JESHI la polisi Wilayani Kilindi
Mkoani Tanga linawatafuta watu wawili kwa tuhuma za kumuuwa mtoto wa jamii ya
wafugaji, Said Omar (19) na kisha maiti
yake kuitundika juu ya mti wa mkunazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda wa polisi
Mkoani Tanga, Fresser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea juzi sa 1 usiku
katika bonde la Kimbe kijiji cha Nyadigwa tarafa ya Kibirashi.
Alisema watu waliofanya kitendo hicho waliichukua maiti ya
mtoto huyo na kuining’iniza juu ya mkunazi kisha kutokomea kusikojulikana na hivyo polisi
inaendelea kufanya uchunguzi pamoja na kuwasaka wauaji hao.
“Tunaendelea kuwasaka waliohusika na taarifa za awali ni kuwa
wamekimbilia milimani na wamekuwa wakirejea majumbani kwao nyakati za
usiku----tuna uhakika tutawatia mbaroni” alisema na kuongeza
“Kitendo ambacho wamekifanya ni cha kikatili na hakikubaliki
katika jamii---tutahakikisha tunawatia mikononi na kuwafikisha katika vyombo
vya sheria” alisema Kashai
Akizungumzia kuhusu jamii kuishi kwa maelewano na
kushirikiana kwa kila jambo, kamanda Kashai aliwataka wafugaji na wakulima kuwa
na utaratibu wa kukutana kila baada ya mwezi mmoja kuzungumza changamoto
wanazokabiliana nazo.
Alisema jamii hizo
zinapaswa kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara kujadili na kuzungumza
changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo jambo ambalo litasaidia kuondosha vitisho vya
uhasama.
“Haya matukio ya ugomvi ugomvi wa wakulima na wafugaji tatizo
ni kuwa hakuna utaratibu wa kukutana na kujadili mambo yawahusuyo hasa mashamba
na mifugo” alisema
“Kama kungelikuwa na utaratibu huo katu tusingelisikia ugomvi
pande mbili hizi popote katika ardhi yetu ya Tanzania---hivyo natoa ushauri
Serikali za vijiji kuandaa mikutano hiyo nasi kama polisi tutaibariki” alisema
Kashai
Kamanda Kashai alisema mikutano hiyo polisi kwa kushirikiana
na vyombo vyengine vya usalama vitashirikiana na wakulima na wafugaji kuandaa
mikutano hiyo lengo likiwa ni kuleta mahusiano mema pande mbili hizo.
EmoticonEmoticon