SERIKALI imetia saini ya makubaliano
baina yake na Kampuni ya Saruji ya Simba iliyopo Jijini Tanga kwa lengo la Kampuni
hiyo kuanza kusafirisha shehena za mizigo kwa kutumia njia ya reli ili kuokoa
athari za uharibifu wa Barabara zinazojitokeza kwa sasa kutokana na
usafirishaji kwa kutumia malori.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania(TRL)Masanja Kadogosa na
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Saruji ya Simba Reinhardt Swart wakishuhudiwa na
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa.
Akizungumzia hatua hiyo Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa alisema kwa sasa serikali
inatumia shilingi milioni moja kwa kila kilometa moja ya Barabara kiasi ambacho
ni kikubwa ukilinganisha na gharama ambazo zingetumika kwa ajili ya kuboresha
njia za reli.
Prof.Mbarawa alisema Kampuni hiyo itakuwa
ikisafirisha tani 35,000 sawa na tani 500,000 kwa mwaka ambapo TRL itakusanya shilingi milioni 40 kwa
kila mzigo jambo ambalo litarudisha uhai wa njia za reli na kuondoa uharibifu
wa Barabara.
“Kwa mwezi magari haya makubwa yaani
malori yanayobeba mizigo yanafanya zaidi ya tripu 3,500 sawa na tripu 35000 kwa
mwaka sasa jiulize ni kwa namna gani Barabara zinaharibika na kusababisha
gharama kubwa sana za ukarabati kwa serikali ….hivyo tunaamini mazungumzo yetu
yataenda vizuri na kufika tulikokusudia”,alisema Waziri huyo.
Aliwataka watumishi wa Kampuni ya
Reli (TRL)kufanya kazi kwa bidii hasa kwa kutambua kuwa kampuni hiyo ndiyo moyo
wa uchumi wa nchi katika sekta ya usafirishaji na kamwe serikali haitamvumilia
mtumishi mzembe kwenye sekta hiyo.
“Lazima wafanyakazi mshirikiane na
kila mmoja ajitume katika kutimiza wajibu wake bora niwe na wafanyakazi
wachache hata ishirini wenye kuliko kukaa hapa na watu wanaoiba dizeli na oili
kama mtu hawezi na aondoke hatuwezi kuendelea kufanya kazi kwa mazoea na
kuharibu shirika hili ambalo ni tegemeo la kiuchumi kwa Taifa”,alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TRL Masanja Kadogosa akizungumza hivi karibuni alisema kuwa kwa mwaka
2014/2015 Kampuni ya Saruji ya Simba Tanga ilisafirisha shehena ya mizigo tani
44,000 ambapo kutoka Julai hadi Disemba 2015 ilisafirisha tani 24,960.
Kadogosa alisema katika kufufua
Kampuni hiyo ya TRL serikali imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani
Milioni 100 sawa Bilioni 200 za kitanzania huku ikilenga kuboresha huduma
mbalimbali ikiwemo matengenezo ya miundo mbinu ya njia za reli.
Naye MKurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha
saruji Swart alisema kuwa hatua hiyo itapunguza gharama za usafirishaji wa
shehena za mizigo ya saruji ambapo katika safari zake wanatarajia tani 20,000
za saruji kutoka Pongwe kwenda Kigoma na tani 15,000 kutoka Pongwe kwenda
Mwanza.
“Uzalishaji wa saruji kwa mwezi ni
tani 105,00 na tunatarajia kusafirisha tani 35,000 kila mwezi kwenda mikoa
mingine tukiamini njia hii itakuwa ni nafuu zaidi,”,alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa
Tanga Martine Shigella aliwahakikishia wamiliki wa kiwanda hicho kwamba
serikali ya mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha inaimarisha ulinzi na usalama wa
mizigo yao ili kusitokee hujuma wakati wa usafirishaji.
“Tunajua kuna hujuma za wizi wa
mizigo na mataruma ya reli lakini kama mkoa tutahakikisha tunapambana na hali
hiyo kwa hali na mali ,”alisisitiza Shigella.