* Mwekezaji wa Poland asema wataanza kujenga Januari, mwakani
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amekagua maghala ya kuhifadhia chakula yaliyopo Kizota nje kidogo ya mji
wa Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Alhamisi iliyopita
kwamba Serikali inalenga kujenga maghala kwenye mikoa sita kupitia mkopo
ambao itaupata kutoka Serikali ya Poland.
Akizungumza na viongozi wa mkoa
wa Dodoma pamoja na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo
asubuhi (Alhamisi, Novemba 6, 2014) wakati akikagua maghala hayo, Waziri
Mkuu alisema katika mkoa huo, Serikali ina nia ya kujenga maghala
makubwa (SILOS) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 za nafaka kwa
wakati mmoja.
“Tukipata maghala yenye uwezo wa
kuhifadhi tani 100,000 tutakuwa na uhakika wa kuchukua na akiba ya
nafaka kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Tabora na Manyara,” alisema.
Waziri Mkuu alifuatana na Bw.
WITOLD KARCZEWSKI ambaye ni mmiliki wa kiwanda kikubwa cha kusindika
nafaka nchini Poland ambacho Waziri Mkuu Pinda alikitembelea alipozuru
nchi hiyo Oktoba 24, mwaka huu. Bw. KARCZEWSKI anamiliki pia kiwanda
kinachotengeneza malighafi za kujengea SILOS.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri
Mkuu, Mkuu wa kituo cha NFRA Kanda ya Kati, Bw. Ruwaichi Mambali alisema
kituo hicho kina maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 30,000 lakini
kwa sasa kina tani 69,000 ambazo kati ya hizo tani 62,000 zipo Kizota
(Dodoma) na tani 7,000 ziko Manyoni (Singida).
Alisema eneo zima la Kizota lina
ukubwa ekari 33 na kwamba kuna maghala matatu yenye uwezo wa kuhifadhi
tani 10,000 kila moja. “Lakini kwa sasa tumelazimika kuweka mahindi
mengine na mtama hapa nje ambayo tumeyafunika kwa maturubali,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. KARCZEWSKI
alitaka kufahamu miundombinu iliyopo kwenye ghala la Kiszota ikiwemo
umabli wa kutoka barabara kuu pamoja na reli. Pia alitaka kujua eneo
zima lina ukubwa kiasi gani. Na alitaka kufahamu mbinu zinazotumika hivi
sasa kuhifadhi chakula kwenye ghala hilo.
Alisema wakipata michoro ya eneo
hilo (site map), atatuma wataalamu wake Januari mwakani waangalie
uwezekano wa kuanza ujenzi mapema iwezekanavyo pindi mazungumzo
yakikamilika.
Alhamisi iliyopita, wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya
kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius Nyerere akitokea Oman,
Waziri Mkuu alisema alikwenda Poland kutafuta msaada wa mfumo wa mkopo
wenye masharti nafuu ambao utasaidia kupambana na tatizo la uhaba wa
maghala kwa ajili ya kuhifadhia nafaka.
Alisema Serikali imelenga mikoa
sita ya kuanzia ambayo ni Ruvuma, Rukwa, Njombe (pamoja na Iringa)
ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mahindi. Pia inaangalia Kanda ya Ziwa
ambako mara nyingi wana uhaba wa chakula; na kwamba itaweka maghala
mkoani Dodoma kwa sababu ni katikati ya nchi ili ikusanye akiba kutoka
mikoa ya jirani ya Singida, Manyara na Tabora.
“Lengo ni kupata uwezo wa
kuhifadhi tani 700,000 hadi 1,000,000 na ujenzi wao siyo kama huu wa
kwetu. Tumewaomba watujengee SILOS (maghala makubwa) kwa sababu zina
teknolojia ya kujua kiasi gani cha nafaka kimeingia, zina unyevu kiasi
gani, unaweza kuweka dawa nafaka zako, kuosha na kukausha na kisha
ukasindika kwa kiwango unachotaka,” Waziri Mkuu aliwaeleza waandishi wa
habari.
Alisema uzalishaji mwaka huu
umetoa ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani 800,000 za mpunga
ikilinganishwa na ziada ya tani 300,000 iliyokuwepo mwaka jana.
“Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata soko la uhakika kwa mazao
ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya
Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake ni tani 240,000 tu
kwa mwaka,” alisema.
EmoticonEmoticon