Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) akiwa katika kikao na
Maafisa Waandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alipofanya ziara
ya kukagua utendaji ambapo aliwataka kuchukua hatua dhidi ya watumishi
wasiowaaminifu wanaolikosesha Taifa mapato stahiki.
Meneja wa Idara ya Forodha,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bandari ya dar es Salaam, Bw. John
Micah (kulia) na Meneja anaye husika na suala la Mafuta Bw. Stephen
Malekano (kushoto) wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (hayupo pichani) alipofanya ziara Idara ya Forodha,
Bandarini, Jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Forodha Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), bandari ya Dar es Salaam, Bw. John Micah,
akifafanua jambo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb)(hayupo pichani), alipofanya ziara ya kushitukiza bandarini,
Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa
Maafisa waandamizi wa Mamlaka ya mapato Tanzania-TRA, alipofanya ziara
ya kushitukiza bandari ya Dar es Salaam na kuagiza kitengo cha ukaguzi
na upimaji wa mizigo bandarini kifumuliwe baada ya watumishi wake
kutofanyakazi ya kukusanya mapato ya Serikali ipasavyo.
Afisa Kitengo cha Bandari
Majahazi, Bw. Mahmood Makame, akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) kuhusu
changamoto ya elimu kuhusu masuala ya kodi kwa wateja wanaotumia Bandari
ya Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kushitukiza katika ofisi hiyo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
……………………………………………………………………………….
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika Kituo cha Forodha
Bandarini, kilichoko katika Bandari ya Dar es Salaam na kuiagiza Mamlaka
ya Mapato Tanzania TRA, kufanya mabadiliko makubwa ya watumishi walioko
katika idara ya upimaji na ukaguzi wa mizigo baada ya kubainika kuwa
baadhi yao wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na upotevu wa mapato
ya Serikali.
Dokta Mpango ametoa muda wa siku
saba kwa TRA kumpa taarifa kamili ya utekelezaji wa maagizo hayo,
ikiwemo kuwahamisha watumishi wote waliokaa muda mrefu kwenye eneo hilo
la upimaji na ukaguzi wa mizigo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji
mapato ya Serikali katika Bandari hiyo.
Ameshangazwa na kitendo cha
Mapato katika Bandari ya Dar es Salaam kutoongezeka licha ya juhudi
kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, kuboresha Bandari hiyo
kutokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kushirikiana na
wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi ya serikali.
“Pamoja na kuwepo kwa mitambo ya
kukagua mizigo (Scanners), baadhi ya bidhaa zinakadiriwa kodi ndogo
ikilinganishwa na thamani ya mizigo huku mizigo mingine ikiwa si ile
iliyotajwa kuwemo kwenye makontena na hupitishwa na watumishi wasio
waaminifu” alisisitiza Dokta Mpango.
Aidha, Waziri huyo wa Fedha na
Mipango ameuagiza ungozi wa TRA kuhakikisha kuwa wanaongeza mapato
katika bandari ya majahazi kutoka wastani wa mapato ya shilingi bilioni
3.5 kwa mwezi hadi shilingi bilioni 5, kulingana na malengo yaliyowekwa
baada ya kubainika kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa mapato ya Serikali
katika eneo hilo.
Dokta Mpango ameuambia uongozi
huo wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kuhakikisha kuwa Bandari ya Majahazi
ianze mara moja kutumia mfumo wa kukusanya mapato ujulikanao kama
TANSIS ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Aidha, ameviagiza vyombo vya dola
kuwachunguza watumishi wote wakiwemo wa ngazi za juu katika idara ya
forodha bandarini na kuwachukulia hatua kali wale wote watakao bainika
kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoikosesha Serikali mapato yake.
EmoticonEmoticon