DC MAKUNGA :SERIKALI WILAYANI HAI IMEJIPANGA KUONDOA KERO ZINAZOWAKABILI WANANCHI

August 17, 2014

Na Mwandishi Wetu,Hai

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga(Pichani) ameeleza kuwa serikali wilayani humo imejipanga kuondoa kero zote zinazoawakabili wananchi wanapoenda kutibiwa katika hospitali ya serikali ya wilaya hiyo zikiwemo lugha chafu za watumishi wa hospitali hiyo

Mhe.Novatus Makunga ametoa kauli hiyo katika mikutano yake ya hadhara na wananchi wa mitaa ya Kingereka na Kibaoni katika kata ya Hai Mjini.

Awali wananchi wa mitaa hiyo walieleza kuwa kero kubwa wanayokumbana nazo katika hospitali hiyo ni pamoja na lugha chafu katika eneo la mapokezi,ukosefu wa dawa pamoja na madaktari kutokaa katika vyumba vyao vya kuwahudumia wagonjwa.

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwemo kuanzisha mpango unaojulikana kama sauti ya jamii ambapo kupitia mpango huo wananchi wanaokumbana na kero katika hospitali hiyo wamekuwa wakitoa taarifa.

"Taarifa hizo zimekuwa zikijadiliwa na kamati ya uongozi ya hospitali hiyo kila mwezi na kuchukuwa hatua na baadaye mrejesho kutolewa kwa wananchi,hivyo zote kwa pamoja tupambane na uvunjaji wa maadili katika hospitali yetu" alisema Makunga

Aidha amewataka wananchi hao kutoa taarifa mara moja pale wanapokumbana na kero yoyote kwa mganga mkuu wa wilaya ama mganga mfawidhi ama muuguzi mkuu na hata yeye kama mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ambapo wote hao walitoa nambari zao za simu za mkononi.

“Tumeanza kuchukuwa hatua na itakuwa vyema pale unapokumbana na kero kutuletea taarifa hapo hapo bila ya kuchelewa,sasa wakati umefika wa kuambiana ukweli,kama mtu anaona kuhudumia umma kunampotezea wakati basi akaanzishe zahanati yake ambapo huko atakuwa huru kutumia lugha chafu,”aliongeza Makunga

Ameeleza maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika hospitali hiyo hayatakuwa na maana endapo kero hizo zitaendelea kudumu na kusababisha wananchi kupata huduma kwa mateso makubwa.

Makunga amezitaja huduma zilizoboresha kuwa ni pamoja na upasuaji mkubwa kwa kuwa na chumba cha kisasa,ukamilishaji wa wote ya upasuaji pamoja na kukamilishwa kwa huduma za X-Ray ambayo itafunguliwa rasmi na mwenge wa uhuru mnamo tarehe 22 ya mwezi huu

Kwa upande wake mganga mfawidhi wa wilaya ya Hai,Dk Fanuel Mollel alikiri kwamba huko nyuma kulikuwa na tatizo kubwa la madaktari wa hospitali hiyo kutumia muda mrefu kwenda kunywa chai kwa kutoka pamoja kwa makundi na hivyo kusababisha wagonjwa kusota kwa muda mrefu.

Amesema hatua za kudhibiti tabia hiyo zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kantini eneo la hospitali hiyo.

Kuhusiana na upungufu wa dawa ameeleza hali hiyo inatokana na taratibu za serikali ambapo kwa sasa zinataka dawa ziagizwe kutoka katika bohari kuu ya madawa(MSD) ambapo mara nyingine ukumbwa na upungufu wa dawa

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »