Kamati
ya Maadili iliyokutana Januari 18, 2018 imepitia shauri lililowasilishwa na
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF wakiwatuhumu viongozi
wanne kwa makosa ya kughushi na udanganyifu wa mapato kwenye mchezo namba 94
kati ya Ndanda FC na Simba uliochezwa Disemba 30,2017.
Shauri
la kwanza lililomuhusu Katibu msaidizi wa Ndanda Ndugu Selemani Kachele,Kamati
imegundua kuwa mtuhumiwa aliitwa wakati wa kuhesabu mapato kuthibitisha deni dhidi
ya Ndanda lenye thamani ya Shilingi Milioni mbili laki mbili na elfu hamsini(2,250,000),deni
ambalo TFF waliagiza wakatwe kwenye mapato ya mechi hiyo,Katibu wa Chama cha
Mpira wa Miguu mkoa wa Mtwara alithibitisha kuwa alimuita kuthibitisha uhalali
wa deni hilo baada ya Muhasibu wa Ndanda kugoma kulipa deni hilo ambalo
linahusu pango la Ndanda kwa Mama mwenye Nyumba.
Hata
hivyo Kamati ilimuhoji zaidi na akashindwa kutoa uthibitisho wa kulipwa kwa
deni hilo na hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa deni hilo limelipwa.
Kamati
imempa onyo kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(a) kanuni za maadili ya TFF toleo la
2013 na imeiomba Sekretarieti ya TFF ifuatilie kama deni hilo limeshalipwa ili
kuepusha ulipaji wa Zaidi ya mara moja.
Shauri
la Pili lilimuhusu Muhasibu msaidizi wa Simba Ndugu Suleiman Kahumbu.
Kamati
haikuendelea na tuhuma dhidi yake baada ya Sekretarieti ya TFF kuamua kuondoa
shauri dhidi yake kwa kuwa alitoa ushirikiano na kutosheka kuwa hana hatia na badala
yake alitumika kama shahidi wa upande wa washtaki.
Shauri
la tatu lilimuhusu Katibu mkuu wa Chama cha soka Mtwara Ndugu Kizito Mbano.
Kamati
ilimuhoji mtuhumiwa na alikiri kuwepo kwa mawasiliano na msimamizi wa kituo
Ndugu Dunstan Mkundi kuhusu nia ya kughushi fomu ya marejesho ya mapato ya
mchezo kati ya Ndanda FC na Simba SC.
Ndugu
Kizito Mbano hakutoa taarifa yoyote ile wala kuonyesha ushirikiano kwa
Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi wakati yeye akiwa msimamizi msaidizi wa
kituo na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Mtwara,hivyo Kamati imemkuta
na hatia na imemuhukumu kutojihusisha na shughuli za Mpira wa Miguu kwa kipindi
cha miaka Mitano(5) kwa mujibu wa kifungu cha 73(7) cha kanuni za maadili TFF
toleo la 2013.
Shauri
la nne lililosikilizwa lilikuwa la Msimamizi wa Kituo cha Mtwara Ndugu Dunstan
Mkundi.
Kamati
baada ya kusikiliza shauri hilo imemkuta na hatia kwa kosa la kushindwa
kuwasilisha fomu ya mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na
Simba ndani ya saa 48 kama kanuni inavyotaka.
Hiyo
ni kinyume na Kanuni ya 32(2) Kanuni za Ligi Kuu toleo la 2015,Vilevile Kamati
imemkuta na hatia ya kushindwa kusimamia mauzo ya tiketi za mchezo kati ya
Ndanda FC na Simba kwa kutotoa taarifa
ya tiketi zilizotumika na zile zilizobaki.
Kamati
ilibaini kuwa Ndugu Dunstan Mkundi akiwa msimamizi wa kituo hakutoa ushirikiano
kwa kutompa taarifa za mapato na idadi ya watazamaji Kamisaa wa mchezo Salum
Singano kinyume na Kanuni ya 32(4) ya Ligi Kuu toleo la 2017.
Aidha
Mkundi ambaye ni msimamizi wa kituo cha Mtwara ameshindwa kutoa maelezo ya
kutosha kuhusu utata wa fomu mbili zilizowasilishwa zilizoonyesha utofauti wa
mapato kwa kiasi cha shilingi Milioni tatu laki saba kumi elfu(3,710,000).
Washtakiwa
wote walihojiwa na Kamati na kuthibitisha kuwa mapato ya mchezo kati ya Ndanda
FC na Simba yalikuwa ni Shilingi Milioni thelathini na saba laki saba na
themanini elfu(37,780,000) na siyo Shilingi milioni thelathini nne sabini elfu(34,070,000)
ambazo Ndugu Mkundi anadai kuwa ndiyo yalikuwa mapato ya mchezo huo.
Kulingana
na nyaraka zilizowasilishwa kutoka klabu za Ndanda FC na Simba mapato ya Vilabu
hivyo yalitokana na asilimia ya vyanzo kutokana na milioni thelathini na saba
laki saba themanini elfu(37,780,000) na siyo Shilingi milioni thelathini nne
sabini elfu(34,070,000)kama alivyowasilisha msimamizi huyo wa kituo cha Mtwara nyaraka
za fedha alizoweka kwenye akaunti za TFF na Bodi ya Ligi.
Kitendo
cha kughushi nyaraka na kupunguza mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba
siyo tu kimeharibu taswira ya mchezo wa Mpira wa miguu,bali pia kimepunguza
mapato ya TFF,Bodi ya Ligi na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mapato
(TRA),Baraza la Michezo la Taifa (BMT),Wamiliki wa Uwanja na Wadau wengine.
Kamati
imemtia hatiani Ndugu Dunstan Mkundi kwa makosa hayo na inamfungia maisha
kutojishughulisha na mchezo wa Mpira wa Miguu.
Kamati
imetoa adhabu hiyo kali ili iwe fundisho kwa wale wote wanaotaka kufanya
ubadhirifu wa ufisadi katika mchezo wa Mpira wa Miguu.
Kamati
inashauri Sekretarieti ya TFF ifuatilie suala hili kwenye vyombo vya dola na
mamlaka husika kwa hatua zaidi za kisheria.
Pia
Kamati imeiomba Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kutafuta njia bora ya
kuimarisha udhibiti wa mapato kwa kuongeza uwajibikaji wa uwazi kwa wadau wote,Vilevile
Kamati inashauri Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kuharakisha mchakato wa
kukusanya mapato yake kwa njia za kielektroniki ili kuziba mianya ya upotevu.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO
LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF