AFYA YA GWAJIMA UTATA

April 04, 2015

gwajima2
KUDHOOFU kwa afya ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye wiki moja iliyopita alizimia wakati akihojiwa na Polisi, kumezua utata.
Wakati baadhi wakijenga hisia kwamba hatua hiyo huenda ikawa ina mkono wa Mungu, au imetokana na kuvurugika kwa mfumo wa kawaida wa ufahamu, hata hivyo maofisa wa Jeshi la Polisi wa Kituo Kikuu Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliofika kumuhoji Gwajima ambaye aliwasili kituoni hapo akiwa mzima wa afya, wamenyooshewa kidole.

Daktari anayemtibu Askofu Gwajima, Photunatus Mazigo, akizungumza na MTANZANIA Jumamosi licha ya kusema maadili hayamruhusu kutaja ugonjwa wake, hata hivyo alieleza kuwa askofu huyo ana maumivu makali katika mguu na mkono wa upande wa kushoto.
“Askofu Gwajima ana maumivu makali katika mguu na mkono wake wa kushoto pamoja na mgongoni, sisemi kuwa huo ndio ugonjwa wake ila inawezekana ikawa hivyo.
“Maumivu hayo huenda ndiyo yalisababisha kushindwa kupanda ngazi aliporudi Polisi kuhojiwa na tulivyomruhusu sio kwamba alikuwa amepona kwa asilimia mia moja, ndio maana tulimpatia kiti (wheel chair) kwa ajili ya kumsaidia,” alisema Dk. Mazigo.
Ingawa Daktari wake huyo hasemi maumivu hayo yametokana na nini, kauli yake hiyo imejenga hisia kwa baadhi kwamba kile kilichotendeka polisi ndio msingi wa maumivu yake hayo.
Kwa mujibu wa Daktari wa Gwajima, pamoja na kwamba walimruhusu Askofu huyo, lakini walimshauri kupumzika wiki moja kutokana na kwamba alikuwa hajapona kikamilifu bali alikuwa ana nafuu tu.
“Tulipomruhusu kurudi nyumbani tulimwambia baada ya wiki moja arudi kuripoti hospitali kwa ajili ya kuchunguza afya yake,” alisema Dk. Mazigo.
Alisema ugonjwa wake sio kwamba ni siri au haujulikani, lakini matatizo aliyoyapata yalimwathiri na kusababisha kukosa nguvu katika mguu na mkono wake wa kushoto.
“Siwezi kusema kuwa ugonjwa wake ni nini kwa sababu maadili hayaruhusu, lakini siku akiniruhusu nieleze nitasema, hata yeye mwenyewe anajua ugonjwa wake mnaweza kumuuliza.
Zaidi, Dk. Mazigo alisema, Gwajima alipofika katika Hospitali ya TMJ alikuwa katika hali mbaya, hivyo kulazimika kumpeleka katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).
Katika chumba hicho alikaa kwa muda wa siku tatu na baada ya kuona kuwa hali yake imebadilika walimhamishia katika wodi ya kawaida.
“Tulimhamisha kutokana na kwamba tuliona hali yake inaendelea kuimarika na baada ya kumfanyia mazoezi tuliona kuwa akipata msaada anaweza kusimama mwenyewe ndio maana tukampatia kiti hicho,” alisema.
Daktari mwingine aliyezungumza na gazeti hili ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema hawezi kusema moja kwa moja kama maumivu hayo ni dalili za ugonjwa fulani na kwamba jambo hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi na uchunguzi wa kitaalamu.
“Wengi wamekuwa wakihusisha dalili hizo na ugonjwa wa kiharusi, lakini siwezi kusema moja kwa moja mpaka kuwe na majibu ya uchunguzi wa kitaalamu,” alisema daktari huyo.
Hata hivyo, alisema watu wenye historia nzuri kwa maana wasio na magonjwa kama shinikizo la damu huwa si rahisi kupata ugonjwa wa kiharusi.
“Kwa hiyo siwezi kusema moja kwa moja, hapa cha muhimu Gwajima mwenyewe awe wazi, lakini pia uzoefu unaonyesha wazi kwamba intelijensia ya polisi mara nyingi kama si wakati wote huwa inakuwa ni ya kutumia nguvu,” alisema Daktari huyo.
Wakati Daktari huyo akisema hayo, Msemaji wa Dk. Gwajima, Mchungaji Yekonia Behanaze, alikaririwa na MTANZANIA Jumapili wiki iliyopita akisema kuwa, askofu huyo hajawahi kuwa na shinikizo la damu.
Awali, mwanasheria wa Gwajima, John Mallya, alisema hali ya mteja wake ilikuwa nzuri lakini hawezi kuzungumzia ugonjwa unaomsumbua.
“Mimi nimezungumza naye asubuhi alikuwa akiendelea vizuri lakini siwezi kuzungumzia ugonjwa wake ni vyema mkamtafuta daktari wake,”alisema Mallya.
Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu kutoka Hospitali Teule wilayani Muheza Mkoa wa Tanga, Aubrey Maonga, alisema hali iliyomkuta Gwajima inaweza kusababishwa na mshtuko wa neva za fahamu au moyo kushindwa kupokea damu inayorudi kutoka mwilini.
“Inategemea alikuwa katika mazingira ya aina gani, lakini hali ile inaweza kusababishwa na mshtuko wa neva za fahamu (neurogenic shock) kama alisikia jambo ambalo hakulitegemea. Hatujui walikuwa wakizungumza nini hadi ashtuke vile.
“Inawezekana pia ni tatizo la damu kutoka sehemu ya chini ya mwili inayotakiwa kurudi kwenye moyo kushindwa kurudi, kwa hali hiyo mtu anaweza kuzimia. Hali hiyo huwakuta watu wanaosimama kwa muda mrefu hasa wanajeshi. Lakini kwa kuwa alikuwa anahojiwa, inawezekana ni mshtuko wa neva za fahamu,” alisema Dk. Aubrey.
Askofu Gwajima aliitwa kwa mara ya kwanza na jeshi hilo Machi 27, baada ya kutoa kauli ya kumkashifu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, kuhusu waraka wa Jukwaa la Wakristo.
Hata hivyo, wakati akihojiwa katika mahojiano hayo yaliyodumu kwa takribani saa saba, alizimia na hivyo kupelekwa katika Hospitali ya Polisi Kurasini na baadaye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya kuhamishiwa Hospitali wa TMJ ambako alitibiwa na kuruhusiwa baada ya siku tatu.
Jeshi la Polisi lilimwita tena kwenye mahojiano Aprili 2 na alipofika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda ya Dar es Salaam, hali yake iliendelea kuwa mbaya kiasi cha kushindwa kupanda ngazi za kuingia kituoni hapo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, juzi alisema hawakuweza kumhoji Askofu Gwajima ili kumpa fursa afya yake iimarike zaidi.
Kova alisema, Askofu Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi akisindikizwa na wasaidizi wake ikiwa ni pamoja na wakili wake saa mbili asubuhi.
“Alifika kituoni akiwa bado anatumia kiti cha magurudumu matatu (wheel chair) na alikubaliana na wapelelezi kwamba akaendelee na matibabu.
“Gwajima anatakiwa kurudi kuripoti Aprili 9 mwaka huu ili aweze kuendelea na mahojiano kuhusu tuhuma za kumkashifu na kumtukana Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,” alisema Kova.
Gwajima atoa madai mazito
Akizungumza na waumini wake siku moja kabla ya kurudi Polisi, Gwajima ambaye kwa maelezo yake mwenyewe aliwahi kuugua kiasi cha kushindwa kutembea kwa miaka sita kabla ya kuokoka, alidai kuna mtu anayemhujumu na kwamba hatafanikiwa.
Alisema, Mungu aliyemwezesha kutembea ndiye atakayemponya tena.
“Najua kinachoendelea. Namwombea mtu mmoja ambaye yuko hapa, nasema nakufahamu vizuri, nakujua vizuri na ninasema hutafanikiwa kwa jina la Yesu,” alisema huku waumini wakijibu ‘ameeen’.
“Nakwambia hutafanikiwa. Usifurahi leo kuniona nimekaa kwenye kiti hiki, bado nina maumivu, bado sina nguvu lakini nimesema lazima leo niende nyumbani mwa Bwana. Wewe ni mtoto mdogo, hujatoka mbali,” aliongeza Gwajima.
“Huyo aliyenifanya nitembee, hawezi kuniacha nikae kwenye kiti hiki tena. Unatakiwa ujue unashindana na mtu aliyewahi kuwa hatembei, lakini Mungu akamtoa kwenye kiti kama hiki. Ole wako wewe unayelazimisha kumrudisha mtu wangu pale, nakwambia sitakaa pale unapofikiri nikae,” alisema.
Aliwataka waumini wake kumsindikiza kituo cha polisi siku aliyohitajiwa kuripoti.
“Kwa hiyo nawaomba watu wote bila kuacha hata mmoja kwa wingi wenu, twende kwa pamoja kule polisi makao makuu, ili muweze kuona kwa ukaribu sana. Lipo jambo nililoliona na nimelisikia linaendelea lakini hawatashinda, asema Bwana wa majeshi, amen,” alisisitiza Gwajima huku akishangiliwa na waumini wake.
Hata hivyo, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kufafanua kuhusu kauli yake hiyo, simu yake iliita bila kupokelewa kwa muda mrefu. Juhudi za gazeti hili kumtafuta Gwajima bado zinaendelea.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »