Na: Veronica Kazimoto
Maafisa
Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wameombwa kuwa mabalozi
wazuri katika sehemu zao za kazi na katika jamii wanayoishi kwa
kuwaelimisha wananchi masuala mbalimbali yanayohusu kodi.
Akizungumza
wakati akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Kodi kwenye Kikao Kazi cha
Maafisa hao kinachoendelea jijini Arusha , Mkurugenzi wa Huduma na
Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard
Kayombo, alisema elimu ya kodi itawafikia watu wengi zaidi kwa kuwa
maafisa hao wana ushirikiano mkubwa katika kutoa habari sahihi kwa umma.
"Kila
mmoja wetu anachokifanya ni sauti kwa mwenzake mahali alipo, ndio maana
hata katika mitandao mbalimbali tumekuwa tukisaidiana kwa kuwa, ukiona
jambo baya linasemwa juu ya taasisi ya mwenzako au Serikali unamsaidia
kutoa ufafanuzi, hivyo, mkielewa mada yangu hapa, najua mtanisaidia
kuelimisha masuala ya kodi katika sehemu zenu za kazi na maeneo
mengine", alisema Kayombo.
Kayombo
alisema kuwa, maafisa hao wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii na
kusahihisha baadhi ya wananchi ambao wanakuwa na elimu isiyo sahihi
kuhusu masuala yanayohusu kodi na ukusanyaji wa mapato kwa ujumla.
Aidha,
pamoja na mambo mengine, Richard Kayombo aliwakumbusha Maafisa hao
suala zima la kudai risiti kila wakati wanaponunua bidhaa ili kuchangia
maendeleo ya nchi.
"Ni
vizuri tu mkafahamu kuwa, tunasimamia kodi mbalimbali ikiwa ni pamoja
na Kodi ya Mapato na Kodi ya Ongezeko la Thamani au kwa jina lingine
Kodi ya Mlaji, ndio maana tunasisitiza kudai risiti kila mnapofanya
manunuzi kwasababu usipopewa risiti na mfanyabiashara aliyesajiliwa kwa
VAT na hata ambaye hajasajiliwa kwa VAT maana yake unakuwa umemnufaisha
mfanyabiashara huyo na familia yake", alisisitiza Kayombo.
Bwana
Kayombo aliwaambia Maafisa hao kuwa, wananchi wakidai risiti kila
wanaponunua bidhaa mbalimbali, wanaepusha udanganyifu unaofanywa na
wafanyabiashara wa kuficha mauzo halisi ambayo yanatumiwa na TRA kama
sehemu mojawapo ya kuwakadiria kodi wafanyabiashara hao.
Kikao
kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinatarajia
kumalizika tarehe 16 Machi, mwaka huu kikiwa na lengo la kuwajengea
uwezo wa namna ya kutangaza shughuli za Serikali na kuhakikisha Idara na
Vitengo vya Mawasiliano na Uhusiano Serikalini vinaimarishwa ili
kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwahudumia
wananchi.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Bw. Richard Kayombo, akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Kodi kwenye
Kikao Kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini
kinachoendelea jijini Arusha. Kikao hicho kinatarajia kumalizika tarehe
16 Machi, mwaka huu. (Picha na Benedict Liwenga).