Mheshimiwa
Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza
inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo
hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao,
kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi
huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika.
Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu
roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu
na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati
wa mchakato wa uchaguzi huu.
Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job
Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa
kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani
yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu
makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge
letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.
Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa
wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale
wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata mbalimbali
kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu
mbili:
- Kwanza, ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
- Pili, nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa
Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi
tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba
yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni.
Nataka Wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi
kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani
yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani pia watafanya hivyo hivyo
kama tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa shukrani zangu za
dhati kabisa kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa
ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana kampeni
za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume
na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na utulivu
mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga kura.
Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa,
na hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu
walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.
Wale waliotarajia kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa
wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni Waafrika
wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara nyingine tena tumedhihirisha,
kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa cha Amani
katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea
nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya nchi
yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi
wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.
Aidha, napenda niungane na ninyi pamoja na Watanzania
wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa pamoja
na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea
kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi.
Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna
walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua za awali za kujiandikisha
hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu wenu
kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na yenye changamoto
nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu
wa nchi yetu walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi
yetu. Natambua mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na
Mzee Karume kwa kujenga misingi imara wa umoja, mshikamano na amani
ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi
na kisiasa na kuijenga misingi yake. Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi)
kwa kupanua na kuimarisha misingi ya uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee
Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza misingi hiyo na kupanua
fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao. Wamefanya kazi
kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha marefu ili
tuzidi kuchuma busara zao.
Mhishimiwa
Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja, tumeshindana katika
kampeni tukiwa wamoja, na tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja. Nataka
niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali
ya Awamu ya Tano itaendelea kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi za Umoja na Amani.
Hatutakuwa na simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga
umoja na amani yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila, vyama au ukanda.
Mheshimiwa
Spika;
Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza kwa
kulalamikiwa sana na wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo
yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni pamoja na:
- Rushwa - Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa wananchi.
- TAMISEMI - Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k.;
- Ardhi – Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;
- Bandari - Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;
- Maji – Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji kupatikana mbali na makazi, n.k.;
- TRA - Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara wakubwa;
- TANESCO - Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;
- Maliasili na Utalii - Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;
- Huduma za Afya (Hospitali) - Huduma kuwa mbali na wahitaji, Ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, n.k.;
- Uhamiaji na Ajira - Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi nchini kwa wageni, Kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, n.k.;
- Elimu - Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;
- Polisi - Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari, Ukosefu wa nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;
- Zimamoto – Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea kazi kama maji, n.k.;
- Mizani – kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;
- Mahakama - Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa kesi. Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.
- Madini – Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia, n.k;
- Kilimo na Mifugo – Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la masoko, Kukopwa mazao ya wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa Maghala, Mabwawa, Malambo, Majosho, n.k.;
- Uvuvi – Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi hususan viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa bahari;
- Reli – Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa reli, upungufu wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara, n.k.;
- ATC – Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa mishahara ila ndege ni moja (1);
- Makundi Maalum – Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa;
- Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo – Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, Haki na maslahi yao, n.k.;
Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi
na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi
ya kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue na mshirikiane
na Serikali na wadau wengine tuzitatue haraka.
Pamoja na kero hizo tutashughulikia pia mambo yafuatayo.
Kuimarisha
Muungano
Mheshimiwa
Spika;
Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini
wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa
huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa
hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani.
Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu,
amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi
Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar
na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo
kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu.
Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha
kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama
na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize
kwa utulivu na amani.
Serikali nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani
ya uwezo wake kuendelea kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa
Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake
ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia
Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja
na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed
Shein tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.
Kuimarisha
Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaheshimu na kuendeleza
utamaduni mzuri uliojengeka nchini wa kuheshimu mihimili ya dola. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata
fedha za kutosha kuendesha shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa
Bunge na Mfuko wa Mahakama. Kwa upande wa Bunge, tutahakikisha fedha
za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinapatikana kwa wakati ili Waheshimiwa
Wabunge mkashirikiane na wananchi wenu kusukuma maendeleo. Kwa upande
wa Mahakama, tutalipa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa Mahakama kwa
kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, kuongeza kasi ya utoaji
haki na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama zetu.
Mchakato
wa Katiba
Mheshimiwa
Spika;
Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba
ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika
kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini
kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya
awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho
ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza
wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.
Uchumi
na Matarajio ya Wananchi
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kukiwa
na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika Awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika
na kukua wastani wa asilimia 7. Katika kipindi
hicho fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa.
Hii ni kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali za Awamu zilizopita
za kujenga miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, uimarishaji wa
bandari, uimarishaji wa reli, na ukuzaji wa sekta za mawasiliano ya
simu na mitandao, ukuzaji na uongezaji wa uwezo wetu wa kuzalisha na
kusambaza umeme.
Napenda kuwahakikishia kuwa tutaendeleza na kuimarisha
ujenzi wa miundombinu mipya na kuiimarisha iliyopo ili kuvutia na kushawishi
wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mheshimiwa
Spika;
Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa ahadi tulizowaahidi Watanzania ni kuendeleza ujenzi
wa barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya;
barabara ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na
upanuaji wa barabara za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga flyovers, barabara za
pete (ring roads), n.k. Uboreshaji
wa barabara na njia nyingine za uchukuzi na usafirishaji kuingia na
kutoka Dar es Salaam ni muhimu sana kwa sababu bandari ya Dar es salaam
ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi jirani.
Mheshimiwa
Spika;
Katika jitihada hizo hizo za kuboresha na kuimarisha
miundombinu ya kiuchumi Serikali ya Awamu ya Tano, katika
kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa reli mpya
katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge). Reli ambazo tunakusudia
zianze kujengwa ni:
- Dar es Salaam – Tabora – Kigoma/Mwanza
- Uvinza – Msongati (Burundi) na Isaka – Kigali (Rwanda)
- Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga;
- Tanga – Arusha – Musoma
- Kaliua – Mpanda – Karema
Mheshimiwa
Spika;
Nchi yetu pia imejaliwa kuwa na madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi asilia umeongeza matumaini
ya watu wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi katika miaka ijayo.
Serikali itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa
manufaa ya Taifa letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo. Aidha,
napenda kuipongeza kwa dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete
na Bunge la 10 kwa kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta
na Gesi yaani The Oil and
Gas Revenues Management Act, 2015. Serikali yangu itasimamia
utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini mkubwa.
Ujenzi
wa Viwanda
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda. Natambua
kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda.
Hatuna njia nyingine kama kweli tunataka kujenga msingi wa uchumi endelevu
katika nchi yetu utakaopaisha uchumi na maisha ya watu wetu. Dira ya
Maendeleo ya 2025 inatutaka tuwe nchi ya watu wenye kipato cha kati.
Tunaweza tukafika huko, na dalili zipo, lakini pia tunaweza tukafika
huko kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia wa mambo ni tofauti. Utofauti
ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha kwamba sisi ni nchi
ya kipato cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha ya watu wengi
hazifanani na takwimu hizo. Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali
ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati
ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi
ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa
viwanda.
Mheshimiwa
Spika;
Tutahakikisha suala la viwanda linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa.
Matarajio yangu ni kuwa Bunge lako Tukufu litatuunga mkono mimi na Serikali
nitakayoiunda katika kufikia lengo hili.
Mheshimiwa
Spika;
Kama nilivyosema wakati wa Kampeni, na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda
vilivyopo na kuhakikisha vinafanya kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa
viwanda vilivyokuwa vya umma kwa makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka
wafanye hivyo mapema. Na hapa nataka nisisitize wito wangu huo kwao.
Najua huko nyuma ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba
ya aina hiyo umekuwa ukilegalega na watu wamejifanyia mambo watakavyo.
Wapo walioacha kabisa uzalishaji na kufumua hata mitambo ya uzalishaji.
Mimi niliahidi, na nataka niseme hapa kwa wazi kabisa, kwamba wale waliobinafsishiwa
viwanda hivyo waanze kazi, waanze kazi mara moja. Wakishindwa basi tutavitwaa
viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na kuwapa watu
wengine wenye nia ya kuviendeleza. Hatuwezi kuwa na watu wanajiita wawekezaji
tunawapa viwanda vyetu halafu wanaviatamia tu. Mimi hilo sitalikubali
na wala sitalivumilia. Nimeielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanza
kushughulikia suala hili mara moja. Naomba Bunge lako lituunge mkono.
Mheshimiwa
Spika;
Njia ya pili ya kuendeleza viwanda ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo
mbalimbali ya nchi yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu ya kufanya hivyo
tayari ipo na baada ya muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo watu wanaotaka
kuwekeza Tanzania sasa, katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka ya
nyuma kidogo, lakini wakati mwingine sisi humu humu – tukiwemo sisi
viongozi kwa kushirikiana na wafanyabiashara matapeli na laghai –
tumehujumu mipango na shauku ya wawekezaji wa nanma hiyo. Pamoja na
shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea vikwazo na kuwapiga
vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi jirani. Sisi
katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa usumbufu
na urasimu wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji
wa ndani na wa nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji
wa Serikali watakaokwamisha jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda
hapa nchini hatutawavumilia.
Mheshimiwa
Spika;
Ni viwanda vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura ya kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile
ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani, hususan kweye
sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini – na maliasili nyingine.
Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa uzalishaji ndani
ya nchi uliofungamana na kushikamana. Viwanda vya aina hii vitahitaji
na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja, na
kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu
ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha bidhaa ambazo
zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) – yaani bidhaa
kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi
vitakuwa na uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje.
Viwanda hivi vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje.
Yote mawili yakitokea, yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na
nje, itatuongezea akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza
na kuendeleza mipango mingine kwa ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura
ya tatu ya viwanda tunavyovikusudia ni kuzalisha ajira nyingi. Shabaha
yetu ni kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda
ifikie asilimia 40 ya ajira zote
zitakazokuwepo nchini wakati huo.
Mheshimiwa
Spika;
Nimeamua kulisema hili kwa kirefu sana kwa sababu ili tufanikiwe
lazima tuelewane na tusaidiane kulisukuma kwa pamoja jambo hili.
Kilimo,
Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa
Spika;
Sekta nyingine ambazo lazima tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza
ni kilimo, mifugo na uvuvi. Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa
kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza
thamani mazao yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi
kikubwa ni nchi ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii inatokana na ukweli
kwamba sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia 75 wanaishi vijijini
na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Wakulima,
wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao
na wanazalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula
chote kinacholiwa hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25 kwenye pato
la taifa yaani GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu
ya fedha za kigeni. Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa
sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu na maisha yetu
ni mkubwa sana. Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wakulima,
wafugaji na wavuvi wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika maisha
yetu na uchumi wa nchi yetu. Nataka kuahidi kwao sitawaangusha.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi
wetu wakulima, wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni watu maskini. Mapato
yao yako chini na wanaishi maisha duni. Lengo letu ni kuuimarisha sekta
hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi lakini
pia ziweze kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadili
maisha yao. Tukiweza kuboresha sekta hizi vijana wengi zaidi watavutiwa
kujiunga nazo na hivyo kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira. Nataka
niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao
tutahakikisha zinatekelezwa. Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia
kwa dhati ahadi hizo ili kuhakikisha kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi
unakuwa wa kisasa zaidi na wenye tija. Baadhi ya mambo tuliyowaahidi
kuyatekeleza ni pamoja na haya yafuatayo:
- Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa ikiwa pamoja na ufugaji wa samaki,
- Kuwapatia pembejeo,
- Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,
- Kuwapatia wataalamu wa ugani,
- Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,
- Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana kufikia lengo hili,
- Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa, kule Kagera ina kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda ambako bei iko juu, tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili wakulima wapate bei nzuri. Tutafanya hivyo pia kwa mazao mengine kama mahindi, chai, pamba, korosho, mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki, n.k.),
- Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa wao kuondolewa kwenye ardhi zao kupisha wawekezaji,
- Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya migogoro hiyo tunaviondosha haraka,
- Kuhakikisha kwamba tatizo la wavuvi kuvamiwa na majambazi na uvuvi haramu linashughulikiwa kikamilifu.
Tatizo
la Umaskini na Ajira
Mheshimiwa
Spika;
Nimezungumzia umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ya matatizo
makubwa mawili yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo la UMASIKINI na pili ni tatizo
la AJIRA. Ni kweli uchumi
wetu umekuwa ukikua kwa kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana
na kasi ya kuondoa umasikini na uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana
wetu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 28.2 ya Watanzania
ni maskini. Na kwamba kwa namna na kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo
baina ya matajiri (walionacho) na maskini (wasionacho) linazidi kukua.
Tukiendelea hivi tunavyoendelea sasa hatutakuwa tunaitakia mema nchi
yetu kwa sababu mgawanyiko mkubwa wa kimapato na tofauti kubwa za kimaisha
baina ya matajiri na maskini ukiachiwa uendelee na kuzidi kukua utachochea
chuki na uhasama baina ya walionacho na wasionacho. Lazima tujizatiti
na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na kuibadilisha
hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa watu wetu.
Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni uendelezaji wa sekta ya viwanda
na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa
Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA. Kama nilivyokwisha
kugusia, ukuaji wa uchumi wetu haujaenda sambamba na kasi ya watu wanaoingia
kwenye soko la ajira kila mwaka. Tatizo la ajira ni kwa vijana wote
waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na ujuzi. Hii inamaana
kwamba sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu sizo zinazozalisha
ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka msisitizo kwenye sekta ya viwanda
hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo
ambavyo ndio mwajiri mkubwa hivi sasa.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na kuweka msisitizo katika Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi kuwawezesha
vijana wetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango
mbalimbali. Ili hili liwezekane, na sisi tutalifanya, linahitaji mambo
mawili makubwa.
Kwanza, kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi.
Hatuna budi kuweka mkazo katika viwango vya ubora vya elimu na stadi
za kazi wanazopata vijana wetu. Nalisema hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia
uendelezaji wa viwanda ikiwa hatujaandaa vijana wenye uwezo, ujuzi,
na stadi za kufanya kazi hizo kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu; hatuwezi
kutaka kuwekeza katika viwanda vya nguo au samani ikiwa hatuna wahandisi
wa mitambo wazuri, wabunifu wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa
na kukubalika. Aidha hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha
shughuli za uzalishaji kama hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi
na kuiendeleza. Kwa hivyo tutaelekeza nguvu zetu katika kuhakikisha
kuwa shule na vyuo vyetu katika ngazi mbalimbali vinafundisha na kutoa
vijana wenye viwango vya hali ya juu vya elimu, maarifa, ujuzi na ufundi.
Mheshimiwa
Spika;
Pili, ni suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka
kujiajiri. Katika kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua
na kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo:
- Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na fani walizosomea;
- Kuwawezesha vijana kuanzisha SACCOS zao na kupitia SACCOS hizo kuwawezesha kupata mikopo;
- Kuwawezesha vijana wajasiriamali kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na mafao mengine katika mifuko hiyo.
Mheshimiwa
Spika;
Tatu, ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali
zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha
shughuli za kina Mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha
Boda Boda na Maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi
mbalimbali halali za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha
yao, n.k. Shughuli za makundi haya zinatusaidia sana katika kupunguza
makundi ya vijana wetu ambao wangekaa tu na kuzurura zurura ovyo bila
shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo wetu wa kuwapatia ajira
tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwawezesha kufanya shughuli
zao kwa utilivu bila bugudha. Niliahidi, na nataka nirudie hapa, kwamba
Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri zetu, pamoja
na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na rafiki
kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa
lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao
na shughuli nilizozitaja tutauondoa. Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza
ukusanyaji mapato, na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao
huipotezea Serikali mabilioni ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana
na kina mama na vijana mitaani. Viongozi na watendaji wa Serikali na
hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya wafanyabishara wadogo
na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.
Afya
Mheshimiwa
Spika;
Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi
wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora
za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi
wanapata huduma bora za afya kwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:
- Kwanza, kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo. Lengo ni kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali ya Rufaa.
- Pili, tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika Nyanja za afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.
- Tatu, tutaongeza bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha, tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.
Elimu
Mheshimiwa
Spika;
Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi
wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya
Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja
na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi. Aidha, tutahakikisha
kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja
na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani
elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama
tulivyoahidi kwenye kampeni. Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi
zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati. Tutashughulikia
maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba
za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha
zaidi.
Maji
Mheshimiwa
Spika;
Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi
sana ya ukosefu wa maji. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo
ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo
ya mijini ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanzisha
miradi mipya mikubwa na midogo ya maji kutoka katika mito, maziwa na
vyanzo vingine vya uhakika vya maji ikiwa pamoja na kuvuna
maji ya mvua. Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua
umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na
salama.
Umeme
Mheshimiwa
Spika;
Suala la upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo
katika nchi yetu pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita.
Hatuwezi kuzungumzia suala la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi.
Serikali yangu itahakikisha kwamba umeme unapatikana wa kutosha na wa
uhakika. Tutakamilisha miradi ya umeme iliyopo na kujenga mingine mingi
mipya ili wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati ya umeme na viwanda
vingi zaidi vidogo vidogo, vya kati na vikubwa vianzishwe.
Madawa
ya Kulevya
Mheshimiwa
Spika;
Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa
letu na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike. Familia
nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya taifa imepotea. Tutaushughulikia
mtandao huo hususan wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa
ya kulevya bila ajizi.
Mheshimiwa
Spika;
Masuala mengine tutakayoyawekea mkazo katika utawala
wa Awamu ya Tano ambayo ninaamini yatasaidia katika kujenga uchumi wetu
ni pamoja na masuala ya Utalii, Mawasiliano, Madini, Ardhi na Makazi,
Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara, Ulinzi na Usalama, utunzaji
wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Ualbino, Wazee,
Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari, wafanyabiashara, wawekezaji,
wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa masuala haya umefafanuliwa
vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Tutayatekeleza ipasavyo.
Mapambano
Dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa
Spika;
Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa
kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Sikufanya hivyo kwa
sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura
zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa,
na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.
Mheshimiwa
Spika;
Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia
rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi
vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima
haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo
zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili
ya watu wetu.
Mheshimiwa
Spika;
Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kimejengwa katika
misingi ya kukataa rushwa na ufisadi. Ndio maana moja ya Imani kuu za
CCM ni ile isemayo: “Rushwa ni
adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa”
Kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na
kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na
ufisadi.
Mheshimiwa
Spika;
Mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kuifananisha rushwa na ufisadi ‘Kama Adui Mkubwa wa Watu’. Akiongea Bungeni Mei 1960, Mwalimu Nyerere
alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
“Rushwa [na ufisadi] havina budi
kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa
na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”
Mheshimiwa Spika;
Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi aliyeichukia
na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha
tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza rushwa na
ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri, wamechoka kabisa, wamechoka
sana, hawako tayari kuvumilia upuuzi wa serikali itayoonea haya rushwa
na kulea mafisadi.
Mheshimiwa
Spika;
Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi
yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi
bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na
mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu
lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba Waheshimiwa
Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati natumbua
majipu haya.
Mheshimiwa
Spika;
Ninafahamu ugumu wa vita niliyoamua kuipigana. Nasema
nafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha na rushwa
sio watu wadogo wadogo. Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi
na ustawi wa nchi yetu hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi
na utumishi ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu. Kwa
hivyo ili niweze kufanikiwa lazima nipate ushirikiano mkubwa toka kwa
Bunge lako tukufu na vyombo vingine vilivyopo na vyenye majukumu ya
kupambana na vitendo hivi.
Aidha, tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga
mkono. Sina mashaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa
na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya
dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kushugulikia tatizo hili nimeahidi kuunda
mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo
husika katika jambo hili havitanikwamisha.
Aidha, nataka niahidi mbele ya Bunge lako tukufu
kwamba, kiongozi yeyote wa kuteuliwa, ambaye mimi nitakuwa nimemteua
kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na ninayo mamlaka ya kumwajibisha,
pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya
rushwa na ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya mimi kuchukua hatua
hizo hatua na taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Mheshimiwa
Spika;
Ninachotaka kusema ni kuwa Serikali yangu itafuatilia
kwa karibu mienendo ya viongozi na watendaji wake ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha
na vitendo vya rushwa na ufisadi. Na tukishajiridhisha hatutasubiri,
tutachukua hatua. Ni imani yangu wengine pia katika ngazi mbalimbali
mtafanya hivyo. Kwa sababu bila kufanya hivyo rushwa na ufisadi vitazoeleka
na kuwa wimbo unaoburudisha badala ya kuudhi na kukera.
Muundo
wa Serikali na Utumishi
Mheshimiwa
Spika;
Nilipokuwa nazunguka na kuzungumza na wananchi wakati
wa Kampeni za Uchaguzi, niliahidi kuwa nitaunda serikali ndogo ya wachapa
kazi.
Aidha, niliahidi pia kuunda serikali ambayo itawatumikia
watu na hasa wananchi wa kawaida. Serikali nitakayounda, nataka iwe
inawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha.
Natoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu,
kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu watumishi
wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali nitakayoiongoza. Lugha za “hiyo ni
changamoto tutaishughulikia”, au “Mchakato
unaendeela” hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Mimi nataka watu wa Kazi Tu. Hatuwezi kulea
watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya,
au wamegeuza ofisi za umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na kuwataka watumishi wa Serikali kufanya
kazi hatuna budi kuyaangalia na kuboresha mishahara na maslahi yao na mazingira yao ya kufanyia kazi
kwa kuwapatia vitendea kazi bora na vya kisasa. Na jambo moja
tutakalolitekeleza ni kuangalia namna ya kupunguza kodi ya mapato katika
mishahara ya wafanyakazi yaani PAYE. Pia tutajitahidi
kuwatambua na kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.
Kuongeza
Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa
Spika;
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato
umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali ya Awamu
ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi
na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba
kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita
kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi
mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni
kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka
katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi
kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo
inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa
Spika;
Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo tutayasimamia
kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza, safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini
tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha
kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi
mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu
wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.
Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za
fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine
za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14
na 2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324
zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
- Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;
- Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;
- Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;
Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari
za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa,
Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.
Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma
za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara
za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za
walimu ngapi?, madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za
nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge
mkono.
Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo
nje ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.
Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha
ambayo kwa kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana
tija na wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera
na mipango ya Serikali.
Nne, tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya
Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana
na usimamizi hafifu tunaiziba. Ni matarajio yangu kutakapoleta Mswada
wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga
mkono.
Tano, tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na
maelekezo mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma
kuhusu ununuzi wa bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali.
Samani zote kwa ajili ya matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa
hapa hapa nchini.
Sita, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu
na kuthibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi
waandamizi wa Serikali; na
Saba, tutaendelea kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali
na Taasisi zake zote yasiyo na tija kwa uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa ajili hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia
kuiunda vitakuwa ni: kupunguza urasimu ili kuongeza
kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali; kubana matumizi kwa kupunguza
yale ambayo kutokana na hali yetu ya uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika; na kurejesha nidhamu ya
Serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Tutatekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja
na mambo mengine kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri; kuongeza usimamizi
katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali kwa kuziba
mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha kwamba wale wote
wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu ya matumizi
ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye miradi
ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji
wa viongozi na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio
wateja na waajiri wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano
itaendelea kubainisha maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo
yanaigharimu Serikali fedha nyingi na kuyadhibiti. Aidha, nitoe wito
kwa Watanzania wote kila mmoja wetu afanye kazi iwe shambani, ofisini,
kiwandani, sokoni, n.k. Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka
kwa Watanzania kutokupenda kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi
vijiweni, muda ambao ungetumika kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu
yangu ni HAPA KAZI TU!
Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa
Kikanda
na Kimataifa
Mheshimiwa
Spika;
Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja
ya diplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika awamu zilizotangulia
za uongozi. Serikali yangu itaendeleza sifa hiyo kwa kujenga juu ya
msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na awamu ya nne chini
ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa waumini
na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo
la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu. Tutaendelea kuwa
waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na daima
tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi wanachama.
Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano
wetu hatua kwa hatua.
Mheshimiwa
Spika;
Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuendelea kushirikiana
kwa karibu na nchi wanachama ambao tunauhusiano wa kihistoria na kidugu.
Tutaendelea kuamini katika Umoja wa Afrika (AU) na azma ya ndoto ya
waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika. Tutaendelea pia kushiriki
kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na kushirikiana
na nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu ya amani, usalama
na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.
Tutaendeleza na kustawisha mahusiano na marafiki
zetu wote Magharibi, Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati
kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi zetu na watu wetu. Tutapenda
kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri kisiasa kukuza mahusiano
yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi. Tutafanya hivyo pia
kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu na Umoja
wa Mataifa (UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia,
Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),
n.k.
Aidha, tutazitaka Balozi zetu zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya fedha
tunazowapelekea hususan katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na
mchango wao katika ukuzaji wa sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia
yetu na Sera yetu ya nje ikijibu changamoto zetu za ndani za ajira,
miundombinu, masoko ya mazao ya wakulima, viwanda n.k.
Hitimisho
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe wito kwa Waheshimiwa
Wabunge, Bunge hili linalo nafasi ya kuweka historia ya kuwa kitu kimoja
na kuweka masilahi ya Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha za
vijembe, mipasho, na ushabiki wa vyama bungeni. Kwanza, tukumbuke wote
bila kujali itikadi za vyama vyetu sisi ni kitu kimoja; na pili tumechaguliwa
kuwawakilisha wenzetu. Baada ya miaka mitano kila mmoja atarudi kwenye
jimbo lake kuomba kura na huko atapimwa kwa maendeleo aliyopeleka.
Tusimame pamoja, Tanzania ni yetu sote tutangulize
masilahi ya nchi mbele, na kwa mara ya kwanza Watanzania waone Bunge
tofauti na sio Bunge la kuzomea, kutoka nje, kutukanana, mipasho, n.k.
Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge hili
Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.
Aidha, napenda kusisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa.
Matarajio na matumaini ya Watanzania waliotuchagua na kutupa ridhaa
ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni makubwa. Wanachotaka
kuona ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo zitakazojibu matumaini
yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na mimi, baada ya miaka mitano
toka sasa, tutapimwa kwa namna tutakavyokuwa tumetekeleza mambo ambayo
tumewaahidi Watanzania wenzetu. Mimi nina amini kabisa kwa ushirikiano
wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu tutaweza kuzitimiza ndoto
za Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa
Spika;
Sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!
Mungu libariki
Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.

EmoticonEmoticon