Mkuu wa Wilaya Mkalama, awataka Bodaboda kuchangamkia fursa NMB

August 03, 2017

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng. Jackson Makata (mwenye miwani) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Mkalama. Wengine ni maofisa wa NMB na wageni waalikwa wakishuhudia tukio hilo.








Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng.Jackson Makata akizindua rasmi tawi la NMB wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng. Jackson Makata (mwenye miwani) pamoja na maofisa wa NMB wakifurahia mara baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Mkalama.

MKUU wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng. Jackson Jonasi Masaka, amewaagiza madereva wa boda boda kuanzisha na kusajili vikundi vya ujasiriamali, ili kujijengea mazingira mazuri kupata mikopo toka tawi la NMB benki, lililozinduliwa wilayani humo. Eng. Masaka ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye uzinduzi rasmi wa tawi la NMB tawi la Mkalama, lililopo katika makao makuu ya wilaya hiyo, Nduguti.
Alisema kufunguliwa kwa tawi hilo kumesogeza karibu zaidi huduma mbalimbali ikiwemo ya mikopo zinazotolewa na NMB benki, kwa wakazi wa wilaya hiyo. Akifafanua, alisema huko nyuma wakazi wa wilaya hiyo pamoja na watumishi wa umma, iliwabidi kufuata huduma za kibenki Singida mjini, umbali wa kilometa 140 kwenda na kurundi.
“Kwa hiyo ninyi madereva wa bodaboda, NMB imesongeza huduma...huu ni wakati muafaka kuboresha shughuli zenu. Msilale changamkeni, jiungeni kwenye vikundi vilivyosajiliwa muweze kupata mikopo itakayokuza mitaji yenu. Mjue tu kwamba dereva mmoja mmoja ni ngumu mno kupata mkopo kwenye taasisi za kifedha”, alisema mkuu huyo wa wilaya. Eng. Makata pia ametumia fursa hiyo kuwahamasisha baba/mama lishe, wauza chips na wajasiriamali mbalimbali wakiwemo wadogo, kuchangamkia mikopo kupitia akaunti ya ‘FANIKIWA’.
“Niipongeze NMB benki kwa kubuni bidhaa hii ya akaunti ya FANIKIWA. Kupitia akaunti hii ya FANIKIWA, wajasiriamali niliowataja hapo juu, wataweza kupata mikopo kati ya shilingi laki tano na milioni 30. Nasisitiza tumieni fursa hizi zilizosongewa karibu zaidi na NMB, ili mkuze mitaji yenu iweze kukidhi mahitaji ya wakati wa sasa,” alisema.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya ameishukru na kuipongeza NMB benki kwa msaada wake wa vitanda 15, magodoro 15, vitanda viwili vya kujifungulia akina mama wajawazito na mashine mbili za kupimia mapigo ya moyo.
“Msaada huu wenye thamani ya shilingi milioni 10 ambao umetolewa kwa kituo cha afya, vitunzwe na kulindwa vizuri ili viweze kutumika kwa kipindi kirefu,” alisema Eng. Makata. Awali meneja wa uhusiano wa biashara kati ya serikali na benki NMB kanda ya kati, Yasin Mfinanga, alisema msaada huo ni mwendelezo wa NMB katika kumuunga mkono Rais Dk. Magufuki kuboresha sekta ya afya.
“Kila mwaka baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji, benki yetu huwa inatenga asilimia moja ya faida, kwa ajili ya kutoa misaada inayolenga sekta ya afya na elimu. Agizo la rais Magufuli la kuchangia madawati katika shule za msingi na sekondari, NMB ilishiriki kikamilifu,” alisema Mfinanga kwa kujiamini.
Mfinanga alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa kanda ya kati, kuacha kabisa utamaduni wa kutunza fedha kwenye simu zao za viganjani na badala yake wazitunze kwenye mabenki ikiwemo ya NMB. Akisisitiza, alisema fedha zinazotunzwa kwenye simu za viganjani usalama wake ni mdogo mno, ikilinanishwa na zile zinazotunzwa kwenye mabenki ya kuaminika.
“Fedha hizi zilizopo kwenye simu za viganjani na wakazi wa kanda ya kati wakijitokeza kwa wingi kuweka fedha benki, hatua hiyo itachangia NMB benki kuwa na uwezo mkubwa katika kutoa mikopo. Aidha, hatua hii itachangia benki kupunguza riba zinazokatwa kwenye gharama za uendeshaji,” amesisitiza zaidi.
Wakati huo huo.mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama, James Mkwega, alisema kufunguliwa kwa tawi la NMB tawi la Mkalama, pamoja na mambo mengine, kutachochea ukuaji wa uchumi. “Binafsi nimefarijika mno…na naipongeza NMB benki kufungua tawi hapa kwetu Nduguti makao makuu ya wilaya ya Mkalama. Huko nyuma tulilazimika kufuata huduma za kibenki Singida mjini kilometa 140 kwenda na kurudi. Madhara yake yalikuwa makubwa mno,” alisema na kuongeza;
“Watumishi wa umma wakiwemo walimu nao wametaabika sana katika kufuata mishahara yao New Kiomboi wilaya ya Iramba umbali wa likometa 90. Hapo ilikuwa kabla wilaya Iramba yaijagawanywa na kuzaa wilaya ya Mkalama. Nakumbuka baadhi ya walimu walikuwa wanatumia usafiri wa baiskeli, wakifika msitu wa Gumanga, walikuwa wakiporwa mishahara yao na majambazi,”
Mwenyekiti huyo ambaye ni diwani (CCM) kata ya Gumanga, alisema kuwa kwa sasa hayo yote yatabaki kuwa histori, baada ya NMB kufungua tawi hilo.
___________________________________________________________________________________
Joachim Mushi, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Mhariri Mkuu wa Thehabari.com.
Mail address:- mushi@thehabari.com/ jomushi79@yahoo.com/ info@thehabari.com
Mobile:- 0717 030066 / 0756 469470
Web:- www.thehabari.com  
          http://joemushi.blogspot.com

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »