RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ametoa wito kwa Baraza la Wauguzi na Wakunga la Zanzibar kusimamia vyema
Sheria ya Baraza hilo sambamba na maadili kwa lengo la kuwahudumia
vyema wananchi na kuzifanya huduma za afya zizidi kuimarika na kuendelea
kuijengea sifa Zanzibar kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.
Dk.
Shein, aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Wajumbe wa
Baraza la Wauguzi na Wakunga waliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya
kujitambulisha kwa Rais wakiwa wameongozana na uongozi wa Wizara ya
Afya chini ya Waziri wa Wizara hiyo Mahmoud Thabit Kombo.
Katika
maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza Wajumbe hao haja na umuhimu mkubwa wa
kuipitia na kuisoma vyema vifungu vyote na hatimae kuifanyia kazi
Sheria ya Baraza la Wauguzi na Wakunga la Zanzibar ya mwaka 2014 ili
waweze kuliongoza vyema na kwa ufanisi zaidi Baraza hilo.
Dk.
Shein, alisema kuwa iwapo Sheria hiyo itasimamiwa vyema fani ya Uuguzi
itaendelea kuwa na mafanikio makubwa sana hapa Zanzibar.
Alieleza
matumaini yake makubwa kwa wajumbe hao ambao wamechaguliwa kutokana na
kuwa kazi hiyo wanaiweza na kuwapongeza kwa kufanya mambo mengi tokea
kuzinduliwa Baraza hilo lenye Wajumbe 13 Mrajis na wasaidizi wake wawili
mmoja Pemba na mmoja Unguja mnamo mwezi June mwaka 2015.
Aidha,
Dk. Shein alisisitiza suala zima la maadili ambalo ndio jambo muhimu
katika fani yoyote duniani na kueleza kuwa katika fani ya Uuguzi suala
la maadili ndio jambo la kulipa kipaumbele ili kuweza kutoa huduma nzuri
ya afya kwa jamii.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuwepo kwa usimamizi katika
suala zima la uuguzi kwani hatua hiyo itaipelekea Zanzibar iweze
kutajika na kuirudisha katika hali yake ya zamani ambapo wananchi kutoka
ndani na nje ya Zanzibar walikuwa wakija hapa nchini kufuata huduma za
afya.
Akieleza
suala zima la upungufu wa wauguzi, Dk. Shein alisema kuwa upungufu wa
wauguzi ni suala la muda mrefu na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha inatatua changamoto
hiyo hatua kwa hatua.
Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Baraza hilo kwa hatua yake
ya kusimamia vyema suala la mafunzo kwa wauguzi ambapo tayari kwa
maelezo ya Wajumbe hao kuna wauguzi 893 wenye Diploma ya Uuguzi, 97
wenye Digirii ya Kwanza, 25 wenye Digrii ya Pili na 1 anaefanya Shahada
ya Uzamivu (Phd) katika kada hiyo.
Aliongeza
kuwa kwa kutambua umuhimu wa kada hiyo, Baraza lina kazi kubwa ya
kuteua Kada muhimu za mafunzo katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA) sambamba na wajibu mkubwa wa kusimamia utafiti.
Katika
kutilia mkazo jambo hilo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar chini ya uongozi wake imeamua kwa makusudi kuanzisha
Taasisi ya Utafiti ya Afya kwa kutambua kuwa utafiti husaidia kutoa
huduma bora za matibabu katika sekta ya afya.
Mapema
Waziri wa Wizara ya Afya Mahamoud Thabit Kombo alieleza kuwa mkutano
kati ya Rais pamoja na Baraza hilo umekuja wakati muwafaka ambapo Wizara
yake imeahidi mambo mbali mbali katika Baraza la Wawakilishi
linaloendelea na kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Wizara na Baraza
hilo yanaweza kutekeleza kile alichokiahidi katika Baraza hilo hivi
karibu katika Bajeti yake.
Waziri
Kombo alieleza miongoni mwa changamoto ni pamoja na kuwekwa pembeni
maadili ya uuguzi, lugha isiyofaa zidi ya wagonjwa, wagonjwa kutozwa
fedha za dawa ambazo zipo hospitalini na zimenunuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili yao mambo ambayo ameahidi kuyavalia
njuga katika kupambana nayo kwa mashirikiano na Baraza hilo.
Nae
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid
Yahya Mzee alieleza haja ya kujua mahitaji ya wauguzi pamoja na upangaji
wa wauguzi katika hospitali za hapa nchini kwani licha ya kuwepo kwa
idadi ndogo ya wauguzi lakini suala zima la usimamizi limekuwa
likikosekana katika eneo hilo kama ilivyo kwa taasisi nyengine za
Serikali.
Dk.
Abdulhamid alisisitiza kuwa licha ya Utumishi kufanya juhudi za
makusudi katika sekta ya afya lakini kinachoonekana ni kuwa wengi
wanaoajiriwa katika sekta hiyo hufanya kazi kinyume na ajira yao na
ndipo unapotokea upungufu wa wafanyakazi huku akieleza kuwa ni vyema
mafunzo yakawa yanaleta mabadiliko ya kiutendaji kwa watendaji wa kada
hiyo ya Uuguzi pamoja na kada nyengine ndani ya taasisi za Serikali.
Nae
Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi Amina Abdulkadir Ali alitumia fursa hiyo
kutoa historia kwa ufupi ya Baraza hilo hapa Zanzibar pamoja na hatua,
utekelezaji na maendeleo ya kazi za Baraza sambamba na mafanikio na
changamoto zilizopo.
Akitaja
miongoni wma mafanikio, Bi Amina aliseama kuwa ni pamoja na kupata
ofisi na vitendea kazi, kuweza kufungua akaunti,kudumisha mashirikiano
na Wauguzi wa Tanzania Bara pamoja na wale wa nchi za Afrika ya
Mashariki na Jumuiya za Kimataifa.
Aliongeza
kuwa kuweza kuwachukulia hatua kwa onyo au kusimamisha kwa wauguzi
waliokuwa na makosa ya maadili na kosa la kughushi vyeti, idadi ya
wanafunzi wanaotaka kusoma Uuguzi imeweza kuongezeka ikilinganishwa na
miaka miwili iliyopita sambamba na kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani
tarehe 12, Mei mwaka huu huko Pemba kwa pesa za Baraza kupitia Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar bila ya kuwahusisha wahisani.
Hiyo
inatokana na ahadi yake Waziri wa Afya ya kushuka chini Ngazi ya
Utendaji ili kuhakikisha ufanisi, Uwajibikaji na Usimamizi na kuwataka
Watendaji wote waungane nae mkono badala ya kulalamika kuwa wanaingiliwa
katika majukumu Yao.
Majukumu
yote ya Wizara ya Afya na Hospitali pamoja na Vituo vyake vyote Vya
Afya vipo chini ya Dhamana ya Wizara Ya Afya ambapo yeye Waziri wa Afya
ndiye aliye na Dhamana Kuu ya Wizara hiyo katika Usimamizi na Utendaji
ulio bora katika kutoa Huduma kwa Wananchi wote wa Zanzibar bila ya
Ubaguzi wa Aina yoyote. Pia Mhe. Waziri wa Afya ametoa tamko la
kushirikisha Kitengo cha Huduma kwa Jamii na Ustawi Wa Jamii
kushirikishwa kikamilifu pale panapokuwa na tatizo ama upungufu wa
Huduma au Mawasiliano kwa Wagonjwa na Wauguzi wanaotokana na Familia zao
EmoticonEmoticon