Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemas Mushi (wa pili kulia) akimkabidhi mbuzi Mchungaji wa Kanisa la EAG, Dennis Shija (wa tatu kulia) ambaye ni msimamizi wa Kituo cha wa Toto na Wazee wasiojiweza Mbagala Kuu ikiwa ni sehemu ya msaada uliotolewa na TTCL kwa vituo vitatu vya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wazee. |
KAMPUNI ya
Simu Tanzania (TTCL) imekabidhi bidhaa mbalimbali za vyakula kwa vituo
vitatu vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wazee
wasiojiweza vyote vya jijini Dar es Salaam, ikiwa ni zawadi ya Siku Kuu
za Chrismas na mwaka mpya kwa makundi hayo.
Akikabidhi
msaada huo leo Makao Makuu ya Ofisi za TTCL Dar es Salaam kwa niaba ya
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri w. Kindamba, Meneja Uhusiano na
Mawasiliano wa kampuni hiyo, Nicodemas Thomas Mushi alisema vituo
vilivyopokea msaada huo ni pamoja na 'Green Pastures Orphanage'
Mapinga-Bagamoyo, Kituo cha Bethel Center Mbagala na Kituo cha Wazee
wasiojiweza cha Bethel cha Mbagala Kuu vyote vya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kugawa msaada huo, Mushi alisema huo ni utaratibu wa
kawaida wa kampuni ya TTCL kutoa msaada kwa jamii hasa kwa makundi ya
watu wasiojiweza ili yaweze kujumuika na Watanzania wengine katika
kusheherekea siku kuu za Chrismas na Mwaka Mpya kwa makundi hayo
yanayokabiliwa na changamoto anuai.
"Huu
ni utaratibu wa kawaida wa kampuni yetu kila mara hali ya uchumi
inaporuhusu huwa tunayakumbuka makundi yenye mahitaji maalum na
nikupitia ule utaratibu wetu wa kawaida wa kurejesha sehemu kidogo ya
faida yetu kwa jamii, tumechangua makundi haya baada ya kupitia maombi
yao na kujiridhisha wana vigezo vya kusaidiwa kutokana na walivyojieleza
changamoto walizo nazo," alisema kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa
kampuni hiyo.
Alisema
kuwa kampuni ya TTCL itaendelea kuyakumbuka makundi hayo maalum na
kuyasaidia kwa chochote kadri inavyokuwa na uwezo wa kufanya hivyo, huku
akishauri taasisi zingine na watu wanaojiweza kusaidia pale wanapokuwa
na uwezo wa kufanya hivyo kwa wasiojiweza. "...Natoa wito pia kwa
makampuni, taasisi na watu wengine wenye uwezo kuunga mkono juhudi hizi
za kusaidia makundi ya wasiojiweza ili yaweze kufarijika kwa namna moja
ama nyingine," alisema.
Aidha
alibainisha bidhaa zilizokabidhiwa ni pamoja na mbuzi watatu, mchele
kilo 300, mafuta ya kula ndoo 9, maharage kilo 300, Sukari kilo 150,
Unga kilo 300, juisi, maji, soda na aina mbalimbali ya mafuta ya
kujipaka na sabuni vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni
5.
Mchungaji
wa Kanisa la EAG, Dennis Shija ambaye ni msimamizi wa Kituo cha wa Toto
na Wazee wasiojiweza Mbagala Kuu alimshukuru Ofisa Mtendaji Mkuu wa
TTCL, Bw. Kindamba kwa msaada walioutoa katika vituo hivyo na
kumuhakikishia watautumia kama ulivyo kusudia.
Aliongeza
kuwa makundi hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo wanapata
faraja kampuni kama TTCL kujitokeza kujitokeza kuwasaidia. "...Sisi
tunashukuru sana kwa msaada tuliopokea leo kwa ajili ya maandalizi ya
siku kuu za mwisho wa mwaka huu, hii sio mara ya kwanza kusaidiwa na
TTCL naomba kuwahakikishia msaada huu utatumika kama ulivyokusudiwa,"
alisema mchungaji huyo.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Kituo cha 'Green Pastures Orphanage' cha
Mapinga Bagamoyo, Restiel Natai aliishukuru kampuni ya TTCL kwa kuamua
kuwakumbuka watu wasiojiweza ili waweze kusherekea kwa furaha siku kuu
hizi za mwisho wa mwaka. Pamoja na hayo alitoa wito makampuni na taasisi
nyingine kujitokeza kuwasaidia makundi kama hayo kwani nayo yanaitaji
faraja hasa kipindi kama hiki ambapo familia zinakutana na kusherehekea
pamoja.
Hata
hivyo, alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiunga mkono kampuni ya
kizalendo ya TTCL ambayo sasa imefanya mageuzi makubwa kihuduma kwa
kutumia huduma zake mbalimbali za mawasiliano kama huduma za intaneti,
simu za mkononi na mezani na vifaa vya mawasiliano anuai kufurahia
huduma bora zenye bei nafuu.