Na Lorietha Laurence-Maelezo
………………………………………….
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa
kumiliki kiwanda cha kutengeneze magurudumu ya magari cha General Tyre
kwa asilimia 100 baada ya kununua hisa 26zenye thamani ya Dola Moja
milioni kutoka kwa kampuni ya Continental AG.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Msajili wa
Hazina wakati wa makabidhiano ya nyaraka za ununuzi wa hisa hizo Katibu
Mkuu Kiongozi ,Balozi.Ombeni Semfue anasema jitihada za kuhakikisha kuwa
serikali inamiliki hisa hizo zilianza tangu mwaka 2012 kwa kufanya
mazungumzo ya awali na mwekezaji.
“Kufuatia hatua hii ya kuweza kumiliki hisa kwa asilimia 100
sasa tutakuwa na fursa ya kuzalisha magurudumu yetu wenyewe na hivyo
kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumia kununua magurudumu
kutoka nje” alisema Balozi.Semfue.
Aidha anaendelea kufafanua kuwa hatua itakayofuata ni kutamfuata
mwekezaji atakayeshirikiana na Shirika la Maendelao la Taifa (NDC)
katika kuzalisha magurudumu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Balozi.Semfue anampongeza Rais Mhe. Jakaya Kikwete kwa
kufanikisha zoezi zima la kuhakikisha serikali inamiliki hisa za kiwanda
cha General Tyre kwa asilimia 100 na hivyo kufufua uchumi wa jiji la
Arusha na Taifa kwa ujumla.
Naye Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru anasema mpaka serikali
kuweza kumiliki hisa hizo ni hatua kubwa sana kutokana na vikwazo
mbalimbali vilivyokuwa vikiwekwa na mwekezaji wa kiwanda hicho
kilichoanzishwa mwaka 1969.
“Haikuwa kazi rahisi kumiliki hisa hizi bila ya jitihada kubwa
iliyofanywa na serikali katika kumshawishi mwekezaji baada ya kuona hana
kuwa hakuwa tayari kuwekeza na hivyo kurejesha umiliki kwetu” alisema
Mafuru.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe.
Uledi Musa, anaeleza kuwa kiwanda hicho kitatoa fursa za ajira zaidi
kitakapoanza kuzalisha tofauti na awali ambapo kiliweza kuajiri
wafanyakazi 360.