni miti, tutakuwa tumeokoa mazingira na hivyo kuisaidia Serikali katika kutunza mazingira yetu." Alifafanua.

Aidha, CPA.  Kashimba, amepongeza ushirikiano baina ya taasi yake na zile za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Wiki ya Huduma kwa wateja ni tukio la kimataifa ambalo linaangazia umuhimu wa huduma kwa wateja na watu wanaotoa huduma kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kwa watoa huduma na wateja na kauli mbiu ya mwaka huu ni TEAM SERVICE “Ushirikiano kwa Huduma Bora.”

“Team service ni ushirikiano wa kutoa huduma, tunapokuwa kama timu inasaidia kujibu hoja za wanachama wetu, vizuri na kwa haraka, ndio maana tumekuwa na watu wa NIDA , ambao wametusaidia sana kutatua changamoto za vitambulisho vya taifa kwa wanachama wetu takriban 36 hivi.” Alisema.

Alisema, “Wanachama wetu hawa wamehudumiwa wakiwa hapa na hawakuhitaji kwenda ofisi za NIDA.” Alisema

Hata wenzetu wa NSSF, ushirikiano tulio nao ni kama timu moja, jambo likiwa kwetu, lakini linahitaji uingiliaji wa NSSF, tunaweza kuliona, kwa hiyo ujumbe wa mwaka huu unatafsiri ushirikiano huu wa kitaasisi.” Alisema CPA. Kashimba.

Alisema ushirikiano kama huu umekuwepo hata kwenye maonesho mbalimbali kama vile Sabasaba, Nane nane na kwingineko, ambapo Mifuko ya PSSSF na NSSF wamekuwa wakikaa pamoja ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja wao.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (kulia), akimkabidhi cheti cha shukrani (Appreciation), Afisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wilaya ya Knondoni, Bi. Zuwena Abdallah, kwa ushirikiano walioutoa wakati wa wiki ya huduma kwa wateja, 2023. Kushoto ni  Mkurigenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa PSSS, Bw. Mbaruku Magawa, na Meneja wa Kanda wa PSSSF Kinondoni, Bi. Ritha Ngalo.

CPA. Kashimba (wakwanza kushoto) kwa karibu akiwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbaruku Magawa (wapili kushoto), akichukua maoni ya mwanachama
Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbaruku Magawa, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Meneja wa Kanda wa PSSSF Kinondoni, Bi. Ritha Ngalo (kushoto), akimuhudumia mteja (mwanachama) wa PSSSF.

CPA. Kashimba akipitishwa kwenye eneo la NSSF ambao nao waliungana na PSSSF kuhudumia wanachama.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »