Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa Tatu kushoto), Mkuu
wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wa kwanza kulia), Mbunge wa
Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kulia), Mbunge wa Kibaha
Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-hanga (wa
kwanza kushoto) wakifunua Jiwe la Msingi kuashiria uzinduzi wa mradi wa
Usambazaji Umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa
Pwani. Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika katika kijiji cha Msufini mkoani
humo.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), Mkuu wa mkoa
wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wa kwanza kushoto), Mbunge wa
Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kushoto), Mbunge wa Kibaha
Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa (wa nne kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-hanga wakifurahia
uzinduzi wa mradi wa Usambazaji Umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA
III) katika mkoa wa Pwani. Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika katika
kijiji cha Msufini mkoani humo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Usambazaji Umeme
vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Pwani. Wengine katika picha
ni Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wa kwanza kushoto), Mbunge
wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kushoto), Mbunge wa Kibaha
Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa (wa nne kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), Mhandisi Gissima Nyamo-hanga.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Usambazaji Umeme vijijini
wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Pwani. Kulia kwa Waziri ni Mbunge wa
Kibaha Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa na kushoto kwa Waziri ni Mbunge wa Chalinze,
Mhe. Ridhiwani Kikwete. Wengine katika picha ni viongozi kutoka Mkoa wa Pwani,
TANESCO, REA na kampuni ya Steg International Services itakayotekeleza sehemu ya kwanza
ya Mradi huo.
Watendaji kutoka kampuni ya Steg
International Services wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini (hayupo
pichani) wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
katika mkoa wa Pwani. Kampuni hiyo itatekeleza sehemu ya kwanza ya Mradi huo wa
Awamu ya Tatu.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(mwenye fulana ya Bluu) na Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakifukia
nguzo ya umeme kwa udongo ikiwa ni ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa
Usambazaji Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu katika mkoa wa Pwani.
Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia
Umeme, Mhandisi Salum Inegeja (wa kwanza kushoto) na Kamishna Msaidizi wa
Madini, Kanda ya Mashariki, Julius Sarota (wa pili kushoto) wakifuatilia
shughuli ya uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu
katika mkoa wa Pwani.
Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, amezindua mradi wa Usambazaji Umeme
vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Pwani ambao utawezesha
vijiji mbalimbali katika mkoa huo kupata huduma ya Umeme.
Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika katika kijiji cha
Msufini mkoani humo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa mkoa
wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete
na Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mhe.Hamoud Jumaa.
Uzinduzi wa mradi huo ulienda sambamba na utambulishaji wa Mkandarasi
atakayetekeleza sehemu ya kwanza ya Mradi huo ambaye ni kampuni ya Steg International Services.
Kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), Mhandisi Gissima Nyamo-hanga alieleza kuwa Mradi wa Usambazaji Umeme
Vijijini wa Awamu ya Tatu unahusisha vipengele Mradi vitatu vya utekelezaji.
Alisema kuwa kipengele cha kwanza cha utekelezaji kitahusisha kufikisha umeme kwenye vijiji
ambavyo havijafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme wa gridi na kipengele cha
Pili kitahusika na kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo
vimefikiwa na miundombinu ya umeme.
“Kipengele cha Tatu katika Mradi huu kitahusika na
usambazaji wa nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi, ambayo ni
vigumu kufikiwa na umeme wa gridi yakiwemo maeneo ya Visiwa”, aliongeza Mhandisi
Nyamo-hanga.
Alisema kuwa Utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Pwani utahusisha vipengele vyote vitatu na
utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza itahusisha
upelekaji umeme katika vijiji 204 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 30.2 ambapo
utekelezaji wa sehemu ya kwanza umeanza Mwezi Februari 2017 na unatarajiwa
kukamilika Machi 2019.
Mhandisi Nyamo-hanga alitoa wito kwa wananchi watakaounganishiwa umeme
kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili wakati mkandarasi
atakapofika katika maeneo yao, wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, alisema kuwa
utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini imefanyika kwa ufanisi kwani katika mwaka
2007 ni asilimia 2.5 tu ya watanzania waishio vijijini walikuwa na umeme lakini
mpaka mwisho wa mwaka 2016, upatikanji wa umeme vijijini ulifikia asilimia 49.5.
Alisema kuwa, Watanzania wana haki ya kujivunia miradi hiyo inayofadhiliwa
na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutekelezwa na TANESCO, kwani ni ya kipekee
duniani kutokana faida zake kwa wananchi wa vijijini ambapo gharama mbalimbali zinabebwa na Serikali huku mwananchi
akitakiwa kulipia shilingi elfu 27,000 ili aunganishiwe umeme.
Alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa miradi hiyo, bajeti iliyotengwa kwa
mwaka wa Fedha 2016/17 ili kusambaza
umeme vijijini ni zaidi ya shilingi Trilioni moja.
Kuhusu hali ya Umeme katika mkoa wa Pwani, aliwaagiza watendaji wa TANESCO na wataalam
kutoka Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo, kujadiliana ili kufahamu mahitaji halisi ya
umeme, hasa ikizingatiwa kuwa kuna viwanda vinavyoendelea kujengwa na vilivyopo
ambavyo vinahitaji si chini ya megawati 60.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutodai fidia katika miradi ya Umeme, kutokana na umuhimu wake katika huduma za
kijamii kama vituo vya Afya, Shule, majumbani na shughuli za kiuchumi ili
kuleta mapinduzi katika maisha ya wananchi hao.
Wabunge pamoja na Mkuu wa mkoa wa Pwani, walipongeza juhudi za usambazaji
umeme nchini zinazofanywa na Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Profesa
Muhongo na kutumia fursa hiyo kueleza changamoto mbalimbali zinazopaswa
kushughulikiwa na Serikali ili wananchi pamoja na viwanda viweze kupata umeme
wa uhakika.
EmoticonEmoticon