WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema amevutiwa sana na kazi iliyofanywa katika
muda mfupi kwenye shamba la kahawa la Aviv lililoko kwenye kijiji cha
Lipokela, wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, eneo kubwa
la shamba limepandwa miche ya kahawa na mingine imezaa na imeshavunwa
ikilinganishwa na wakati alipofika shambani hapo Julai 2013 na
kutembelea tu kitalu cha miche ya zao hilo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Februari 2, 2015) wakati
akizungumza na wafanyakazi na menejimenti ya shamba la Aviv baada ya
kulitembelea na kukagua miundombuinu ya umwagiliaji wa matone ya maji
kwenye shamba hilo.
“Mkuu wa shamba hili, Bw. Medu amenieleza kwamba mpaka sasa,
wameshavuna kahawa mara moja na wanatarajia kuvuna tena hivi karibuni;
lakini ili waweze kuanza kupata faida ni lazima wavune mara nne.”
“Kilimo kinataka uvumilivu na kinataka uwekezaji mkubwa… ni
lazima kiwepo; hata kwa wakulima wadogo ni lazima kiwepo licha ya ugumu
wake. Sasa ukisema kilimo ni kigumu na ukaacha kulima wakati una mke na
watoto, je hao watakula wapi?”, alihoji.
Aliwasifu wamiliki wa shamba hilo kwa kuchagua kulima zao la
kahawa kwani lina walaji kila mahali ulimwenguni kote. “Wameamua kulima
kahawa aina ya Arabica ambayo inakubalika duniani. Uhitaji wa kahawa hii
upo kila mahali kwa sababu wanywaji wapo,” alisema.
Waziri Mkuu alisema pamoja na mafanikio hayo, shamba la Aviv
linakabiliwa na changamoto ya nishati kwani linahitaji megawati 2.5 ili
liweze kuendesha mitambo yake ambayo kwa sasa inatumia mafuta
yanayoligharimu fedha nyingi.
Aliwataka wamiliki wa shamba hilo waendelee kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Mapema, akisoma risala ya kampuni ya Aviv, Mkuu wa shamba hilo
ambaye pia anasimamia uzalishaji wa zao la kahawa Afrika Mashariki, Bw.
Medu Medappa alisema hadi sasa wamekwishalima hekta 1,060 na zote
zimekwishawekewa miundombinu ya umwagiliaji wa matone na kati ya hizo,
hekta 810 zimekwishapandwa miche ya kahawa.
“Shamba letu lina ukubwa wa hekta 2,000 na hadi sasa tumeshalima
hekta 1,060 na zilizobakia ni kwa ajili ya kutunza mazingira na uoto wa
asili kwenye vilima vinavyotuzunguka,” alisema.
Alisema hadi sasa wamekwishaajiri wafanyakazi 1,500 kwenye
shamba hilo na kutoa mafunzo kwa wakulima wanaoishi vijiji vya jirani.
“Pia tumewapatia miche ya bure kaya 673 na kutokana na mafunzo
tunayowapa, wanavijiji wameweza kulima kahawa inayoendana na viwango vya
kimataifa vya uzalishaji kahawa ambavyo ni miezi 22,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu akijibu moja ya
hoja kwenye risala ya Bw. Medappa iliyohusu eneo la hekta tisa
kuchukuliwa na Wakala wa Ujenzi wa Barabara (TANROADS), alisema eneo
hilo ni muhimu kwa ujenzi wa barabara za mkoa huo kama ambavyo shamba
hilo ni muhimu kwa mkoa huo.
“Lile eneo limetengwa na TANROADS kwa ajili ya kutengeneza
kokoto za ujenzi wa barabara. Barabara za lami tunazitaka. Tunahitaji
kazi hii iendelee la sivyo barabara zetu zitakufa,” alisema.
Alisema watu wa TANROADS wakimaliza kazi yao, lile eneo litabaki
tupu na mwekezaji huyo anaweza kulitumia kadri atakavyoona inafaa kwa
sababu liko ndani ya eneo lake.
……………………………..
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
FEBRUARI 3, 2015.