NAIBU WAZIRI MGALU AWASHA UMEME KATA ZA LUGOBA,MANDELA- PWANI

May 04, 2018

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati mstari wa kwanza) akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Hondogo Kata ya Mandela mkoani Pwani. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete na wengine wanaoshuhudia ni Wataalam Waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliyenyanyua mkono akishangilia baada ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Hondogo Kata ya Mandela na mwenye shati la kijani ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete. Wengine ni Watumishi kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Uongozi wa Halmashauri ya Chalinze pamoja na Wananchi wa Kata hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akielekea katika eneo la tukio la uzinduzi rasmi wa kuwasha umeme katika kijiji cha Hondogo. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wengine katika picha ni wananchi kutoka Kata ya Mandela.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akihutubia wananchi wa Kata ya Mandela pomoja na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Saleni kata ya Lugoba, wanaoshuhudia ni Watumishi kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, REA, Uongozi wa Halmashauri ya Chalinze pamoja na Wananchi wa kata ya Lugoba.

……………….

Na Rhoda James, Pwani

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amezindua rasmi upatikanaji wa huduma ya umeme katika Kijiji cha Saleni Kata ya Lugoba na kijiji cha Hondogo Kata ya Mandela mkoa wa Pwani.

Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 3 Mei, 2018 katika vijiji hivyo wakati alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Ujazilizi (Densification) na miradi mengine ya umeme inayotekelezwa mkoani humo na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mgalu aliwaagiza watumishi wa TANESCO na REA kuhakikisha wanaunganishia wananchi wote umeme kwa wakati ili wananchi wafaidike nishati hiyo kwa maendeleo ya kiuchumi.

Pia aliwataka wananchi wa Pwani kuchangamkia fursa ya mradi huo pindi umeme unapofika katika kata zao.

“Fanyeni wiring haraka katika Zahanati na Mashuleni pia katika nyumba zenu ili muunganishiwe umeme wa REA kwa gharama ya shilingi 27,000 tu,” alisema Mgalu.

Mgalu alisema kuwa tayari Kaya 65 katika Kata ya Mandela zimeunganishwa na umeme na kaya nyingine 85 zimeongezwa kwa ajili ya utekelezaji.

Aliongeza kuwa, ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini vitakuwa vimepata umeme kwa kuwa tayari Wakandarasi wote wamekwisha idhinishiwa malipo yao na hivyo kuwataka ambao wameondoka katika maeneo yao kurudi haraka.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lugoba Rehema Issa, alisema kuwa wananchi walichelewa wenyewe kufanya wiring kutokana na sababu mbalimbali lakini sasa watafanya haraka.

“Pia tulikuwa na tatizo la transforma lakini sasa tumewekewa na wananchi wangu watapata umeme,”alisema Issa.

Aidha, Diwani Issa alisema yapo baadhi ya maeneo ambayo hayajapata umeme hivyo alitumia fursa hiyo kumuomba Naibu Waziri Mgalu asaidie ili vijiji vipate umeme kwa wakati.

Kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Jimbo la Chalize Riziwani Kikwete alimshukuru Naibu Waziri Mgalu kwa kutembelea jimbo lake na kwa kasi kubwa ya kuhakiksha wananchi wote wa Pwani wanapata umeme kwa wakati.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »