Na Joachim Mushi,
WANAHARAKATI Ngazi ya Jamii nchini
wametoa madai kuelekea Uchaguzi Mkuu huku wakiiomba Serikali iharakishe
mchakato wa uandikishaji daftari la kudumu la wapiga kura ili vijana
wengi wanaostahili waweze kuitumia haki yao ya msingi ya kushiriki
mchakato wa uchaguzi na ule wa kura ya maoni.
Madai hayo yametolewa katika tamko
lao lililotolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) kwenye
warsha ya majadiliano kati ya waandishi wa habari, wachora katuni na
waandishi wa habari za mitandao ya jamii iliyofanyika jijini Dar es
Salaam.
Katika madai hayo wanaharakati
ngazi ya jamii pia wameomba elimu ya uraia na ya mpiga kura itolewe kwa
wingi ili iwafikie vijana wapate hamasa ya kujitokeza kugombea na kupiga
kura, ikiwa ni pamoja na kuvitaka vyama vya siasa kuweka mfumo wa
uwiano kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kupata nafasi
sawa kama wagombea kwenye uchaguzi bila upendeleo wala woga.
Aidha imetaka vijana wanaojitokeza
kama wagombea wawekewe mazingira rafiki ikiwezekana wapewe ruzuku ya
kuwasaidia kushindana kwenye uwanja wa demokrasia, pamoja na kushauri
Sera ya Taifa ya Vijana pamoja na Mkataba wa Vijana wa Afrika
unalitambua kundi la vijana kama rasilimali mojawapo muhimu sana kwenye
maendeleo na pia katika kulinda amani na utulivu kwenye Bara la Afrika.
“…Hata hivyo pamoja na kwamba
vijana ni zaidi ya 60% bado mchango na thamani ya vijana haujatumika
ipasavyo kwenye demokrasia ya Tanzania, huku thamani yao ikionekana tu
nyakati za uchaguzi kwa kutumiwa kama walinzi au wapambe wa wagombea,”
imeeleza sehemu ya tamko hilo.
Limebainisha kuwa pamoja na
uanzishwaji wa Mabaraza ya Vijana kwa vyama vingi, mengi hayana nguvu ya
maamuzi kwa kuingiliwa na vyombo vya juu vya Chama, ikiwa ni pamoja na
kukumbusha kuwa mwaka 2010 ulikuwa ni mwaka ambao vijana wengi waliingia
Bungeni na wamekuwa chachu kubwa ya kuchangia na kuibua mijadala yenye
tija Bungeni.
Hata hivyo imeeleza kuwa bado
idadi ya vijana wanaojitokeza kupiga kura hasa wasichana bado ni ndogo
ukilinganisha na ile ya wanaojiandikisha na wanaoshiriki kwenye kampeni,
vijana wengi wanaojitokeza kwa kuweka nia ya kugombea wamekumbana na
kigingi cha uteuzi kwa kutokubalika ndani ya vyama kwa mawazo mgando
kwamba umri wao hauwawezeshi kufanya uchambuzi wa masuala makubwa ya
kitaifa, kadhalika changamoto ya nguvu yao ndogo kiuchumi ajira ambayo
inawafanya wasiweze kushindana kikamilifu katika uwanja usio na usawa wa
siasa.
Kwa upande wa vyama vya siasa
tamko hilo limetaka watu wenye ulemavu waingizwe kwenye sera na mipango
ya nchi kwa vitendo kwani bado ushiriki wao kwenye masuala ya uchaguzi
na uongozi uko chini.
Madai mengine ni pamoja na Vyama
vya siasa kuweka mfumo wa uwiano kuhakikisha zinazingatia ushiriki wa
watu wenye ulemavu kwenye uchaguzi kama wagombea na wapiga kura,
Serikali kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu ili washiriki
kikamilifu kwenye michakato yote ya maendeleo, hii ni pamoja na
uchapishaji wa sheria na kanuni kwa lugha rahisi ikiwemo maandishi ya
nukta nundu, vituo rafiki vya kampeni na kupiga kura kwa watu wenye
ulemavu.
Mengine ni pamoja na watu wenye
ulemavu wa ngozi, kudai ulinzi na usalama wa maisha yao, kama raia wa
taifa hili, uwepo wa mikakati ya kuelimisha umma uondokane na mawazo
potofu yanayoashiria kutishia uhai na usalama wa kundi hili na hasa
wenye ulemavu wa ngozi. Hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wote
watakaohusika.
“…Serikali ihakikishe upatikanaji
wa taarifa na maarifa kwa njia rahisi ikiwemo lugha ya alama na
maandishi ya nukta nundu kutoa elimu ya mpiga kura na pia vyombo vya
habari kama vile TV ziweke wakalimani hasa katika vipindi vya taarifa ya
habari na vipindi vyote vyenye mijadala ya kitaifa. Mgombea tutakayempa
kura ni Yule ambaye miongoni mwa sera zake itakua ni kupinga ukatili wa
kijinsia kwa hali zote bila woga wala upendeleo
Aidha mengine ni pamoja na
Serikali itakayoingia madarakani kuhakikisha inaunda Tume ya Kughulikia
Ukatiki wa Kijinsia kama zilivyo Tume nyingine, kuunda mahakama maalum
ya kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia ngazi ya familia na kuweka
mikakati halisi ya kuhakikisha kwamba kila mwanamke ana haki ya uchumi
na haki ya maisha endelevu/ajira akiwa kijijini au mjini, mwenye
ulemavu, mzee au kijana, wanawake na wanaume wote wapate kipato
kinachotosheleza kuishi maisha bora kama binadamu.
Warsha hiyo ya siku moja
iliyoandaliwa na TGNP Mtandao kwa ushirikiano na Mfuko wa Wanawake
Tanzania (TWF) imejumuisha makundi mbalimbali ya wanahabari ikiwa ni
lengo la kuwajengea uwezo kuandika masuala ya kijinsia kwa kina.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
EmoticonEmoticon