MAKUBWA HAYA......WAZAZI WA MISS TANZANIA 2014 WAIBUKA KUDAI CHAO

November 21, 2014

Wazazi wa Miss Tanzania mpya, Lilian Kamazima wameitaka Kamati ya Miss Tanzania  iwape maelezo ya uhakika kuhusu zawadi na taji la binti yao kwa kuwa hadi sasa wako njiapanda.
 
Kauli hiyo ya  Eva na Deus Kamazima imekuja siku chache baada ya mrembo huyo kuwasili jijini Arusha akitokea Dar es Salaam.
Wakizungumza nyumbani kwao, Majengo Juu jijini Arusha jana, wazazi hao walionyeshwa kushangazwa na hatua ya kumpokea binti yao akiwa hana taji, pamoja na fedha ambazo alistahili kupatiwa kama mshindi.
Walisema kuwa walimpokea binti yao kama ‘yatima’, hata tiketi ya ndege alilazimika kulipiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwandago Investment Ltd, aliyemuibua katika ngazi ya Kanda ya Kaskazini.
“Tunaiomba Kamati ya Miss Tanzania itupe maelezo ya kina kuhusu zawadi, taji pamoja na vitu vingine kwa kuwa tumempokea binti yetu kama bila zawadi wala taji,” walieleza wazazi hao kwa nyakati tofauti.
Awali, mrembo huyo alisema kuwa pamoja na kwamba bado hajakabidhiwa taji wala zawadi yoyote na Kamati ya Miss Tanzania, lakini kitendo cha kupewa kiti hicho ameridhika.
“Sijapewa taji wala zawadi , lakini kitendo cha kupewa kiti cha umalkia nimeridhika,” alisema  Lilian.
Mkurugenzi wa  Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema kuwa ni kweli bado hawajamkabidhi fedha na zawadi  kwa kuwa kuna taratibu za kiofisi bado zinafanyika.
“Ni kweli, tulimwambia atuachie akaunti yake kwa kuwa kuna taratibu zinafanyika, tutamwekea pesa na kuhusu zawadi huyo alirithi taji, hakuwa mshindi wa kwanza, lazima mwelewe,” alisema Lundega.
 
edited by fredy mgunda

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »