Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Bi. Susana Mkapa na Afisa Mwandamizi wa Wizara hiyo Bw.
John Sausi wakizungumza jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) na
Waandishi wa Habari kuhusu Hali ya uchumi na utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2017/18 katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango
Jijini Dar es Salaam.
Maafisa Waandamizi kutoka Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) wakifurahia jambo wakati Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari ambapo aliangazia suala la hali ya
Uchumi na kubainisha kuwa ni imara ukilinganisha na nchi nyingine za
Afrika Mashariki, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar
es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaabani (kushoto) akizungumza na
wadau waliohudhuria Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) na waandishi wa habari katika
ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam kulia.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu Hali ya uchumi na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2017/18 ambapo alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kuwakamata
wanaowalazimisha watanzania kufanya malipo kwa Dola badala ya Shilingi,
mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini
Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akitoa maelekezo kwa Benki nchini
kuangalia namna ya kupunguza riba kwa wakopaji na pia kufuata vigezo
stahiki kwa mkopaji ili kuondoa mikopo chechefu wakati wa mkutano kati
yake na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (mbele) akiwa katika Mkutano na waandishi
wa habari kuhusu hali ya uchumi na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2017/18 katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es
Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
………………………………………………………
Na. Paschal Dotto.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha
na Mipango imewatoa hofu wananchi kuhusu uvumi wa kuongezeka kwa deni la
Taifa kwamba deni hilo ni himilivu na liko chini ya ukomo wa hatari.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philipo Mpango wakati akitoa
mwenendo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2017/2018 .
Dkt. Mpango alisema kuwa katika
tathimini iliyofanyika mwezi Novemba mwaka huu inaonesha kuwa uwiano wa
deni hilo na pato la Taifa ni asilimia 32.5 likilinganishwa na ukomo wa
asilimia 56.
“Katika kuangalia ukomo wa deni
hili ambao uko chini, inaonesha kuwa deni hili ni himilivu katika
kipindi cha muda wa kati na muda mrefu”, alisema Dkt. Mpango.
Akieleza takwimu hizo, Waziri
Mpango amesema kuwa mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, deni la Taifa
lilifikia shilingi bilioni 47,823.1 ikilinganishwa na bilioni 42,552.4
katika kipindi kama hicho mwaka 2016 ambapo kati ya kiasi hicho,
shilingi bilioni 13,417.5 ni deni la ndani sawa na asilimia 28.1 na
shilingi bilioni 34,405.6 ni deni la nje ambalo ni sawa na asilimia
71.9.
Dkt. Mpango alisisitiza kuwa
ongezeko hilo lilitokana na kupatikana kwa mikopo mipya ya nje na ndani
ya nchi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maeneeleo.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni
ujenzi wa mradi wa umeme Kiwira (Kiwira Coal Mine), miradi ya uboreshaji
wa huduma za maji kwa jamii, mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa
kinyerezi na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege ambapo miradi hiyo
itawezesha watanzania kufika uchumi wa kati wenye viwanda.
“Mambo muhimu ya kujiridhisha
nayo ni kwamba mikopo inayokopwa itumike katika kujenga uwezo zaidi wa
kuzalisha mali na huduma nzuri kwa watanzania”, alisisitiza Dkt. Mpango.
Aidha Waziri Mpango amesema kuwa
kufuatia hatua zinazochukuliwa na Serikali, ukwasi kwenye benki za
biashara uliongezeka na kusaidia kupungua kwa riba ya mikopo baina ya
mabenki na kufikia wastani wa asilimia 3.53 mwezi Novemba mwaka huu
kutoka wastani wa asilimia 14.93 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016/2017.
Vilevile riba za dhamana za
Serikali zilishuka kutoka wastani wa asilimia 15.56 katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2016/2017 hadi asilimia 8.76 mwezi Novemba, 2017 na
kuongeza kuwa Serikali inatarajia kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta
binafsi itaanza kuimarika.
Aidha, Dkt. Mpango amewaonya watu
wanaotoa takwimu za uongo kuacha mara moja kwani wanaipotosha jamii,
huku akiwataka waandishi wa habari kupata takwimu maalumu kutoka Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili kuweka takwimu sahihi.