AWADH MASSAWE ATEULIWA KUWA MKURUGENZI MKUU WA TPA

October 18, 2015
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Rais Dkt. Jakaya Kikwete amemteua Bw. Awadh Massawe (pichani kushoto)kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Rais alitangaza uamuzi huo Ijumaa iliyopita wakati wa tukio la kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo inayosemekana kuwa kubwa katika ukanda huu wa Afrika mara itakapomalizika.

Akihutubia wakati wa tukio hilo, Dkt. Kikwete alisema yeye alishamaliza uteuzi huo na kumwambia Bw. Massawe afuatilie tu barua yake rasmi ya uteuzi.

“Mimi nilishalimaliza hilo, fuatilia tu barua yako ya ajira,” alisema Rais huku akishangiliwa na umati.

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Massawe amekuwa akifanya kazi kama Kaimu katika nafasi hiyo tangu mwezi wa Pili mwaka huu na kufanikiwa hadi sasa kufanya mageuzi makubwa katika kuleta ufanisi katika bandari hapa nchini. 

Pia kabla ya kukaimu nafasi hiyo, alikuwa Meneja Bandari ya Dar es Salaa.

Baada ya kuwa Kaimu Mkurugenzi, alianzisha mikutano ya wadau yenye lengo la kurudisha mahusiano yaliyokuwa yameyumba kati ya pande hizo mbili.

Mikutano hiyo inayofanyika kila Alhamis ya mwisho ya kila mwezi inalenga kuhusisha wadau mbalimbali katika majadiliano ya jinsi ya  kuboresha ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam.

Pia mwisho wa mwezi wa Sita mwaka huu, TPA ilifungua ofisi ndogo katika mji wa Lusaka, Zambia.

Mafanikio mengine ya hivi karibuni ni kuanza kwa mfumo mpya wa malipo kwa njia ya mtandao katika bandari ya Dar es Salaam.

Inatarajiwa kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi huo wa bandari ya Bagamoyo unaotarajiwa kugharimu dola bilioni 10, kutaongeza uwezo wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zinazohudumia tani milioni 12 za mizigo kwa mwaka, makasha 6,000 na kuajiri watu 3,200 na vibarua 1,500.

Bandari hiyo mpya inatarajiwa kuhudumia tani 600,000 za mizigo na makasha 1,000 kwa mwaka na kuajiri watu 1,000.

Awamu ya kwanza ya mradi huo itahusisha gati nne ambapo mbili kati ya hizo zitatumika kwa huduma ya makasha pekee, moja kwa ajili ya mizigo mingine.

Tayari TPA iko katika hatua za mwisho kabisa kulipa fidia kwa wanavijiji zaidi ya 2,000 walioachia ardhi yao kupisha mradi huo.

Mradi huo utatekelezwa kwa makubaliano ya pande tatu za serikali ya Tanzania, China Merchants Holdings International (CMHI) ya China na State Government Reserve Fund (SGRF) ya Oman.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »