VIONGOZI
wa madhehebu mbalimbali ya kidini wameombwa kusaidia kuondoa unyanyapaa
wa wagonjwa wa Ukimwi ikiwa ni sehemu kamili ya kukabiliana na janga
hilo nchini.
Aidha
wametakiwa kutumia program mbalimbali walizonazo katika mahubiri na
kazi zao kuhakikisha kwamba taifa haliwi na maambukizi mapya ya Ukimwi
na wale waliokuwa nao wanathaminika.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS),
Dk. Leonard Maboko katika mkutano wa kuimarisha uratibu wa Afua za
Ukimwi katika Taasisi za Kidini uliofanyika Chuo cha Maendeleo na
Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo.
Alisema
wakati taifa linapata maambukizi mapya 81,000 kwa mwaka, si sahihi kwa
viongozi hao wa kidini kuupambanisha ugonjwa huo na mshahara wa dhambi.
- Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko akizungumza wakati akifungua mkutano wa kuimarisha uratibu wa Afua za Ukimwi katika Taasisi za Kidini uliofanyika Chuo cha Maendeleo na Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo.(Picha zote na The Beautytz)
Alisema
pamoja na ukweli kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, lakini ni kweli pia
kwamba wapo ambao wanapata ugonjwa huo bila wao kufanya chochote kile.
“Mke
yupo nyumbani, mme anachepuka na kuleta ukimwi nyumbani kwa mama… kama
tukisema Ukimwi ni dhambi, huyo mama ana dhambi yake nini? Na mtoto
aliyezaliwa na Ukimwi, tatizo la mtoto nini?” aliuliza Mkurugenzi akisisitiza haja ya kuondokana na unyanyapaa na kusaidia kwa pamoja kukabiliana na janga hilo.
Unapotoa
hotuba na kusema kwamba utakufa na Ukimwi wako, haitoi tumaini kwa
mgonjwa na wewe unaweza kuwa sababu ya yeye kuamua kuambukiza watu zaidi
alisema Mkurugenzi huyo.
“madhehebu yana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika shughuli za Ukimwi” anasema
Mkurugenzi na kuongeza kuwa yuko katika mapambano na Ukimwi kwa miaka
22 na ana kila sababu ya kusema kwamba madhehebu ya dini yana mchango
mkubwa katika kampeni dhidi ya Ukimwi.
Anasema
akiwa mchungaji (alitolewa katika kazi hiyo) anaamini ipo haja ya
kuwapo na mabadiliko ikiwa mapambano hayo yanatakiwa yafanikiwe.
Katika
mkutano huo ambao umefadhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na
Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) alisema kwa muda sasa imekuwa
ukisimama na kutaja Ukimwi unaonekana kama umetaja dhambi hali ambayo
inaongeza unyanyapaa na pia kuwafanya watu wasiwe wa wazi na afya zao.
Aidha
alisema kwamba kwa sasa kuna tatizo la wanaume wengi kutopima afya zao
na hata wakipima hawafuati maelekezo na wanakuwa wa kwanza kufa kutokana
na kushindwa kutumia dawa inavyotakiwa.
- Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mwitikio wa Kitaifa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Audrey Njelekela akizungumza kuhusu nafasi ya viongozi wa dini katika kuleta mabadiliko ya mapambano dhidi ya Ukimwi kwenye mkutano wa kuimarisha uratibu wa Afua za Ukimwi katika Taasisi za Kidini uliofanyika Chuo cha Maendeleo na Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo kwa ufadhili wa UNESCO.
Alisema
kwamba kuwa na nusu ya Watanzania wanaoabudu Mungu kunatoa takwimu
zisizo rasmi kwamba watu wengi wanasikiliza mafundisho hivyo wakati
umefika kwa wahubiri na viongozi wengine wa dini kutumia madhehebu
kufunza maadili na kuepusha maambukizi mapya.
Alisema
dini zipo kwa ajili ya kuwanusuru wanadamu na dhambi na kwa kuwa
imeelezwa hata katika kitabu, kwamba mgonjwa hufuata tabibu, kuendelea
kuwasema wenye ugonjwa huo haitasaidia kurekebisha hali bali kuifanya
iwe ngumu zaidi.
Pamoja
na kutaka viongozi hao kupanga namna ya kuwatia moyo waumini wao
kutambua hali zao na kuwasaidia katika kutumia dawa kwa ukamilifu,
Mkurugenzi huyo alisema hali ya Ukimwi nchini Tanzania kwa sasa ni
asilimia 4.7 kutoka asilimia 5.1 miaka minne iliyopita.
- Mratibu wa shughuli za watoto na vijana TACAIDS, Grace Kessy akieleza kuhusu kutekeleza maazimio ya ESA ya mwaka 2013 ambapo nchi zinahamasishwa kutoa elimu kubwa kwa vijana wao kuhusu afya ya uzazi wakati wa mkutano wa kuimarisha uratibu wa Afua za Ukimwi katika Taasisi za Kidini uliofanyika Chuo cha Maendeleo na Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo kwa ufadhili wa UNESCO.
Aidha
alisema kwamba pamoja na virusi kuonekana kufubazwa kwa asilimia 52
mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya hali ya maambukizi bado ipo juu huku
mikoa ya Mtwara, Lindi na Arusha ikiwa chini.
Alisema
pamoja na kuonekana kwamba kiwango cha maambukizi kimeshuka mtu anaweza
kujiuliza sababu zake kama mipango ya kukabiliana na Ukimwi inapata
mafanikio au watu wengine zaidi walioambukizwa wamefariki dunia.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mwitikio wa Kitaifa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Audrey Njelekela, alisema katika mkutano huo
viongozi wa madhehebu mbalimbali nchini wanatarajiwa kutoka na mpango
mkakati utakaohusisha mipango ya na taifa katika kampani ya kukabili
Ukimwi.
Alisema
katika mkutano huo wa siku mbili, viongozi hao pamoja na kubadilishana
uzoefu watapata nafasi ya kujifunza umuhimu wa kuratibu mapambano hayo
ili kutumia vyema rasilimali watu na fedha zilizopo,
Alisema
pamoja na kuwepo kwa vikwazo katika shughuli za uratibu ikiwamo
kukosekana kwa mtengamano na ukosefu rasilimali fedha, kuna faida kubwa
ya kufanya uratibu kwa ajili ya kuwa na taarifa za uhakika na kutorudia
kazi.
Alisema
Tume ya kudhibiti Ukimwi ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa
kuita viongozi hao wa dini imelenga kufanya mapambano ya kukabili Ukimwi
kuwa endelevu na yenye wigo mpana.
Alisema katika mkutano huo pia walielezana kila kundi lipo wapi linafanya nini na kuimarisha uratibu dhidi ya ugonjwa huo.
Naye
Mwakilishi wa UNESCO katika mkutano huo, Herman Mathias ambaye pia ni
Mratibu wa Ukimwi Unesco alisema kwamba mkutano huo pia una lengo la
kutekeleza maazimio ya ESA ya mwaka 2013 ambapo nchi zinahamasishwa
kutoa elimu kubwa kwa vijana wao kuhusu afya ya uzazi.
Aidha
mkutano utaangalia maelekezo kuhusu 2020 vijana kufikiwa na huduma
rafiki za afya ya uzazi, kupunguza ndoa za utotoni, unyanyasaji kijinsia
na ukeketaji.
Alisema
watu wa dini wana mchango mkubwa ndio maana Unesco kwa kushirikiana na
Tume ya Ukimwi wameandaa mkutano huo ili kubadilisha mawazo na uzoefu.