Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecki Sadiki Akifungua mafunzo ya siku
mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi
wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo jijini Dar es salaam.
Waratibu wa
Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na
Maafisa uchaguzi waliohudhuria mafunzo leo jijini Dar es
salaam kujiandaa usimamizi wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
Oktoba 25 mwaka huu.
Waratibu wa
Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na
Maafisa uchaguzi waliohudhuria mafunzo leo jijini Dar es
salaam kujiandaa usimamizi wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
Oktoba 25 mwaka huu.
Picha/ Aron Msigwa- MAELEZO.
***************************************************************
Na.Aron Msigwa- MAELEZO, Dar es Salaam.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es slaam Said Mecki Sadiki amewataka Waratibu wa
Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya Siasa katika
mkoa huo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa ushirikiano ili
kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa amani na utulivu na kuepusha
manung'uniko yanayoweza kujitokeza.
Akifungua
mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi,
Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo jijini Dar es
salaam Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Dar es salaam ni miongoni mwa
maeneo yenye wapiga kura wengi hivyo mkoa kwa kushirikiana na Tume ya
uchaguzi umejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wote waliojiandikisha
wanapiga kura kwa amani na utulivu Siku ya uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu.
Amesema
Wakurugenzi wa Halmashauri wa mkoa huo ambao ndiyo wasimamizi wa
uchaguzi katika wilaya wanalo jukumu la kuwaita na kuwaelimisha viongozi
wa vyama vya siasa juu ya taratibu na kanuni za kufuata wakati wa
uchaguzi mkuu ili wajenge mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa
ushirikiano.
Aidha,
amewasisitiza wasimamizi hao kutojihusisha kwa namna yoyote ile na
kampeni za siasa wakati wa kutekeleza majukumu yao kwani kufanya hivyo
watakuwa wanahujumu ufanisi wa uchaguzi mkuu katika mkoa wa Dar es
salaam.
Ili
kudumisha amani na utulivu vituoni amewataka kufanya kazi zao kwa
umakini mkubwa kwa kuwa suala la amani vituoni litakuwa mikononi mwao
wakati wa kipindi chote cha upigaji wa kura Oktoba 25 mwaka huu.
"Simamieni
kanuni, sheria na taratibu, msionyeshe upendeleo wowote wala kufanya
kampeni za aina yoyote ile ndani ya vituo vya kupigia kura, jambo hilo
halikubaliki hata kidogo,mfanyeni kazi mliyotumwa ili msiwe sehemu ya
tatizo katika nchi hii" Amesisitiza Sadiki.
Ametoa
wito kwa wananchi kuendelea kutunza kadi zao za kupigia kura ili waweze
kuzitumia siku ya uchaguzi na kuvionya vikundi, watu au vyama
vinavyojaribu kuwarubuni wananchi kwa kununua kadi zao za kupigia kura
kuacha tabia hiyo.
"
Watu wanaofanya hivi wanafanya unyang'anyi, nawataka waache tabia hii
kwani haina tija kwa mamaendeleo ya taifa letu,ukichukua au kuiba kadi
ya mtu unamnyima haki ya kupiga kura muhusika na huo sio uungwana"
Amesisitiza.
Ametoa
wito wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kudumisha amani wakati wa
upigaji wa kura na kuwataka wananchi wote waliopanga kufanya vurugu
wakati wa uchaguzi kuacha
"Sisi
kama Serikali hatuvumilia aina yoyote ya uvunjifu wa amani,
tutaimarisha ulinzi yapo maeneo korofi ambayo yamekuwa na vitendo vya
uvunjifu wa amani tunayajua, tunawahakikishia wananchi watapiga kura kwa
amani na kurudi makwao wakiwa salama"
Kuhusu
waangalizi wa Kimataifa waliowasili nchini ambao baadhi yao watafanya
kazi jijini Dar es salam amesema watafanya kazi zao kwa mujibu wa
taratibu na kanuni walizopewa na Tume na kuongeza kuwa kazi yao itakua
ni kuangalia kama tumnazingatia na kufuata sheria tulizojiwekea na si
kuingilia shughuli za wasimamizi wa zoezi la upigaji wa kura.
"Suala
la kusimamia zoezi la upigaji wa kura ni letu wenyewe, msiwaruhusu
waanze kuwapa taratibu za upigaji wa kura wa nchi walizotoka wala kutoa
maamuzi yoyote, kazi yao itakua ni kuangalia mwenendo wa uchaguzi wetu
na si vinginevyo" amesisitiza.
Aidha,
amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawapeleka mawakala wao
mapema katika vituo vya kupigia kura kabla ya kuanza kwa zoezi la
upigaji wa kura ili kuondoa manung'uniko yanayoweza kujitokeza.
Kwa
upande wake Bi. Clesensia Mayala ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu, Kanda
ya Kusini Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema lengo la mafunzo hayo ni
kuwakumbusha wasimamizi na Maafisa uchaguzi kuzingatia na kufuata
taratibu zilizotolewa na Tume ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Amesema
katika mafunzo hayo washiriki hao watajadili masuala mbalimbali ikiwemo
wajibu na majukumu ya waratibu na wasimamizi wa uchaguzi,majukumu ya
makarani waongozaji wa vituo vya kupigia kura ,kuangalia fomu
zitakazotumika wakati wa upigaji kura,taratibu za upigaji kura, Fomu
zitakazotumika wakati wa kuhesabukura, kujumlisha na kutangaza matokeo
ya Urais,Wabunge na Madiwani.
Amefafanua
kuwa wasimamizi wote wa uchaguzi watakua na jukumu la kuhakikisha kuwa
vituo vyote ya uchaguzi vinafunguliwa kwa wakati na kufungwa kwa
kuzingatia muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanatimiza
wajibu wao wa kikatiba.
Kwa
upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Temeke Bw. Photidas Kagimbo
amesema uchaguzi mkuu katika eneo analolisimamia utafanyika kwa uhuru
na usalama na kuongeza kuwa wamejipanga vyema kuwahudumia wananchi wote
waliojiandikisha ambao watajitokeza kupiga kura siku hiyo.
Amesema
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kupeleka vifaa mbalimbali katika
maeneo mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kupiga kura Oktoba 25 na
kufafanua kuwa kazi inayoendelea sasa ni utoaji wa elimu ya mpiga kura
kwa wananchi.
Kuhusu
uhakiki wa taarifa za wananchi katika daftari la kudumu la Wapiga kura
kwa wananchi walioshindwa kuhakiki kutokana na sababu mbalimbali amesema
liko mikononi mwa Tume ya Taifa ya uchaguzi na kwamba wao wanasubiri
maelekezo ya Tume hiyo na daftari kamili litakalokuwa na orodha ya
wapiga kura wote litakalopelekwa kwenye vituo vya kupigia kura kabla ya
tarehe ya uchaguzi ili kutoa fursa kwa vyama vya siasa na wananchi
kupitia majina yote.