MGOMBEA
Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif
Sharif Hamad, ameahidi kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara
wakubwa na wadogo iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar katika
uchaguzi mkuu ujao.
Akiwahutubia
wafuasi wa Chama hicho katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja
vya Kwageji Bububu, Maalim Seif amesema atarekebisha mfumo wa ushuru
katika bandari ili kuepusha wafanyabiashara kulipa ushuru mara mbili
wanaposafirisha mizigo yao kuelekea bandari ya Dar es Salaam.
Amesema
hali hiyo imekuwa ikiwadhoofisha wafanyabiashara wa Zanzibar, jambo
amesema ataliwekea utaratibu mzuri, ili wafanyabiashara waweze kuendesha
shughuli zao bila ya usumbufu.
Akizungumzia
wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo wale wa Jua kali, Maalim Seif
amesema atawaekea mazingira mazuri kuweza kufanya shuguli zao.
Amesema
chini ya uongozi wake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar
atahakikisha kuwa wafanyabiashara hao hawanyanyaswi, na watawekewa
maeneo maalum ya kufanya biashara zao, na kwamba hakutokuwa na ulipaji
wa kodi zisizotambulika katika maeneo yao.
Aidha ameahidi kuanzisha benki ya uwekezaji, ili kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo wadogo.
Nae
afisa uchaguzi wa CUF Bw. Muhene Said Rashid, amewataka wanachama hao
kuweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia wasioweza kupiga kura wakiwemo
wagonjwa, wazee na wenye ulemavu, ili kila aliyejiandikisha aweze
kupiga kura kwa mgombea anayemtaka.
Aidha amewataka kuelimishana juu ya namna ya upigaji kura, ili kuepuka uharibifu wa kura na kupiga kura kwa usahihi.
Mgombea
Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif
Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa Chama hicho katika viwanja vya
Kwageji Bububu.
Wafuasi wa CUF wakisikiliza na kushangilia hotuba ya mgombea Urais wa Chama hicho katika viwanja vya Kwageji Bububu.
Imail
Jussa Ladhu, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Timu ya Ushindi CUF,
akihutubia kwenye mkutano huo. (Picha na Salmin Said, OMKR)
EmoticonEmoticon