Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), limesambaza
waraka mpya kwa wanachama wake, likiwamo Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ukisema mameneja wote wa usajili wa wachezaji kwa mfumo
wa Mtandao (TMS-Transfer Matching System Managers) hawana budi kujiunga
na mawasiliano mapya ili kupata taarifa mbalimbali za usajili na
uhamisho wa wachezaji.
FIFA limeleta mfumo huo unaoitwa GPX yaani Global Players Exchange
ambao malengo yake ni kurahisisha kufanya usajili kwa mchezaji mmoja
kwenda timu nyingine lakini kabla ya kufanya hivyo utasaidia kupata
taarifa kamili za mchezaji huyo na shabaha kuu ni kurahisisha
mawasiliano ya TMS Managers nchi nzima, klabu na mashirikisho mbalimbali
duniani.
GPX ni kama mtandao wa kijamii unaoweza kulinganishwa na ‘WhatsApp’
unaofanya kuwa na mawasiliano ya karibu na FIFA imeagiza kuwa ni lazima
mameneja wa TMS wa kila klabu na mashirikisho ya ya mpira wa miguu
kujiunga na mtandao huo ambao si tu kwamba utafanya kazi katika nchi
husika, bali pia unaunganisha ulimwengu wote.
Kwa mameneja wa usajili wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (SFDL) na Ligi Daraja la Pili
(SDL) watakaokuwa tayari basi hawana budi kuwasiliana na Meneja Usajili
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupata maelezo ya kina ya namna
ya kujiunga na mtandao wa GPX.
EmoticonEmoticon