Kamati ya Maadili ilikutana tarehe 14/3/2018 kupitia shauri linalomhusu Ndugu
Michael Richard Wambura, Makamu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF)
ambaye anashtakiwa na Sekretarieti ya TFF kwa makosa matatu ya kimaadili.
TUHUMA ZILIZOWASILISHWA
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha mbele ya Kamati mashtaka matatu (3)
ambayo ni;
1. Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho
(TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali
ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la
2013.
2. Kughushi barua ya kuelekeza alipwe
malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali
ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la
2013.
3. Kufanya vitendo vinavyoshusha Hadhi
ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama
ilivyorekebishwa 2015)
MAELEZO YA KOSA
Ndugu Michael Richard Wambura alichukua fedha isivyo halali kwa kughushi
barua ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED ya kujipa mamlaka ya kulipwa kwa kula
njama na waliokuwa Viongozi Wakuu wa TFF; Rais na Katibu Mkuu waliopita.
Kitendo hiki ni kuvunja maadili na kushusha hadhi ya Taasisi ya TFF.
SHAURI LILIVYOENDESHWA
Ndugu Wambura alipelekewa wito wa kufika mbele ya Kamati siku ya tarehe
14/3/2018 ili awasilishe utetezi kuhusu tuhuma zinazomkabili. Ndugu Wambura
alipewa hiari ya kutoa utetezi huo kwa mdomo, kutuma kwa maandishi, kuleta
mashahidi au kutuma mwakilishi kama kifungu cha 58 cha Kanuni za Maadili za TFF
toleo la 2013 kinavyoelekeza. Ndugu Wambura alimtuma mwakilishi wake, Wakili
Emanuel Muga, aliyefika na kuthibitisha kuwa ametumwa na mteja wake (Ndugu
Michael Richard Wambura) kuwasilisha utetezi wake mbele ya Kamati.
Baada ya kuelezwa mashtaka yanayomkabili mteja wake, Wakili Muga aliiomba
Kamati kuwa mteja wake anaomba kupewa muda wa kupitia shauri hilo ili aandae
utetezi, vielelezo, na mashahidi. Mara baada ya kutoa ombi hilo Kamati
ilimruhusu asubiri ili ipitie kabla ya kufanya uamuzi. Baada ya majadiliano
wajumbe walikubaliana kuwa suala hili si geni kwa Ndugu Wambura; hivyo siyo
kweli kuwa hana ufahamu nalo. Pia moja ya vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya
Kamati ni utetezi wa maandishi wa Ndugu Wambura kuhusiana na suala hilo ulioandikwa
4/12/2017. Hivyo Kamati ilijiridhisha kuwa Ndugu Wambura anao ufahamu wa
kutosha wa suala hilo na alikuwa na uwezo wa kufika mbele ya Kamati ili kutoa
maelezo ya ziada.
Kamati ilimjulisha Wakili Muga kuhusiana na uamuzi huo na kumtaka aanze
kujikita katika kujibu mashtaka yaliyowasilishwa mbele yake. Hata hivyo Wakili
Muga hakutaka kufanya hivyo na badala yake aliomba apewe muda zaidi wa kuandaa
utetezi, vielelezo, na mashahidi. Kamati ilimkumbusha Wakili Muga kuwa wito
wake ulijieleza vizuri hivyo ilikuwa ni wajibu wake kumshauri mteja wake
ipasavyo na kumsaidia katika kujibu mashtaka yaliyofikishwa mbele yake. Baada
ya maelezo hayo Kamati ilimuuliza Wakili Muga kama yuko tayari kuendelea na
shauri au vinginevyo na yeye akaridhia kuwa shauri liendelee.
Baada ya makubaliano hayo, Wakili Muga alipewa nafasi ya kujibu mashtaka
matatu yanayomkabili mteja wake.
Shitaka la kwanza:
“Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) za malipo
ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume
na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”
Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Michael Richard
Wambura alipokea malipo kutoka Chama cha Miguu Tanzania (FAT) na baadaye TFF
ikiwa ni marejesho ya mkopo ambao FAT ilikopeswa dola la kimarekani $30,000
kutoka katika kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED kwa ajili ya kusaidia uendeshaji
wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2002. Mkataba wa deni hilo ulisainiwa na
Ndugu Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT. Hata hivyo Kamati haikupata nyaraka
wala kumbukumbu zozote zile zinazoonyesha kuwa Ndugu Wambura alipata idhini ya
kukopa kiasi hicho cha fedha kutoka katika Kamati Tendaji ya FAT. Vilevile
Kamati haikuona uthibitisho wa kiasi hicho kupokelewa kwenye akaunti za FAT
zaidi ya Mkataba ambao ulisainiwa na Ndugu Wambura peke yake bila kuwa na
shahidi mwingine kutoka FAT kinyume na taratibu za kawaida za mikataba. Vile
vile Kamati imeshangaa ni taratibu gani zilitumika kwa taasisi kama FAT
kuchukua mkopo mkubwa kama huo kwenye kwenye kampuni hiyo badala ya taasisi za
fedha kama vile benki ambazo ndizo zinazojishughulisha na masuala hayo.
Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Wambura, kwa
nyakati tofauti, alipokea jumla ya sh.84,000,000.00 kutoka FAT na baadaye TFF
kama marejesho ya mkopo kwa niaba ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED. Hata
hivyo Kamati haikupata uthibitisho wa kisheria kutoka kampuni ya JEKC SYSTEMS
LIMITED unaomuidhinisha Bw. Wambura kupokea malipo ya mkopo huo kwa niaba yake
zaidi ya barua Kumb. Na. JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa
kampuni hiyo. Hata hivyo barua hiyo, licha ya kuandikwa miaka 10 baada ya Bw.
Wambura kuchukua nusu ya mkopo huo, haikuwahi kupokelewa TFF na wala haikidhi
matakwa ya kisheria ambayo ni kuwa na Power of Attorney iliyosajiliwa kwa
Msajili wa Hati na Nyaraka.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na Sekretarieti malipo ya mkopo huo
yalifanyika kwa awamu ambapo mara ya kwanza Ndugu Wambura alilipwa $15,000
alizopokea tarehe 29/4/2004. Hata hivyo Kamati ilibaini mapungufu katika fomu
hiyo kwani maombi ya kulipwa fedha hiyo yalitolewa na Ndugu Wambura na
kuidhinishwa na yeye mwenyewe, kinyume na taratibu za fedha.
Malipo hayo ya mkopo hayakufanyika kwa kipindi cha miaka 10, chini ya
Uongozi wa Ndugu Leodgar C. Tenga, mpaka alipoondoka madarakani na kuingia
uongozi mpya chini ya Ndugu Jamal Malinzi ndipo yalipoanza kufanyika tena.
Kamati inapata mashaka juu ya uhalali wa deni na malipo hayo kwani hakukuwa na
madai wala malalamiko yoyote yaliyowasilishwa kudai au kukumbushia deni hilo
kwa kipindi chote hicho. Katika hali ya kawaida siyo rahisi kulipa deni hilo
bila kujiridhisha uhalali wake.
Shitaka la pili
“Kughushi barua
ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo
hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za
TFF Toleo la 2013.”
Sekretarieti iliwasilisha nakala ya barua ya tarehe 21/6/2016 kutoka kwa
Bibi Irene W. Maganga ambaye ni mke wa mmiliki
wa kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED, Marehemu Enock Maganga na mmoja wa
wasimamizi wa mirathi ya marehemu walioteuliwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Barua hiyo inakanusha kuwa kampuni hiyo haikuwahi kupokea malipo yoyote ya deni
hilo. Hii inaonyesha kuwa Ndugu Wambura hakuwahi kupewa mamlaka ya kupokea
fedha hizo na pia hakuwahi kuziwasilisha kwa wamiliki wa kampuni hiyo fedha
alizopokea kutoka FAT na TFF. Kwa msingi huo hata uhalali wa barua Kumb. Na.
JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo aliyoiwasilisha
kuonyesha kuwa ameidhinishwa kupokea malipo hayo unatia shaka. Ndugu Wambura
hajawahi kukanusha maelezo yaliyomo kwenye barua hiyo licha ya kupewa nafasi
akiwa Makamu wa Rais wa TFF.
Shitaka la tatu:
“Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi
ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama
ilivyorekebishwa 2015)”
Kamati imejiridhisha bila shaka kuwa vitendo
vya Ndugu Wambura vinashusha hadhi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF).
Kitendo cha Ndugu Wambura kuiingiza FAT na baadaye TFF katika mkopo wa $30,000
bila kufuata taratibu zozote ni ukiukwaji mkubwa wa maadili. Vile vile kitendo
hicho kimelipaka matope shirikisho hilo mbele ya umma kwani mambo aliyoyafanya
hayaakisi ukubwa na umuhimu wa taasisi hiyo. Kwa nafasi yake ya Makamu wa Rais,
Ndugu Wambura ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, hivyo vitendo hivyo
haviendani na hadhi na majukumu ya nafasi yake hiyo.
HUKUMU
Kosa la kwanza:
Kulingana na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la
2013, Ndugu Michael Richard Wambura, amefanya kosa la kifisadi ambalo adhabu
zake ni;
- (i) faini isiyopungua shilingi 10,000,000.(ii) kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5
- Kama suala ni zito na limekuwa likijirudia rudia, kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha.Kosa la pili:Kwa kosa la kughushi kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, kinatoa adhabu ya kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5.Kosa la tatu:Kwa kosa la kushusha hadhi ya Shirikisho ni kwenda kinyume na Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015). Hili ni kosa la kimaadili ambalo adhabu zake zinaenda sambamba na adhabu nyingine zinazotolewa na Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.Baada ya kupitia shauri hili na kuridhika pasipo na shaka kuwa Ndugu Michael Richard Wambura ametenda makosa hayo yote, Kamati imemfungia Ndugu Michael Richard Wambura kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia uzito wa kosa lake kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.Kwa kuwa suala hili linahusisha masuala ya rushwa, Kamati inaielekeza Sekretarieti, kwa kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, ilifikishe suala hili la Ndugu Michael Richard Wambura katika vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi. Aidha Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Ukaguzi kuwa waliokuwa viongozi wakuu wa TFF wakati malipo hayo yanafanyika, Ndugu Jamal Malinzi (Rais) na Ndugu Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao waunganishwe katika uchunguzi huo.HITIMISHOKamati haikupendezwa na taarifa zilizowasilishwa na Sekretarieti kuhusu juhudi zilizofanywa na vyombo mbalimbali kuizuia isifanye kazi yake kwa mujibu wa Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015) na Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013. Kamati inaviasa vyombo hivyo kutoingilia mambo ya mpira wa miguu, hasa vyombo vya kimaamuzi, kwani athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa ustawi wa mpira wa miguu nchini.IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF