Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina akizungumza na vyombo mbalimbali
vya habari katika ukumbi wa Ofisi ya Wizara hiyo mjini
Dodoma leo. Kushoto ni Naibu Waziri wake Mhe.Abdalah Ulega na mwishoni
ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt.
Mary Mashingo. Mkutano huo ulikuwa kwa ajili yakutoa tathimini ya zoezi
la upigaji chapa mifugo baada ya kumalizika kwa siku 15 za awali
baada ya muda wa nyongeza wa siku 30 uliotolewa na Waziri Mpina.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina akijibu maswali ya
Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Ofisi ya Wizara hiyo Mjini
Dodoma leo. Mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya kutoa tathimini ya zoezi
la upigaji chapa mifugo baada ya kumalizika kwa siku 15 za awali
baada ya muda wa nyongeza wa siku 30 uliotolewa na Waziri Mpina.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema wizara
yake haina mpango wa kuongeza tena muda zoezi la utambuzi wa mifugo
na kuwataka wafugaji popote walipo nchini kupaza sauti zao ili kuhakikisha
kuwa ng’ombe na punda wote wamepigwa chapa ifikapo Januari 31 mwaka
huu.
Pia Waziri Mpina amechukizwa na tabia ya baadhi ya
watendaji wa Serikali kuwakatalia wafugaji kupiga chapa mifugo yao kwa
kisingizio kuwa sio wakazi halali wa maeneo husika jambo ambalo amesema
halikubaliki na kusisitiza kuwa zoezi lisihusishwe na migogoro ya muda
mrefu ya matumizi ya ardhi na hivyo kuagiza kuwa ng’ombe na punda
wote nchini wapigwe chapa isipokuwa ya kutoka nchi jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu
tathmini ya utekelezaji wa zoezi upigaji chapa mifugo, Mpina alisema
hadi kufikia Januari 16 mwaka huu jumla ya ng’ombe 10,306,359 sawa
na asilimia 59.3 ya lengo wameshapigwa chapa ikiwa ni ongezeko la asilimia
20 ya tathmini ya awali.
Aidha amesema wafugaji wote nchini wataoshindwa kupiga
chapa mifugo yao ndani ya muda uliowekwa hatua kali zitachukuliwa kwa
mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Namba 12 ya mwaka
2010 ibara ya 4 kifungu cha 26 huku akizionya halmashauri ambazo zitashindwa
kutekeleza kikamilifu hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wake.
Alisema hadi sasa halmashauri 100 zimepiga chapa
zaidi ya asilimia 50, halmashauri 54 zimepiga kati ya asilimia 10 hadi
50, halmashauri 14 zimepiga chini ya asilimia 10 huku halmashauri 9
zikiwa bado hazijaanza kabisa zoezi hilo.
Waziri Mpina amezitaja Halmashauri hizo ambazo hadi
sasa hazijaanza kupiga chapa ni Tandahimba, Nanyumbu, Mafia, Newala,
Halmashauri za miji ya Newala, Nanyamba, Masasi na Manispaa za Kigamboni
na Ilemela Mwanza ambapo amesema halmashauri 68 ambazo ziko chini ya
asilimia 50 na ambazo haijaaanza kabisa tayari halmashauri hizo ameziwasilisha
kwa Waziri Mkuu.
Pia alisema halmashauri 6 zina ng’ombe wengi wa
maziwa walio kwenye mpango wa kuvalishwa hereni pamoja na mikoa mingine
ambapo jumla ya ng’ombe wote wa maziwa nchini 782,995 kwa sasa, aidha
jumla ya punda 572,353 wanatarajiwa kupigwa chapa, taarifa kutoka mikoani
kuhusu utekelezaji wa zoezi hili zinaendelea kukusanywa kila siku.
Alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 20.8 katika
muda wa kipindi cha wiki mbili tangu muda wa nyongeza kutolewa ongezeko
hili ni kutokana na juhudi za pamoja za uhamasishaji uliofanywa kati
ya Wizara na halmashauri pamoja na mchango mkubwa uliotolewa na vyombo
vya habari .
“Hivyo juhudi kubwa za pamoja baina ya Wizara,
Halmashauri, vyombo vya habari na wafugaji zinahitajika ili kukamilisha
zoezi la upigaji chapa kwa asilimia 100, kwa kuwa hadi sasa bado asilimia
40.7 ya ng’ombe hawajapigwa chapa “alisema
Aidha Waziri Mpina amesema kipimo cha asilimia hakitakuwa
kigezo cha mwisho cha uhakiki mifugo iliyopigwa chapa badala yake ni
kuhakikisha kila ng’ombe na punda mwenye umri wa kuanzia miezi sita
wamepigwa chapa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji, Mashimba Ndaki alipongeza
juhudi kubwa zilizofanywa na wizara hiyo katika kusimamia zoezi la upigaji
chapa ambalo limeungwa mkono na wafugaji wengi nchini.