Sport Azam U-20 kuanza na Mbao Ligi ya Vijana kesho

November 16, 2016

Team: 
Azam B
TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam U-20’, kesho saa 8.30 mchana inatarajia kuanza kutupa karata ya kwanza kwenye Ligi ya Taifa ya Vijana kwa kukipiga dhidi ya Mbao katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera.
Azam U-20 iliyojiandaa vema kuelekea michuano hiyo, imepangwa kwenye kituo cha Bukoba chenye timu nane kinachounda Kundi A, kikiwa na timu nyingine za Kagera Sugar, Toto African, African Lyon, Mwadui, Stand United na Yanga.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Idd Cheche, alisema kuwa wamejipanga vilivyo kuanza vema michuano hiyo kwa kupata ushindi kesho.
“Kikosi changu kipo kamili kwa ajili ya michuano hiyo, kimefanya maandalizi mazuri na malengo yetu makubwa ni kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kituo hiki na hatimaye kuibuka mabingwa,” alisema.
Cheche aliwatoa hofu mashabiki wa Azam FC kwa kuwaaambia kuwa wakae mkao wa kula kutokana na ubora wa timu yao na ipo vizuri kwa ajili ya kushindana na hatimaye kutwaa ubingwa.
Mabingwa hao wa kihistoria wa michuano ya awali ya vijana ya Uhai Cup, wanatarajia kung’arishwa vilivyo na baadhi ya mastaa wake wakiwemo mshambuliaji Shaaban Idd na kiungo Masoud Abdallah, ambao pia wamepandishwa kucheza kwenye timu ya wakubwa ya kikosi hicho.
Tayari mchezo wa ufunguzi wa kituo hicho umefanyika jana, ambapo ilishuhudiwa Kagera Sugar ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga huku leo Jumatano ukitarajiwa kupigwa mtanange mwingine utakaohusisha watani wa jiji la Shinyanga, Stand na Mwadui.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »