TIMU ya soka ya mkoa wa Simiyu imeanza vibaya
mashindano ya Copa-Coca-Cola ngazi ya taifa baada ya kupokea kipigo cha mabao
3-1 kutoka kwa vijana wa Mkoa wa Kigoma kwenye mchezo wa ufunguzi uliochezwa
katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana.
Kigoma walipata bao la kwanza mapema kwenye dakika
ya nane kupitia kwa Juma Swalehe, huku Juma Zuberi akiongeza bao la pili dakika
ya 30 na Idrisa Akilimali alihitimisha karamu ya mabao kwa Kigoma kwa kufunga
bao safi mnamo dakika ya 57, bao la kufutia machozi la Simiyu lilifungwa na
Kaluona Abdallah katika dakika ya 88 ya mchezo huo.
Michuano hiyo ilizinduliwa na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Fenella Mukangara ambaye aliwashauri makocha
wa timu kutumia michuano ya Copa-Coca-Cola kama changamoto ya kuibua vipaji
vipya katika timu zao kwa wasichana na wavulana.
Mukangara aliwaasa vijana kuhakikisha wanajituma
kulitangaza taifa la Tanzania katika michuano mabalimabli ya kimataifa. “Nina furaha sana kuona wasichana
pia wakijumuishwa katika michuano hii ya Copa-Coca-Cola na pia natoa shukrani
zangu za dhati kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa kuhakikisha
kuwa soka la wanawake linakuwa hapa nchini”, Mukangara alisema.
Mukangara pia aliwasisitiza washiriki wote wa
michuano hiyo kuhakikisha kuwa wanazingatia nidhamu ya mchezo uwanjani. “Tuna
imani kuwa washiriki wote mtazingatia sheria za mchezo huu kama inavyagizwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA)”, Aliongeza Mukangara.
Naye Meneja wa Coca-Cola nchini Yebeltal Getachew alielezea nia yao ya dhati
katika kuendeleza michuano hiyo ya Copa-Coa-Cola nchini. Wachezaji wanaofanya
vizuri katika michuano hii hupelekwa nchini Afrika Kusini kwa mafunzo zaidi.
Copa-Coca-Cola ni michuano pekee ambayo huanzia
ngazi ya chini kabisa na baadaye ngazi ya Taifa ikishirikisha mikoa yote ya
Tanzania bara pamoja na Zanzibar.
Kwa upande wake Rais wa TFF Jamal Malinzi aliwaonya
viongozi wa timu zote zinazodanganya umri na kusisitiza kuwachukulia hatua za
kinidhamu. “Katika kuonesha umakini katika michuano hii tumewaondoa wachezaji
87 kutoka katika mikoa ya Mbeya na Lindi kutokana na kudanganya umri”, Malinzi
alisisitiza.
Michuano ya Copa-Coca-Cola itafikia tamati mnamo
Desemba 20, mwaka huu, katika Uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es salaam.
EmoticonEmoticon