Na Jumia Travel Tanzania
Je ushawahi kupanga kwamba unataka kwenda kulala kwenye hoteli ya nyota ngapi? Ni vigezo gani ambavyo huwa unavitumia kutambua kwamba hoteli hiyo hadhi yake ni nyota fulani? Ni vigezo gani huja kwanza akilini pindi unapofanya uchaguzi wa hoteli hiyo? Ni maswali magumu ambayo mtu wa kawaida hawezi kuyajibu labda awe anajihusisha au kufanya kazi kwenye sekta ya hoteli au mtu anayesafiri mara kwa mara.
Mara nyingi linapokuja suala la kuchagua hoteli ya kwenda miongoni mwa vitu vinavyopewa kipaumbele ni pamoja na kiwango cha huduma za hoteli husika, miundombinu, vyumba, mahali ilipo na gharama.
Suala la kuzipa hoteli hadhi ya nyota fulani limekuwa likizua mijadala kwenye nchi tofauti kutokana na changamoto ya vigezo vinavyotumika kufanikisha zoezi hilo kutofautiana kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kwa mfano hoteli ya nyota nne kwa nchini Tanzania inaweza kuwa ni ya nyota mbili huko Misri kutegemea vigezo vilivyotumika. Katika kujaribu kutatua changamoto hiyo nchi nyingi duniani zimeunda mamlaka maalum kusimamia zoezi hilo ambapo mara nyingi huwa ni serikali au taasisi.
Hivi karibuni kampuni inayojihusisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao barani Afrika, Jumia Travel ilizindua ripoti ya Utalii mwaka 2017 ambapo ndani yake imebainisha kuwa kati ya hoteli zenye nyota moja mpaka tano watanzania wengi wanapendelea zaidi za nyota mbili (41%) na tatu (39%).
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa maeneo yanayotembelewa zaidi pamoja na gharama za hoteli zake ni Zanzibar (30%) ambapo chumba huanzia USD 134, Dar es Salaam (26%) gharama ni kuanzia USD 100, Arusha (10%) gharama ni kuanzia USD 50, Mwanza (4%) gharama ni kuanzia USD 34, Bagamoyo (3%) gharama ni kuanzia USD 58, Mbeya (2.5%) gharama ni kuanzia USD 24, Moshi (2%) gharama ni kuanzia USD 42 na Dodoma (1.5%) gharama ni kuanzia USD 23.
Intaneti imekuja kubadili mfumo mzima wa namna biashara na huduma mbalimbali zinazovyotolewa siku za hivi karibuni. Baadhi ya faida zake ni pamoja na kuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara kuwafikia na kuwakutanisha na wateja tofauti ndani ya muda mfupi, kujitangaza kwa gharama nafuu pamoja na kurahisisha namna ya upatikanaji wa huduma zao.
Jumia Travel katika ripoti yake hiyo kwa kutumia mtandao wake mpana wa hoteli takribani 1300 nchini Tanzania, zaidi ya 30,000 barani Afrika na zaidi ya 300,000 duniani kote, imekuwa ikihamasisha na kupendekeza mifumo rahisi kwa wamiliki na mameneja wa hoteli inayowawezesha kufanya shughuli zao muda na mahali popote walipo sio lazima mpaka wawe kwenye vituo vyao vya kazi.
Mfumo huo ambao unaitwa Extranet husaidia kupokea huduma kutoka kwa wateja, kukubali au kukataa, kupata maoni na pia kutambua wateja wao ni watu wa aina gani na wanapendelea huduma zipi zaidi kwenye hoteli wanazozitembelea. Hivyo huwa inawarahisishia kwenye kufanya maboresho kwenye maeneo ambayo wateja hawapendelei pamoja na kuongeza huduma ambazo wateja wanazipendelea lakini hawakuzipata.
Vivyo hivyo kwa upande wa wateja ambao hapo awali iliwabidi kwenda moja kwa moja hoteli au kutembelea tovuti moja baada ya nyingine kutafuta huduma sasa wamewezeshwa kufanya huduma za hoteli tofauti sehemu moja. Hivi sasa wanayo fursa kubwa ya kufanya huduma ya hoteli ndani ya muda mfupi mtandaoni kama vile kuchagua hoteli, mahali ilipo, aina ya chumba, bei, upatikanaji wake na namna ya kufanya malipo.
Ripoti hiyo iliangazia pia mchango wa sekta utalii nchini kwenye pato la taifa ambapo takwimu zinaonyesha kwamba 72.4% ya mapato hutokana na matumizi ya wageni wanaotoka nje ya nchi huku 27.6% hutokana na ya watalii wa ndani. Kwa kuongezea, 85.5% ya matumizi hayo ni kwa ajili ya kustarehe au kutalii huku 14.5% ni kibiashara.
EmoticonEmoticon