Miss Tanzania 2014 asaidia kituo cha New Life Orphans Home,Boko jijini Dar

December 31, 2014

Miss Tanzania Lilian Kamazima (kulia) akimkabidhi zawadi ya mwaka mpya Msimamizi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha New Life kilichopo Boko, Mwanaisha Magambo kwa ajili ya watoto 102 waliopo kituoni hapo, tukio hilo lilifanyika juzi.
Miss Tanzania Lilian Kamazima (kulia) akiwa na Miss Kinondoni Maria Shila wakiwa wamembeba mtoto aliekuwa kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha New Life cha Boko, mtoto huyo alifikishwa hapo akiwa na siku nne tu tangia kuzaliwa kwake.
Sehemu ya Watoto wanaolelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha New Life kilichopo Boko,wakimsikiliza Miss Tanzania Lilian Kamazima.
Miss Tanzania Lilian Kamazima (kulia) akiwa na watoto katika kituo cha New Life cha Boko.

Redds Miss Tanzania 2014 Lilian Deus Kamazima jumapili iliyopita alitoa misaada ya vyakula vya aina mbalimbali kwa kituo cha New Life Orphans Home kilichopo eneo la Boko nje kidogo ya jiji la D’salaam. 

Kituo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 2005 awali kilikuwa maeneo ya magomeni makuti kilianza na watoto yatima 17 na baadae kuongezeka hadi kufikia 70. Na kulazimika kuhama eneo hilo na kuhamia kigogo ambapo waliishi eneo hilo hadi hivi karibuni walipopata mfadhili mmoja kutoka nchini Qatar ambaye amewajengea jumba moja kubwa na la kisasa eneo la Boko Dawasa, alisema bi Mwanaidi Magambo ambaye ni Mlezi wa Kituo hicho. 

Kituo hicho kina watoto wapatao 105 ambapo  60 kati yao ni wasichana na 45 wavulana. Kituo hicho kinalea watoto wadogo kabisa wa umri wa mwezi mmoja hadi miaka 18. Hivi karibuni tulimpokea mtoto mwenye umri wa siku 5 kutoka hospitali ya wilaya ya Temeke ambaye mama yake alifariki mara tu baada ya kujifungua, alisema bi. Magambo. 

Kituo hicho kwa sasa kina matatizo ya vyakula, vitanda, magodoro, madaftari pamoja na sare za shule kwa ajili ya watoto hao yatima. Bi Magambo alimshukuru sana Mfadhili huyo kutoka nchi ya Qatar kwa kuwajengea jengo hilo, lakini alisema kwa sasa watahitaji mfadhili wa kuwalipia bili za umeme na maji pamoja na mahitaji mengine kituoni hapo. 

Kituo hicho kina bahati ya kutembelea na warembo wa Miss Tanzania ambapo mwaka 2007,  Miss Tanzania 2000 Jacqueline Ntuyabariwe alitembelea kituo hicho wakati bado wapo eneo la Magomeni Makuti na kuwapatia misaada mbalimbali. 

Miss Tanzania 2014 Lilian Kamazima alikabidhi vyakula vya aina mbalimbali ikiwemo mchele, unga wa ngano, sembe, sukari, maharage, mafuta ya kupikia, sabuni, soda, juisi, maji ya kunywa, na biskut vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni mbili. 

Miss Tanzania 2014 Lilian aliishukuru kampuni ya Swissport Tanzania ambao ndio waliofadhili ziara yake hiyo, na kuwaomba watanzania wengine kujitokeza kwa wingi kusaidia watoto yatima na wengine wanaoishi katika mazingira magumu. 

Ziara hiyo ya mrembo wa Taifa Lilian ilikuwa ni zawadi ya sikukuu za mwisho wa mwaka ambao ililenga kuwafariji watoto waliopoteza wazazi wao kwa namna moja au nyingine, na pia kutimiza Kauli mbiu ya mashindano ya urembo ya Miss Tanzania isemayo [Beauty with Purpose] Urembo na Malengo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »