DIRISHA DOGO LA USAJILI.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesikitishwa kwa hitilafu
iliyotokea siku ya mwisho ya usajili usiku wa Desemba 15, mwaka huu kwa
kufeli kwa mtandao wa mfumo wa usajili hali iliyosababisha vilabu
kushindwa kukamilisha usajili kwa wakati kupitia mfumo huo.
TFF
inaendelea na jitihada za kuwasiliana na Mwendeshaji wa mfumo huo
waliokasimiwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA) walioko Tunis,
Tunisia ili kutatua tatizo hilo la kimtandao haraka iwezekanavyo ili
kuweza kukamilisha usajili wa dirisha dogo. Katika mawasiliano na kampuni hiyo, FIFA na CAF wamekuwa wakipewa Taarifa ya kila hatua inayochukuliwa na TFF.
Wakati
huu ambao jitihada hizo zinaendelea, TFF imevitaka vilabu kuwasilisha
nyaraka za usajili wa dirisha dogo katika ofisi za Makao Makuu ya TFF
Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
TFF imetoa muda hadi Jumamosi Desemba 23, 2017 kwa vilabu kuwasilisha nyaraka hizo za usajili wa dirisha dogo.
TFF inasisitiza vilabu vyote kuzingatia kusajili kwa wakati pale inapotokea dirisha la usajili limefunguliwa.
RATIBA MPYA LIGI KUU YA VODACOM
Ligi
Kuu ya Vodacom iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji
inaendelea mwishoni mwa mwezi huu kwa mechi za raundi ya 12
zitakazochezwa kati ya Desemba 29 na 31 mwaka huu, na Januari mosi
mwakani.
Vilevile
mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8
kamili mchana. Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo
wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8 kamili mchana, na
saa 4 kamili usiku.
Uamuzi
huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zinataoneshwa moja kwa moja
(live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi
kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa
wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi (mileage).
Hivyo,
mechi 102 kati ya 152 zitaoneshwa moja kwa moja ikiwemo zile
zinazofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida
zinachezwa kuanzia saa 1 kamili usiku.
Mechi
za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1 usiku),
Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8 mchana), Mtibwa Sugar vs
Majimaji (saa 10 jioni), Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31;
Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao vs Yanga (saa 10
jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni), na Mwadui
vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).
Baada
ya raundi ya 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapisha mechi za Kombe la
Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports
itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya
13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.
Kwa
upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30
kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba
31.
Ligi
Daraja la Pili (SDL) itaanza hatua ya pili Desemba 29 kwa Kundi B, C na
D wakati mechi za Kundi A zitafanyika kuanzia Desemba 30, 2017.