Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
chini ya Makamu Mwenyekiti Wakili, Jerome Msemwa leo imetoa maamuzi ya
shauri la upangaji wa matokeo wa kundi C kwa Ligi Daraja la Kwanza
(StarTimes League).
Akisoma hukumu hiyo baada ya kumaliza kuwahoji viongozi wa vilabu na
wenyeviti wa vya vyama vya mpira wa miguu vya mikoa jana, Wakili Msemwa
amesema adhabu hizo zimetolewa kwa kufuata Kanuni za Nidhamu za TFF, na
nafasi ya kukata rufaa kwa wahusika juu ya maaamuzi hayo ziko wazi.
Klabu za Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora
(Tabora) zimekutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya
kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao.
Upande wa klabu ya JKT Kanembwa FC ya mkoani Kigoma, imeshushwa
daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL), baada ya kushika nafasi
ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C.
Kamati ya Nidhamu imewafungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu
mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola
na kamisaa wa mchezo huo Moshi Juma baada ya kukutwa na hatia ya upagaji
matokeo.
Aidha kamati pia imemkuta na hatia kocha msaidizi wa klabu ya Geita
Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu
Magolikipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita
Gold wamefungiwa miaka 10 kutojihusisha na mpira wa miguu sambamba na
kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kila mmoja.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum
Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu
wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa huru na Kamati ya
Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Yusuph
Kitumbo, Katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Fateh
Remtullah, Mwenyekiti wa klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha
msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian wamefungiwa maisha
kutojihusisha na mpira wa miguu.
Mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi Tabora v JKT Oljoro, Masoud Mkelemi
na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde wamefungiwa kwa muda wa miaka kumi
kutojihusisha na mpira wa miguu, na kutozwa faini ya shilingi milioni
(10,000,000) kumi kila mmoja.
Katibu wa klabu ya Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT
Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora,
Boniface Komba, na Meneja wa timu ya Polisi Tabora, Mrisho Seleman,
wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia.
Kutokana na maamuzi hayo ya Kamati ya Nidhamu ya TFF, Kamati husika
zitakaa kupitia Kanuni na kutangaza timu itakayopanda Ligi Kuu (VPL)
msimu ujao na timu zitakazopanda Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes) msimu
ujao.