MSIWARUHUSU WATOTO KWENDA KWENYE FUKWE ZA BAHARI BILA WAANGALIZI”

April 04, 2015
TANGA.
 JESHI la Polisi Mkoani Tanga limetoa tahadhari kwa wazazi na walezi mkoani hapa kutowaruhusu watoto wao bila kuwepo uangalizi kwenda kwenya fukwe za bahari nyakati za sikukuu ya Pasaka kwani wanaweza kuogelea na kupoteza maisha.

Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Juma Ndaki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuelekea sikuuu hiyo ambapo alisema kuwa katika jambo hilo wazazi wanapaswa kuwa makini sana kwani furaha inaweza kugeuka kilio.

Alisema kuwa licha ya hivyo wamiliki wa kumbi mbalimbali za stahere mkoani hapa kuacha kujaza watoto wengi mahali ambapo hakuna hewa kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea matatizo kwao.

Aidha alisema kuelekea siku hiyo Jeshi hilo limejipanga vilivyo kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali mkoani hapa pamoja na kuwataka wananchi kutoa taarifa watakapobaini kuwepo viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.

  “Jeshi letu limejipanga na kujithatiti vilivyo kuhakikisha wananchi katika maeneo mbalimbali wanasheherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu kwa kuimarisha ulinzi “Alisema Kaimu Kamanda Ndaki.

Hata hivyo aliwataka wananchi kutoa taarifa za uhalifu endapo zitakuwa zikijitokeza kwenye maeneo yao ili kuweza kuyapatia ufumbuzi haraka pamoja na kuwa waangalifu wanapotoka kwenye nyumba zao kwenda kwenye ibada za usiku.

Alisema wananchi watakaokwenda kwenye ibada za usiku wahakikishe wanakuwepo waangalizi kwenye nyumba zao ili kuendelea kuangalia hali ya usalama mpaka watakaporudi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »