Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
Serikali imezindua rasmi Mfumo
wa uboreshaji na kusaidia upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba kupitia
Mzabuni mmoja Mkoa wa Dodoma.
Uzinduzi huo umefanywa na Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Steven Kebwe katika sherehe
zilizofanyika leo mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali
wakiwemo wawakilishi kutoka Wilaya saba za Mkoa wa Dodoma.
Mhe. Dkt. Kebwe amesema kuwa
mfumo huo ni mzuri na utakuwa shirikishi kwani utahakikisha kuwa jamii
inapata mahitaji sahihi ya dawa na pia wanafanya wa sekta wanafanyakazi
kwa bidii kwa lengo la kupambana na upungufu wa dawa unaoweza
kujitokeza nchini.
Amesema kuwa moja ya vitu
vikubwa wanavyovifanya sasa ni kutekeleza sera ya Matokeo Makubwa Sasa
katika sekta ya afya kwani Barani Africa, Tanzania na Afrika ya Kusini
zimekuwa nchi zinazojitahidi kufuata mifumo mizuri ya dawa kutokana na
taarifa ya shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
“Mifumo hii itatusaidia na
kuboresha mahitaji ya dawa katika vituo vya afya, na hivyo kupunguza
vifo mbalimbali vinavyotokana na wananchi kutumia dawa na tiba ambazo
sio sahihi kwa sababu ya kukosa dawa katika vituo vya afya”, alisema
Mhe. Kebwe.
Hivyo Mhe. Dkt. Kebwe ameziagiza
Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha zinatekeleza mfumo kwa
ufanisi ili mikoa mingine ije kujifunza kutoka kwao kwa ajili ya
kusaidia kupunguza upungufu wa dawa na vifaa vya tiba hapa nchini.
Amesema kuwa wananchi wanakwenda
katika vituo vya afya wanapenda wakute huduma nzuri na za kuridhisha
huku wakipata dawa na huduma nyingine za upimaji kwa gharama nafuu.
Aidha, Mhe. Dkt. Kebwe amefafnua
kuwa, sasahivi wameamua kuja na mfumo huo kwa kuwa utasaidia sana
kuboresha afya za wananchi na kutekeleza malengo ya Minelia.
Ameongeza kuwa Serikali
itaendelea kujipanga zaidi katika kufundisha na kuelekeza watumishi
na kutengeneza mifumo mipya ambapo kwa ajili ya kusogeza huduma karibu
na wananchi kulingana na bajeti.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.
Rehema Nchimbi ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa msaada mkubwa kwa
Tanzania hasa mkoani Dodoma katika Wilaya husika kwani utasaidia
kuboresha afya za wakazi wa Dodoma.
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa
anaamini kuwa mfumo huo utasimamia na kutekelezwa kama ilivyopangwa ili
mikoa mingine ipate kuja kujifunza kupitia mkoa wa Dodoma.
“Naomba Mhe. Mgeni rasmi wakati
tunasherehekea Uzinduzi huu, tuombe tupate mwongozo kwa udhibiti wa dawa
zinazosambaa kwa kasi kupitia vyombo vya habari”, alisema Mhe. Nchimbi.
Mfumo huo utatoa fursa kwa Duka
la Dawa la Bahari Limited kuzindua mfumo wa usambazaji wa dawa na vifaa
tiba katika vituo vya afya na Hospitali katika Wilaya zote saba za mkoa
wa Dodoma.
Duka hilo limepewa jukumu hilo
baada ya kushinda zabuni na hivyo linatarajiwa kupata fedha zake kupitia
Mfuko wa Afya ya Jamii, Mfuko wa Bima ya Afya na vyanzo mingine vya
Halmashauri za Wilaya zote.
Mfumo huo ni wa kwanza kuanza kutekelezwa hapa nchini na kwa majaribio umeanzia mkoani Dodoma chini ya mradi tuimarishe Afya.
EmoticonEmoticon