WAZIRI MPINA AWAKAANGA VIONGOZI WANAOHUJUMU WAFUGAJI, AMSIFU DC GODWIN GONDWE KUSIMAMIA KIKAMILIFU SEKTA YA MIFUGO

December 26, 2017
 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina wa pili kulia akitazama mifugo ya ngombe aina ya Borani waliyopo kwenye ranchi ya mzeri wilayani Handeni mkoani Tanga wakati wa ziara yake wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Handeni,Godwin Gondwe
  Mkuu wa wilaya ya Handeni,Godwin Gondwe kushoto akimuleza jambo  WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kulia ambaye alifanya ziara ya kikazi wilayani humo
 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akisisitiza jambo wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kumaliza ziara yake kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Handeni,Godwin Gondwe
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina wa pili kutoka kushoto akiwa na Mkuu wa wilaya ya Handeni Godwin Gondwe wakati alipoitembelea ranchi ya mzeri wilayani humo
NA MWANDISHI MAALUM, HANDENI
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amechukizwa na tabia ya baadhi  watendaji wa Serikali katika Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba na Serikali za Mitaa kukamata mifugo kiholela na kutoza faini zisizo na misingi ya kisheria huku akisifu utendaji kazi ya wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe katika usimamizi wenye weledi wa sheria za mifugo nchini.
Mpina ametoa kauli hiyo akiwa wilayani Handeni ambapo alitumia fursa hiyo kupiga marufuku ukamataji mifugo kiholela huku akimtaja Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Gondwe kama kielelezo cha kuwa kiongozi wa kwanza kitaifa anayezifahamu vizuri na kuzisimamia kikamilifu sheria za mifugo na kuleta tija katika ukuaji wa sekta hiyo ikiwemo kuanzisha kijiji cha wafugaji,kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na utoaji huduma bora za mifugo wakati wote.
Akizungumzia tatizo hilo la ukamataji holela wa mifugo nchini, Waziri Mpina amesema kama sekta hiyo isingekuwa inazalisha mazao ya mifugo na Serikali kuamua kuagiza kutoka nje ya nchi basi ingezilazimu kutumia kiasi cha sh. Trilioni 17.8 huku kaya milioni 4.49 za  kilimo nchini zinajishughulisha na ufugaji mifugo aina mbalimbali.
“Watendaji wa Serikali waliofanya hujuma na dhuluma kwa wafugaji hawatabaki salama, tutawafuatilia na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria”alisema.
Amesema  Sheria ya misitu na. 14 ya mwaka 2002 kifungu cha 26 kinazuia mifugo kuingia kwenye hifadhi za misitu ya kitaifa au iliyo chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo pamoja na wafugaji kuvunja sheria hiyo bado wanahitaji kutendewa inavyostahili kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuweka ulinganifu wa watanzania wote mbele ya sheria za nchi.
Waziri Mpina amebainisha kuwa kumekuwa na mazoea mbalimbali ya ukamataji holela wa mifugo yanayoendelea nchini ambayo yanatekelezwa bila kuzingatia sheria ya ustawi wa Wanyama (Animal welfare Act No.19 of 2008) na Kanuni zake za mwaka 2010 kifungu cha 7 na 8 na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na 17 ya mwaka 2003 (Animal Disease Act No.17 of 2003) hivyo mifugo imekuwa ikishikiliwa kama kidhibiti kwa muda mrefu na mingine kufa kutokana na magonjwa na ukosefu huduma ikiwemo matibabu,chanjo na kuogeshwa ili kuepuka magonjwa ndorobo na kupe.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema wao kama Serikali ya wilaya katika sheria ndogo yao ikiwa kundi la mifugo litaingia kwenye maeneo yasiyoruhusiwa wameweka faini isiyozidi sh 300,000 kwa kundi la ng’ombe ambapo alisema pamoja na pongezi za Waziri Mpina bado wataendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuboresha sekta ya ufugaji ikiwemo uimarishaji wa majosho, malisho na uzuiaji uuzaji nyama kiholela barabarani.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »