Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72)
imekutana jana (Februari 16, 2016) kupitia taarifa za mechi mbili za
Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kati ya JKT Kanembwa na
Geita Gold SC, na Polisi Tabora na JKT Oljoro ambapo Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) lilisimamisha matokeo yake hadi taarifa hizo
zitakapopitiwa.
JKT Kanembwa ilifungwa mabao 8-0 na Geita Gold SC katika mechi
iliyofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi
Tabora ilishinda mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Baada ya kupitia taarifa hizo na vielelezo vingine, Kamati ya
Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeonyesha mashaka kutokana na kuwepo
viashiria vya upangaji wa matokeo (match fixing).
Kwa vile suala hilo
linahusisha masuala ya kinidhamu, na kwa kuzingatia Ibara ya 50(1) na
(11) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 69 ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Kamati
ya Saa 72 imemuelekeza Katibu Mkuu wa TFF apeleke suala kwenye Kamati
ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya uchunguzi na hatimaye kufanya uamuzi.