Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano
Mwansasu (kulia), akitoa maelezo kwa Maafisa wa Idara mbalimbali kutoka
kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar
(AAKIA) waliofanya ziara ya mafunzo. Kushoto ni Msaidizi wa Mkuu wa
kitengo cha Ulinzi na usalama JNIA, Bw. Hamis Mashaka.
Maafisa
wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA),
Bw. Shaaban Kombo (kuanzia wa pili kulia), Bi. Zakhia Mohamed, Bw. Salehe Said
na Bi. Fatma Yussuf wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu
(kulia) akiwaelekeza jambo wakati wa ziara yao ya mafunzo iliyofanyika jana.
Msaidizi
wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), Bw. Hamis Mashaka (kushoto), akitoa maelezo mbalimbali
yanayohusiana na ulinzi na usalama kwa maafisa kutoka idara mbalimbali za
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) cha Zanzibar jana
walipofanya ziara ya mafunzo.
Meneja
Uendeshaji cha Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian (kulia) akiwapa
maelezo mbalimbali Maafisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Abeid Amani Karume (AAKIA) walipofanya ziara ya mafunzo jana.
Afisa
Habari katika jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (VIP-JNIA), Bw. Kenny Kwenga (kushoto) akitoa maelezo
ya namna watu mashuhuri wanavyohudumiwa kwa maafisa kutoka Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA), walipofanya ziara jana.
Kulia ni Msimamizi wa VIP, Bi. Josephine Mwaisukule.
Na Mwandishi Wetu
MAAFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na
usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.
Maafisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli
hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo
mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa husika.
Mkuu wa msafara wa maafisa hao, ambaye ni Mkuu wa
Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Bw. Shaaban Kombo alisema JNIA
inaulinzi madhubuti kwa abiria na mizigo hukaguliwa kwa kutumia mitambo maalum
kabla ya kupanda ndege au kuingia ndani ya jengo kwa kazi mbalimbali, ambapo
wameahidi kufuata nyayo hizo ili kuzuia uhalifu unaofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu.
Bw. Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya
msingi ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo
pia katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa
vitambulisho unavyofanyika, ukiwa ni tofauti na AAKIA ambao hutoa vitambulisho
vya kudumu mara baada ya taratibu kukakamilika, wakati JNIA hutoa vitambulisho
vya muda kwa muombaji ili aweze kuendelea na kazi, wakati akisubiri cha kudumu kikamilike
kutengenezwa.
“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu
hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja
anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la
kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda
kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika
matengenezo,” alisema Bw. Kombo.
Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha
JNIA, Bw. Lugano Mwansasu alisema ziara ya maafisa wa AAKIA imewafariji na
kuanza ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza
kulingana na maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.
Bw. Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), kuiga mfano huu wa kupeleka maafisa wake kwenye viwanja
mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la
kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo
chini ya serikali.
“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi
tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu
tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa
ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Bw. Lugano.
Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA,
Bw. Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na
mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.
Bw.Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika
kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na
masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.
EmoticonEmoticon