NCHI NANE KUCHUANA MICHUANO YA KIMATAIFA YA MCHEZO WA WUSHU DAR ES SALAAM.

August 17, 2014
NA ELIAS KIMARO,DAR ES SALAAM.
NCHI nane zikiwamo za China, Kenya, Iran na wenyeji Tanzania inatarajiwa kuchuana katika michuano ya kimataifa ya mchezo wa Wushu itakayofanyika kati ya Agosti 30-31 jijini Dar es Salaam.
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Wushu Tanzania (TWA), Sempai Golla Kapipi ameiambia TANGA RAHA kuwa, michuano hiyo itafanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja na Tanzania kuanzia saa 4 asubuhi.

Sempai Kapipi alisema wenyeji Tanzania itawakilishwa na klabu 23 na wachezaji wengine mmoja mmoja dhidi ya wawakilishi wa nchi za Kenya, Uganda, Iran, China, Libya, Nigeria na Zimbabwe.

"Nchi zilizothibitisha mpaka sasa kushiriki michuano hiyo ni majirani zetu wa Kenya na Uganda, Iran, China, Zimbabwe, Nigeria na Libya na wenyeji Tanzania itakayowakilishwa na klabu 23," alisema.

Katibu huyo alifafanua kuwa katika michuano hiyo kutakuwa na mitindo miwili itakayoonyeshwa kupitia mchezo huo maarufu kama Kungfu ya Sanda na Tai-ru itakayohusisha mapigano ya mapanga.

Sempai Kapipi alisema kuwa wapo katika mipango ya kuwaalika wanamichezo wa judo, karate na ngumi ili kuonyesha manjonjo yao.

Hii ni mara ya pili kwa chama hicho kuandaa michuano mikubwa ya mchezo huo baada ya awali kuandaa michuano ya taifa iliyohusisha klabu pekee za Tanzania iliyofanyika Ufukwe wa Coco mwaka 2011.

Naye Mkurugenzi wa mashindano wa chama hicho, Karama Masoud 'Karapina' alisema maandalizi yanaendelea vyema na wawakilishi wa nje ya nchi na klabu za mikoa mbalimbali wataanza kuwasili wiki ijayo.

"Kila kitu kimekaa vema na tutaanza kupokea wageni ndani ya wiki ijayo, hadi siku ya kuanza kwa michuano tunaamini wawakilishi wote watakuwa wameshawasili jijini Dar es Salaam," alisema Kalipina.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »