Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bi. Seriel
Mchembe mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) kwa ziara ya
kikazi ya siku moja. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen
Kebwe. (Picha na OWM).
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Gairo, Bw. Ahmed
Shabiby mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) kwa ziara ya
kikazi ya siku moja. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt.
Stephen Kebwe nawa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bi. Seriel
Mchembe (Picha na OWM).
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw.
Cliford Tandari mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) kwa
ziara ya kikazi ya siku moja. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya
Mvomero. (Picha na OWM).
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akipanda mti nje ya Ofisi ys Mkuu wa Wilaya ya Gairo
mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017) ikiwa ni sehemu ya
kuadhimisha Siku ya Upandaji Miti Kitaifa. Wengine ni viongozi wa Mkoa
na Wilaya wakishuhudia. (Picha na OWM).
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akimwagilia mche alioupanda nje ya Ofisi ys Mkuu wa
Wilaya ya Gairo mara baada ya kuwasili wilayani humo (Juni 3, 2017)
ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Upandaji Miti Kitaifa. Wengine ni
viongozi wa Mkoa na Wilaya wakishuhudia. (Picha na OWM).
Viongozi na
watumishi wa Wilaya ya Gairo wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
(hayupo pichani) katika mkutano aliouitisha mjini Gairo Juni 3, 2017.
(Picha na OWM).
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi na watumishi wa Wilaya ya Gairo
(hawapo pichani) katika mkutano aliouitisha mjini Gairo Juni 3, 2017
(Picha na OWM).
………………………………………………………………………………………..
* Ni la sh. milioni 213/- la fedha za maendeleo.
*Ataka apewe taarifa ifikapo Juni 30.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Clifford Tandari
aitishe kikao na uongozi wa Halmashauri ya Kilosa na kupata kauli yao ni
lini watalipa zaidi ya sh. milioni 210 wanazodaiwa na Halmashauri ya
Gairo.
“Katibu Tawala itisha kikao cha
Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri,
waseme ni lini watazileta fedha hizo ambazo zilitumwa kwao wakati
Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ikiwa haijafungua akaunti zake,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi,
Juni 3, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Morogoro, wilaya
ya Gairo na watumishi wa Halmashauri ya Gairo mara baada ya kupokea
taarifa ya mkoa na wilaya katika kikao kilichofanyika Gairo mjini
“Kilosa ni lazima wazilipe hizo
fedha. Katibu Tawala simamia zoezi hilo na kama watachelewa, uzikate
moja kwa moja kwenye fedha yao wanayoletwa kutoka Ofisi ya Rais
(TAMISEMI). Nataka nipewe taarifa ya maamuzi hayo kabla Juni haijaisha,”
amesema.
Mapema akitoa taarifa ya wilaya
hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bi. Siriel Mchembe alisema wanaidai
Halmashauri ya Kilosa sh. 233,228,679 ambazo ziliingizwa huko wakati
wilaya hiyo inaanzishwa na hawakuwa wamefungua akaunti ya wilaya.
“Fedha hizi zilikuwa zinapitia
Kilosa wakati wilaya ya Gairo imeanzishwa kwa kuwa kipindi hicho wilaya
ya Gairo ilikuwa bado haijafungua akaunti. Fedha hizi zinajumuisha
ruzuku ya uendeshaji, mapato ya ndani na miradi ya maendeleo,” alisema.
Alisema Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC) iliagiza wilaya ya Kilosa ilipe deni hilo
kabla ya Juni 2016 lakini hadi sasa wameshalipa sh. milioni 20 tu ambapo
sh. milioni 10 zililipwa Desemba 2015 na nyingine milioni 10 zililipwa
Mei 2017.
Akisisitiza kuhusu makusanyo ya
mapato, Waziri Mkuu amewakumbusha watumishi hao kuwa Serikali
imekwishatoa agizo la kutumia mashine za kielektroniki kukusanya mapato
ifikapo Julai mosi.
“Makusanyo ya mapato ya ndani ni
eneo muhimu sana. Tumeshaagiza, mwisho wa kutumia mifumo ya kawaida ni
Juni 30. Kuanzia Julai mosi, kila eneo ni lazima litumie mashine za
kielektroniki,” alisema Waziri Mkuu.
Alihoji ni kwa nini Halmashauri
ya Gairo ililenga kukusanya sh.milioni 889.5 lakini kufikia Aprili mwaka
huu, makusanyo halisi yalikuwa ni sh. milioni 356.2 sawa na asilimia
40.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza
Mamlaka ya Mapato (TRA) ya wilaya hiyo ambao hadi kufikia Aprili, 2017
wameweza kukusanya sh. milioni 601.5 ikilinganishwa na makadirio yao ya
kukusanya sh. milioni 471 kwa mwaka. Waziri Mkuu aliwapongeza kwa sababu
wamevuka lengo kwa asilimia 127.6.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye
ziara ya siku ya wilaya hiyo, asubuhi alipanda mti kwenye Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya ikiwa maadhimisho ya siku ya upandaji miti hapa nchini.
Pia alikagua mradi wa maji wa
kijiji cha Chakwale, na mradi wa visima 10 ambayo imekuwa na mgogoro kwa
muda mrefu. Pia atazungumza na wananchi wa Gairo mjini kwenye mkutano
wa hadhara.
EmoticonEmoticon